Hujuma dhidi ya CHADEMA nje


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 02 February 2011

Printer-friendly version
Zitto kung’olewa rasmi
Zitto Kabwe

MRADI wa vyama vitatu vya upinzani nchini unaolenga kupunguza nguvu za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) bungeni, huenda ukakwama.

Habari zinasema tayari wabunge wa vyama hivyo kupitia kile kinachoitwa, “Umoja wa kambi isiyorasmi bungeni,” wamewasilisha kwa spika wa Bunge, maombi ya kutaka kubadilishwa kwa kanuni za bunge.

Wabunge wa NCCR-Mageuzi, Chama cha Wananchi (CUF) na United Democratic Party (UDP), wanataka kanuni zibadilishwe ili kuondoa neno “rasmi” katika uwakailishi wa upinzani bungeni.

Hivi sasa kanuni zinatambua kile kinachoitwa “kambi rasmi ya upinzani” inayoongozwa na chama chenye wabunge wengi kuliko kingine chochote katika upinzani au kilichofikisha asilimia 12 ya wabunge wote.

Kiu ya wabunge wa vyama vitatu ni kuondoa neno “rasmi,” ili na wao waweze kutambuliwa na hata kupewa uongozi wa kamati muhimu za bunge.

Kamati ambazo wanapigania, ni Kamati ya Hesabu za Serikali, Kamati ya Hesabu ya Mashirika ya Umma na Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa.

Kwa mujibu wa kanuni za bunge za sasa, kamati zote hizi zimekuwa zikiongozwa na upinzani ili kuchochea jicho makini na kutoa changamoto kwa serikali.

Viongozi wa kamati hizo muhimu wanachaguliwa katika Kamati za Kudumu za bunge, lakini sharti watoke miongoni mwa wabunge wa kambi rasmi.

Mara hii, Hamad Rashid ambaye amekuwa kiongozi wa kambi rasmi bungeni, akishirikiana na John Cheyo (UDP) na David Kafulila (NCCR-Mageuzi), wanataka mabadiliko katika kanuni ili wasikose uongozi wa kamati hizo.

Wiki mbili zilizopita, viongozi wa vyama hivyo walijitambulisha kwa waandishi wa habari kuwa wao ni “kambi isiyo rasmi” bungeni; laki Spika Anna Makinda aliwajibu siku iliyofuata kuwa wanachotaja hakimo katika kanuni na kwamba hakiwezi kuruhusiwa.

Spika Makinda alisema kambi isiyorasmi ambayo wanatafuta akaina Hamad, inapingana na mfumo wa mabunge ya Jumuiya ya Madola na kwamba haikubaliki.

“Siyo kwamba akina Hamad wanatafuta kuungwa mkono; tayari wameandika barua kwa spika. Wanataka kanuni za bunge zibadilishwe ili wao waweze kuongoza kamati hizo,” anasema mbunge mmoja wa CCM ambaye ni waziri.

Mabadiliko ambayo Hamad na wenzake wanataka yafanyike yanahusu kanuni ya 113 (11) inayotoa ruhusa kwa kambi rasmi ya upinzani kuongoza kamati hizo.

Mtoa taarifa wa MwanaHALISI anasema, kazi ya kubadilisha kanuni hizo imekuwa ngumu kwa sababu mbili kubwa.

Kwanza, “Spika Makinda ana hofu kuwa kukubaliana na matakwa ya Hamad na wenzake kunaweza kumshushia hadhi aliyojingea mbele ya serikali na chama chake.

Anasema, “Sikiliza kijana. Ni majuzi tu, CHADEMA wamelalamika kunyang’anywa nafasi ya umeya kule Arusha. Sasa ukiwanyang’anya na hiki kidogo walichopata, lazima watapiga kelele na umma utawasikiliza. Sidhani kama chama chetu kitakuwa tayari kufika huko,” anasema waziri mmoja mwandamizi katika serikali ya Rais Jakaya Kikwete.

Pili, mtoa taarifa anasema, “Neno kambi rasmi liliwekwa ndani ya kanuni za sasa, kwa shinikizo la Hamad Rashid wakati wa kuunda kanuni hizi mpya. Alifanya hivyo ili kuzuia wenzake kutoka nje ya kambi rasmi kuongoza kamati hizi.”

Inaelezwa kwamba Hamad alitaka kuwekwa kwa kifungu hicho kwa kuwa aliamini kuwa chama chake ndicho kitakachoongoza upinzani bungeni kwa kuwa kina mtaji wa kutosha visiwani Pemba.

Kilichosababisha Hamad kushinikiza kuandikwa neno rasmi kulikuja kufuatia hatua ya mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo kumshinda Hamad mwaka 2005.

“Wakati ule CUF ilikuwa inaunda kambi rasmi ya upinzani bungeni peke yake. Cheyo akaenda kugombea nafasi ya mwenyekiti wa PAC. Akamshinda Hamad ndani ya kamati. Sasa ilipoundwa kamati ya kanuni kuangalia kanuni mpya, Hamad akasisitiza kuwekwa kwa neno hili rasmi,” anasema mbunge mmoja ambaye alikuwa mjumbe wa kamati ya kanuni.

Anasema, “Hamad anataka kuongoza kamati ya hesabu za mashirika ya umma, huku Cheyo akitaka kamati ya hesabu za serikali. Nashangaa kwa nini hawaamini kuwa CHADEMA ina uwezo huo. Huu ni ubinafsi.”

Haikufahamika mara moja, mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), Kafulila ambaye amekuwa bega kwa bega na Hamad Rashid kutaka kuunda kambi yao, anataka kushika nafasi ipi.

MwanaHALISI lilipowasiliana na Mnadhimu wa upinzani bungeni, mbunge wa Singida Kusini Mashariki, Tundu Lissu kujua iwapo anafahamu mradi wa CUF na wenzao, haraka alisema, “Siyo tunaufahamu, tunaujua fika.”

Hata hivyo, Lissu ambaye ni wakili wa mahakama kuu alisema, “Tunafahamu vilevile kuwa huko ni kuvunja misingi ya bunge la jumuiya ya madola.”

Anasema, “Bunge la Jumuiya ya Madola linataka chama kinachoshika nafasi ya pili, ndicho kinachokuwa chama rasmi cha upinzani bungeni; na kwa msingi huo, ndicho kinachostahili kusimamia serikali.”

Kuhusu hoja ya kushirikiana na vyama vingine, Lissu alisita kuwa wazi, lakini alisema hilo linajadilika, ikiwa ni pamoja na CUF kuweka wazi uhusiano wake na CCM.

“Hata wewe unajua. Huku CUF ni chama cha upinzani na kule Zanzibar ni chama kilichoko serikalini. Hapa tunahitaji kuelewana. Au wewe huoni hilo?” aliuliza.

Taarifa zilizopatikana tukienda mtamboni zinasema uongozi wa CHADEMA unataka kufanyika kwa majadiliano ya viongozi wakuu wa vyama.

Akizungumzia taarifa zilizoandikwa na gazeti la Mwananchi la Jumapili iliyopita kuhusu mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kurejeshwa katika nafasi ya naibu kiongozi wa upinzani, Lissu alisema, “taarifa hizo hazina ukweli.”

Alipoulizwa ukweli ukoje, Lissu alisema, “Ukweli ni kwamba suala hilo limekwisha. Suala la Zitto halikuwa sehemu ya ajenda na hivyo halikujadiliwa na Kamati Kuu (CC) ya CHADEMA.”

Anasema CC iliyokutana Desemba mwaka jana ilibariki uamuzi wa kumvua Zitto nafasi ya naibu kiongozi wa upinzani bungeni na kusema, “Kilichofanywa na wabunge hakihusu CC.”

Alipotakiwa kueleza kama CC haikujadili suala la Zitto kurejeshewa nafasi yake, msimamo wa wabunge kwa sasa ukoje, Lissu alisema, “Ni kujaza nafasi.”

Alisema, “Tunakwenda Dodoma. Huko tutafanya uchaguzi na tutajaza nafasi yake.”

Desemba mwaka jana wabunge wa CHADEMA walimuondoa Zitto katika nafasi ya naibu kiongozi wa upinzani bungeni kwa tuhuma za kupingana na msimamo wa wabunge na chama kwa jumla na akutangaza msimamao wake kataika vyombo vya habari.

Aidha, Zitto alikuwa miongoni mwa wabunge wachache waliokacha msimamo wa wenzao wa kutoka bungeni wakati Rais Kikwete akizindua bunge la kwanza baada ya uchaguzi.

Kwa muda sasa, Zitto amekuwa akilaumiwa kwa kuwa na mahusiano na Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Usala wa taifa (TISS), Jack Zoka na mbunge wa Igunga na mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Rostam Aziz.

0
Your rating: None Average: 4.3 (4 votes)
Soma zaidi kuhusu: