Huu sasa ni mgogoro wa kikatiba


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 19 August 2008

Printer-friendly version

KAMA kuna kitu kinachokera mno viongozi wakuu wa serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa sasa, basi kuendelea kwa mjadala unaohusu nafasi ya Zanzibar kimuungano kunaongoza.

Mjadala wa suala hili umepamba moto, hali inayotokea licha ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kusema wanasheria wakuu wa serikali wa pande mbili za Muungano, watatafuta ufumbuzi.

Waziri Mkuu aliliambia Bunge Julai kwamba wanasheria wakuu watatoa tafsiri ya yale yanayotamkwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 ambayo yeye aliyasoma tu alipokuwa anajibu swali la mbunge wa Chwaka, Yahya Kassim Issa wa CCM.

Alichokisema Waziri Mkuu ni kwamba Zanzibar si nchi bali sehemu ya Jamhuri ya Muungano. Kinachoonekana sasa, ni hali ya mtafaruku ulioibuka na kugawa Watanzania.

Viongozi wakuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ambao wote ni makada wa CCM, wanaunga mkono msimamo wa kwamba Zanzibar ni nchi yenye mamlaka yake kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano. Kwao, Zanzibar, kwa kuwepo Rais, Baraza la Wawakilishi, Mahakama, Nembo, Bendera na Wimbo wa Taifa, ni nchi kamili.

Msimamo huu unasisitizwa kila pale itokeapo Mtanzania wa upande wa Bara, amesema vinginevyo.

Kwa hivyo, habari ndiyo hiyo: SMZ na Wazanzibari wamesimama vilivyo kwa imani hiyo na wameacha – labda kwa muda – mgawanyiko mkubwa wa kiitikadi uliojengeka na kuzidi kulelewa na mfumo wa utawala wa Tanzania na kujumuika katika kutetea wanayoiita “nchi” yao.

Lipo tatizo kubwa katika Jamhuri kuhusu suala hili muhimu kwa mustakbali wa Taifa lililotokana na kuunganishwa kwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar iliyokuwa chini ya uongozi wa Mzee Abeid Amani Karume na Jamhuri ya Tanganyika iliyokuwa chini ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Naona viongozi wakuu wa Serikali ya Muungano (SMT) pamoja na wa CCM walioko Bara, wamepatwa na mshtuko mkubwa kuona matamko ya Waziri Mkuu yaliyosaidiwa na Spika wa Bunge, Samuel Sitta, aliyepiga marufuku suala hilo kuendelea kujadiliwa bungeni, hayajafanikiwa kusimamisha mjadala.

Lakini viongozi hawa wanaumia zaidi wanapoona kelele zinakuwa nyingi kiasi cha kutisha kila Mtanzania wa Bara anapotilia mkazo msimamo wao kwamba Zanzibar si nchi.

Wakati wanadhani ni faraja akitokea Mtanzania wa Bara; akiwemo mbunge, na hata Zanzibar – kama alivyojitokeza Mwanasheria Mkuu wa zamani wa SMZ, Hamidu Mbwezeleni na kada mkuu wa CCM na mbunge wa Donge, Ali Ameir Mohamed – na kutoa matamshi yanayounga mkono msimamo wa viongozi wakuu upande wa Bara, kumbe mtafaruku unazidi.

Mtafaruku huzidi kwa sababu majibu ya matamshi hayo yakitoka upande wa Zanzibar, yanakuwa machungu isivyoweza kuelezeka. Ni machungu kiasi kwamba yanazidisha kuweka majaribuni mustakbali wa Taifa.

Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe aliamua kuingia kwenye ngoma wiki iliyopita. Alipokuwa bungeni akijadili hoja ya makadirio ya matumizi ya Wizara ya Sheria na Katiba, alitonesha vidonda walivyonavyo Wazanzibari tangu kuambiwa kuwa yao si nchi bali “sehemu ya Jamhuri ya Muungano.”

Ni kama vile daktari huyu wa sheria hakusoma alama za nyakati kabla ya kueleza alichokieleza kuhusu suala hilo. Alikuwa bado akiamini Ali Juma Shamhuna alitoa kauli binafsi kwenye Baraza la Wawakilishi aliposema Zanzibar ni nchi tena itabaki hivyo na wala hakuna Mzanzibari atakayekubali kutishwa maana “wakati wa kutishana umepita.”

Dk. Mwakyembe ambaye kaka yake amefikia ngazi ya Naibu Katibu Mkuu katika SMZ, baada ya kushikilia msimamo unaowapendeza viongozi wakuu wa CCM Bara, alimshambulia Shamhuna, mwakilishi Donge, jimbo atokalo pia Ali Ameir Mohamed, ambaye maelezo yake kwenye gazeti moja kuhusu suala hilohilo, bila ya shaka hayajawakera viongozi hao kwa namna alivyoyapangilia kwa ustadi mkubwa.

SMZ ilishatoa msimamo kuhusu suala hilo. Zaidi ya kauli aliyowahi kuitoa Shamhuna ambaye mbali na kuwa Waziri wa Habari, pia amevikwa wadhifa wa unaibu Waziri Kiongozi, msimamo huo ulisisitizwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Kiongozi, Hamza Hassan Juma, mwakilishi wa Kwamtipura.

Lakini kwa sababu wanaona ni kama vile “heshima haipo” juu ya mamlaka ya Zanzibar, SMZ wamemtuma tena waziri huyo kijana na mpya kabisa ndani ya Baraza la Mawaziri, Hamza, kutunisha misuli ya SMZ.

Hakika matamshi ya safari hii ni makali zaidi ambayo hapana shaka yataendelea kuwapa CCM Bara fundisho kubwa na kuwasukuma katika tafakuri mpya juu ya kile wanachokusudia kukifanya.

Kwa vile Dk. Mwakyembe alimtaka Shamhuna akome na kuhimiza aadabishwe na CCM, Hamza naye amemtaka Dk. Mwakyembe aombe radhi viongozi wa SMZ na wananchi wa Unguja na Pemba kwa “kuwadharau.”

Nikope sehemu ya tamko hili la 16 Agosti. “Kauli ya Mwakyembe ni ya uchochezi yenye lengo la kugonganisha viongozi na yenye kugawa wananchi… matamshi (yake) yamevuka mipaka na ameonyesha jeuri na dharau dhidi ya SMZ na kumtaka aombe radhi mawaziri wa SMZ kwa utovu wa nidhamu aliowafanyia.”

Kauli nzito ambayo naamini huenda viongozi wakuu wa Bara hawakuitarajia ni Hamza anaposema, “Mawaziri wa Zanzibar hawawajibiki kwa Waziri Mkuu wala kwa Bunge bali wanawajibika kwa Waziri Kiongozi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.”

Mwanasheria Mbwezeleni anataka Mahakama ya Katiba itumike kutafuta ufumbuzi badala ya kutumia wanasheria wakuu wa serikali. Anasimama kwenye makubaliano ya Muungano.

Msomi mwenzake wa sheria, Profesa Issa Shivji, anaamini ufumbuzi unahitaji hatua za kisiasa zaidi kuliko kisheria. Anataka majadiliano ya viongozi wa pande mbili yatumike kupata ufumbuzi huku akishurutisha kuwa muungano ubaki ila kwa wananchi wenyewe kuachiwa kuamua.

Mjadala wazi anaopendekeza Profesa Shivji, si chaguo la haki kwa CCM ambayo kada wake mwandamizi, Ali Ameir Mohamed, anasema sera yake ni Muungano wa serikali mbili si vinginevyo. Na huu ndio msimamo wa CCM tangu enzi za Mwalimu Nyerere.

Kadhalika, matumizi ya Mahakama ya Katiba, haionyeshi kuridhi viongozi wa CCM na hadi sasa hakuna taarifa za kuwepo mawasiliano ya wanasheria wawili wa serikali kama ilivyoahidiwa na Waziri Mkuu. Ina maana Watanzania wanalazimishwa kuendelea kusubiri kabla ya kupata msimamo.

Ni dhahiri Taifa linakabiliwa na utata ambao sasa unajengeka kuwa mgogoro wa kikatiba kuhusu muungano ulioasisiwa na wale wazee wawili, Mwalimu na Mzee Karume tangu 26 Aprili, 1964.

Lakini wahenga walishasema, “mficha maradhi kilema kitamuumbua” na wakasema “asiyesikia la mkuu huvunjika guu” kama walivyosema “usipoziba ufa utajenga ukuta.” Lazima kujenga ukuta maana viongozi walidharau makusudi kuziba ufa.

0
No votes yet