Hukumu ya Makamba: Makamba, Londa washiriki Rushwa


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 04 August 2009

Printer-friendly version
Mbunge Halima Mdee

MwanaHALISI ndilo gazeti pekee ambalo liliandika na kung'ang'ania ufuatiliaji wa madai ya Mbunge Halima Mdee

Kwamba Yusufu Makamba, aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa sasa wa CCM na mbunge wa kuteuliwa; na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Salum Salehe Londa, walishiriki katika vitendo vya rushwa kuhusiana na uuzaji wa viwanja viwili vya Kawe Ukwamani, Dar es Salaam. Ufuatao ni uamuzi wa Spika wa Bunge, Samuel Sitta kuhusu sakata hilo alioutoa katika mkutano wa bunge uliomalizika mwishoni mwa wiki.

UTANGULIZI

Chimbuko la Malalamiko

Waheshimiwa Wabunge, uamuzi wangu wa leo unatokana na malalamiko yaliyowasilishwa kwangu na Mheshimiwa Yussuf Rajab Makamba, (Mb) (ambaye katika Uamuzi huu ataitwa Mlalamikaji wa Kwanza) na Mheshimiwa Salum Salehe Londa, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni (Mlalamikaji wa Pili), dhidi ya kauli ya Mheshimiwa Halima James Mdee (Mb), (Mlalamikiwa) aliyoitoa Bungeni tarehe 7 Agosti, 2008 wakati akichangia Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2008/2009.

Pamoja na mambo mengine, Mheshimiwa Halima James Mdee, (Mb), alitoa madai kwamba

  1. Mheshimiwa Yussuf Rajab Makamba (Mb) akiwa Mkuu na Mkoa wa Dar es Salaam alimlinda Mstahiki Meya Salum Londa kwenye sakata la uuzaji wa Viwanja Na. 695 na 696 vilivyopo Kawe Ukwamani;
  2. Mheshimiwa Yussuf Makamba na Mstahiki Meya Salum Londa walishiriki kwenye vitendo vya rushwa kuhusiana na uuzaji wa Viwanja hivyo; na
  3. Watendaji wa Halmashauri walihamishwa ili kuficha ukweli wa mambo hayo.

Kutokana na kauli ya Mheshimiwa Halima Mdee, (Mb), Mheshimiwa Yussuf Rajab Makamba, (Mb), na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Mhe. Salum Londa kwa nyakati tofauti, waliwasilisha malalamiko yao kwangu. Mheshimiwa Yussuf Rajab Makamba alikanusha taarifa iliyotolewa na Mheshimiwa Halima James Mdee (Mb) kuhusu Viwanja Na. 695 na 696 na kuniomba nichukue hatua ili Mheshimiwa Halima Mdee athibitishe madai yake.

Mheshimiwa Salum Salehe Londa naye alikanusha tuhuma zilizotolewa dhidi yake na kuniomba nichukue hatua ili Mheshimiwa Mdee, (Mb), aliyedai kuwa amemkashifu kwa kulitumia Bunge, athibitishe madai yake na akishindwa kufanya hivyo amwombe radhi vinginevyo atamchukulia hatua nyingine za kisheria.

Baada ya kupokea malalamiko hayo, niliyapeleka kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa mujibu wa Kanuni ya 71(1) na (2) na Kanuni 4(1) (b) ya Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Bunge Toleo la 2007, ili iyafanyie uchambuzi na kutoa mapendekezo.

Tarehe 31 Disemba, 2008, kabla ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge haijaanza kazi ya kusikiliza shauri hili, nilipokea barua kutoka kwa Mlalamikaji wa Kwanza akiomba kuyaondoa malalamiko yake na kutoa sababu kuwa amekwishayasahau machungu aliyoyapata kutokana na kauli ya Mlalamikiwa.

HOJA KUHUSU MALALAMIKO HUSIKA

Hoja ya Msingi

Hoja ya msingi katika suala hili ilikuwa ni kuthibitisha iwapo madai yaliyotolewa na Mlalamikiwa Bungeni, tarehe 7 Agosti, 2008 dhidi ya Walalamikaji hayakuwa ya ukweli.

Mahojiano ya Kamati na Mlalamikaji wa Pili na Mlalamikiwa

Alipoitwa mbele ya Kamati, Mlalamikaji wa Pili alikanusha madai yote yaliyotolewa Bungeni na Mlalamikiwa na kusisitiza kuwa, mchakato mzima wa umilikishwaji wa Viwanja Na. 695 na 696 ulifanywa na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kisheria.

Aidha, katika kuthibitisha maelezo yake aliwasilisha vielelezo mbalimbali vilivyohusika na umilikishwaji wa viwanja husika.

Mlalamikiwa naye alipoitwa mbele ya Kamati, alisisitiza kuwa, kauli aliyotoa Bungeni ni ya ukweli, hawezi kuifuta na hataomba radhi kwa Mlalamikaji wa Pili na katika kuthibitisha madai yake, aliwasilisha nyaraka mbalimbali za kuonesha na kuthibitisha maelezo yake aliyoyatoa Bungeni.

Kamati ilibaini pia kuwa, Taarifa iliyoandaliwa na Wataalam wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi kuhusu sakata la viwanja 695/696 vya Kawe ilihusisha baadhi ya Maafisa waliosababisha tatizo lenyewe na hivyo ikawa haina uzito.

Kujitoa kwa Mlalamikaji wa Pili

Tarehe 17 Januari, 2009 baada ya Kamati kupokea maelezo na ushahidi wa mdomo na nyaraka kutoka kwa Mlalamikaji wa Pili na Mlalamikiwa, nilipokea barua kutoka kwa Mlalamikaji wa Pili naye akiniarifu kuwa anaondoa malalamiko yake.

Baada ya kujitoa kwa Walalamikaji wote wawili, Kamati ilikamilisha kazi yake kwa hatua waliyoifikia na kuwasilisha taarifa yake yenye mapendekezo yake kwangu.

UAMUZI WA SPIKA

Baada ya kuzingatia taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na hususan ushauri walioutoa kuhusu suala hili, na kwa kuelewa hali halisi kwamba, Walalamikaji wote wawili walijiondoa katika kuendeleza malalamiko yao dhidi ya Mlalamikiwa, nimeridhika kwamba, Mheshimiwa Halima Mdee (Mb) halazimiki kuyafuta madai yake aliyoyatoa Bungeni tarehe 7 Agosti, 2008 wala kuwaomba radhi Bungeni Waheshimiwa Yusuph Makamba na Salum Londa.

Kwa hiyo maelezo aliyoyatoa Bungeni Mheshimiwa Halima Mdee tarehe 7 Agosti, 2008 yanabaki kama yalivyo.

Naishukuru Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, kwa kufanya kazi kwa umakini mkubwa na kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za Bunge, katika kulishughulikia suala hili.

Waheshimiwa Wabunge, nahitimisha kwa kusema kuwa, kwa taratibu za kibunge, suala hili limefikia mwisho wake.

Uamuzi huu nimeutoa leo tarehe 31Julai, 2009

Samwel J. Sitta
SPIKA

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: