Huyu anajua ‘machungu’ ya Rostam


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 20 July 2011

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki

HATIMAYE Rostam Adulrasul Aziz ameandika historia. Ni kwa kujiuzulu nafasi zake zote ndani ya chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hii ni baada ya miezi mitatu ya malumbano kati yake na baadhi ya wajumbe wapya wa sekretarieti ya CCM.

Kwa wale tuliobahatika kuwa ndani ya sakata zima la kupanda na kushuka kwa Rostam, hatutakuwa tumetenda haki tusipoeleza kilichojiri mpaka kuanguka kwake.

Ni vema tukaeleza haya ili kuipa historia nafasi yake; lengo likiwa kufanya umma uelewe nini kilijiri.

Rostam alikuwa rafiki wa muda mrefu wa Edward Lowassa. Ni wazi pia alikuwa rafiki wa Rais Jakaya Kikwete. Sina uhakika ni nini kilimfanya Rostam awe karibu na Kikwete kuliko Lowassa katika miaka ya 2002 hadi 2005.

Rostam alikuwa na mapenzi ya kweli na Kikwete; alidhihirisha mapenzi yake hayo mwaka 2002 pale palipotokea mivutano ndani ya mtandao iliyohusu nani hasa awanie nafasi ya urais kati ya Kikwete na Lowassa.

Wakati huo ilikuwa ikinong’onwa na kuripotiwa kuwa Lowassa alikuwa na nguvu kubwa ndani ya chama kuliko Kikwete.

Wengi walimuona Kikwete kuwa mtu wa matukio mepesi kama vile kukaa na wazee na kula nao, ili kujionyesha kuwa yeye ni “mtu wa watu” mwenye uwezo wa kuishi maisha kama yao.

Hatimaye baada ya ushawishi mkubwa wa Rostam, wakati wa mkutano wa bunge la bajeti mwaka 2003, ndipo Lowasa alipokubaliana na matakwa la Rostam.

Aliwaita wazee nyumbani kwake, wakuu wa mikoa 14 na watu wengine maarufu waliokuwa wanamuunga mkono na kuwatangazia rasmi kuwa hatogombea tena urais. Aliekeza wafuasi wake kuhamishia nguvu zao kwa Kikwete.

Hili halikuwa jambo rahisi. Baadhi ya wafuasi wake waligoma hadi kufikia wengine kuamua kukaa pembeni.

Miongoni mwa waliokaa pembeni ni Anne Makinda na Abdulrahman Kinana. Ila Kinana inadaiwa alijiondoa baada ya kuona wenzake ndani ya mtandao wanachafua wagombea urais wengine.

Kilichofuata ikawa kutafuta uungwaji mkono ndani ya chama. Kwa nguvu ya Rostam na Lowassa hili lilifanikiwa, huku Umoja wa Vijana (UV-CCM) ukiwa ndiyo nguzo kuu ya kusimamia kampeni za Kikwete.

Vijana waliotapakaa nchi nzima walianza kazi ya kumwita Kikwete kwenye matamasha mbalimbali kwa lengo la kumjenga kisiasa.

Baada ya hilo kukamilika, likaingia zoezi Na. 2 ambalo ni Rostam kutafuta njia ya kujipenyeza katika maeneo nyeti ya dola ili kuwaaminisha kuwa Kikwete anafaa.

Hilo lilifuatiwa na kampeni ya chinichini na wazi na upikaji taarifa, nyingine za “kiintelijensia” ili kuonyesha Kikwete ana nguvu isiyoweza kuzuilika.

Hatimaye, hata Rais Benjamin Mkapa akashawishika kumuunga mkono Kikwete.

Rostam alipiga hesabu za haraka na kugundua kitendo cha kupiga kura tatu kwa mgombea mmoja kilikuwa hatari kwa Kikwete.

Ni baada ya kubaini Frederick Sumaye, Profesa Mark Mwandosya, Dk. Abdallah Kigoda na Dk. Salim Ahmed Salim kuungana ili wafuasi wao wapigiane kura.

Kitendo cha wafuasi wa Kikwete kumpigia kura yeyote kwa kupitia utaratibu wa kura tatu, kama ulivyoelezwa kwenye kanuni za uchaguzi za CCM, kilikuwa kinakamilisha safari ya kushindwa kwake maana angekuwa anaongezea wenzake ushindi, huku yeye akibaki na kura chache.

Katika uchaguzi huo, kati ya kura zaidi ya 215 zilizopigwa, Kikwete alipata kura 76 tu.

Kwa maana nyingine, ilibidi kumshawishi Mkapa kupindisha kanuni za uchaguzi. Ghafla Mkapa akatangaza mtu “mmoja kura moja.”

Huu ukawa ushindi mwingine wa Kikwete uliotengenezwa, kurabatiwa na kuandaliwa na au kwa msaada wa Rostam.

Uchaguzi mkuu ulikuwa mwepesi kwa kuwa kazi zote za chini zilifanywa na Rostam ambaye aliongoza timu kubwa ya wapiga kampeni waliotapakaa nchi nzima.

Mathalani, mimi nilikuwa nikiongoza kundi la watu tuliokuwa tukipokea maelekezo kutoka kwa Rostam moja kwa moja.

Baada ya ushindi wa Kikwete ndipo hasa tatizo la umoja ndani ya kundi kubwa la wanamtandao lilipojitokeza.

Katika kuhakikisha kila mwanamtandao anapata stahiki yake, Rostam akajikuta anatengeneza uadui na “vyombo” vya dola na viongozi wa chama, jambo lililochangia anguko lake la juzi.

Kosa la kwanza lilikuwa ni kusimamia Lowassa kupewa uwaziri mkuu. Baadaye “akamuumba” Samwel Sitta kwa kumpa nafasi ya spika – mtu ambaye alikuwa na matumaini makubwa ya kuwa waziri mkuu.

Katika kuhakikisha mpango wake wa kumweka Sitta katika kiti cha uspika unafanikiwa, Rostam aliwaomba wagombea wengine walioonekana wenye nguvu, akiwamo Philip Marmo kujitoa katika kinyang’anyiro hicho.

Inaaminika Rostam alifanya yote haya kwa baraka za Kikwete mwenyewe. Bali hapa ndiko ilikuwa tamati ya ndoa ya wanamtandao….

Mtandao uliobaki ukawa ule wa wote walioamini kuwa ni marafiki wa Kikwete, wakati ukweli ulikuwa Kikwete hakuwa tena na upande, bali aliunga mkono upande ulioonekana kushinda.

Kwa upande wa pili, ilianza kuonekana kuwa Kikwete amepoteza hamu na Rostam na ushawishi wake.

Ghafla Kikwete alimteua Pius Msekwa kuwa makamu mwenyekiti wa CCM, ilhali akijua Msekwa ni mhanga wa uspika uliochukuliwa na Sitta chini ya maelekezo thabiti ya Rostam.

Shughuli zote za kuendesha chama sasa zikawa chini ya Msekwa huku yeye akiwa nyuma akitazama minyukano yao.

Kama vile haitoshi, Kikwete akamteua George Mkuchika kuwa naibu katibu mkuu wa CCM, Tanzania Bara. Mkuchika alikuwa mhanga wa Rostam katika kinyang’anyiro cha nafasi ya katibu wa wabunge wa CCM.

Alipambana na Ali Ameir Mohammed. Ushindi wake huu haukuja hivihivi. Ilikuwa kama kumlipizia kisasi hasa baada ya Mkuchika, aliyekuwa rafiki wa Kikwete, kumgeuka wakati wa kampeni. Mkuchika alimuunga mkono Mwandosya.

Matokeo yake, Rostam akawa tayari amezungukwa na maadui wa kisiasa ndani ya chama, ndani ya bunge na ndani ya serikali.

Ripoti ya Bunge ya Richmond ilikuwa eneo mojawapo ambalo bunge chini ya Spika Sitta, CCM na serikali viliungana kuwashambulia Rostam na Lowassa, jambo lililobadili mwelekeo kutoka kilichoitwa na Kikwete, “ajali ya kisiasa” na kuwa tuhuma na hatimaye kuachia ngazi.

Bado wale viongozi waliokuwa wakituambia ubaya wake wamenyamaza kimya.

Ni wazi kabisa kumfanya Dk. Harisson Mwakyembe kuwa mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza sakata la Richmond hakukuwa kwa bahati mbaya.

Huyu alikuwa meneja wa kampeni wa Mkuchika katika kinyang’anyiro cha ukatibu wa wabunge wa CCM.

Matokeo ya uchaguzi uliopita ndiyo yaliyoleta taharuki ndani ya CCM, huku yakitafutwa majibu mepesi ya kufanya vibaya kwa chama hicho.

Mathalani hakuna aliyetayari kusema chama kiliwekwa pembeni katika uchaguzi mkuu uliopita na hata mwenyekiti wa kampeni, Kinana, alikuwa hajui kinachofanyika zaidi ya kuongea na vyombo vya habari.

Kazi zote za Umoja wa Wanawake (UWT) zilihamishwa kwenye chama zikakabidhiwa kwa mke wa rais, Mama Salma, huku zile za UV-CCM zikikabidiwa kwa watoto wa rais, Ridhiwani na Miraji Kikwete.

Kuna taarifa kuwa baadhi ya maeneo kama Iringa, msafara wa Ridhiwani ulikuwa na magari mengi zaidi kuliko aliyokuwa nayo mgombea mwenza, Dk. Mohammed Gharib Bilal.

Akiwa Iringa, Ridhiwani alivishwa uchifu, huku Dk. Bilal akiachwa bila kufanyiwa chochote, jambo lililosababisha chuki kwa wananchi, serikali na katika chama. Wenye chama walijitenga na shughuli za kampeni na kuiacha familia na marafiki zao.

Rostam hajajiuzulu kwa kuogopa matambo ya Nape Nnauye na wapambe wake. La hasha. Ni kwa kujua kwa dhati kuwa siyo kwamba Nape anawakilisha maazimio ya NEC, ukweli anawakilisha mawazo na maelekezo ya Kikwete.

Kwa kutambua hawezi kupambana na Kikwete anayepigana naye chini kwa chini, akaamua kufanya uamuzi wa busara wa kujiuzulu.

Rostam ameondoka. Lakini bado ana machungu na kinyongo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: