Huyu anaomba kazi ya kuua CHADEMA


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 24 November 2010

Printer-friendly version
Tafakuri

EMMANUEL Martine anachumbia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Anataka kimpe fedha ili akisaidie “kudhibiti vijana waliokinyima kura” katika uchaguzi uliopita.

Mradi wa kijana huyu anayejiita “mwanachama mwaminifu” wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), unalenga kuvamia vyuo vikuu nchini ambako anadai CHADEMA imejenga ngome.

Katika andishi lake alilolipa kichwa cha maneno “Waraka wa Siri,” anasema CHADEMA ina mkakati madhubuti kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015, hivyo anataka CCM imwezeshe kuudhibiti.

Anasema vijana wamekuwa mwiba mkali kwa chama na serikali, kwa sababu CHADEMA wamefanikiwa kupenyeza kile alichoita “sumu” vyuoni. Sasa anataka CCM imwezeshe aondoe sumu hiyo.

Andishi hilo la Martine linaonekana kuwa limewasilishwa kwa viongozi wa juu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), idara ya usalama wa taifa, makamu mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UV-CCM), Beno Malisa na mtoto wa rais, Ridhiwani Kikwete.

Martine anajitambulisha kuwa ni kiongozi wa jukwaa la vijana la taifa, mratibu wa shughuli za vijana wa CHADEMA, makamu mwenyekiti wa vyuo vikuu nchini na mwanzilishi wa alichoita “CHADEMA University Network” – mtandao wa CHADEMA Vyuo Vikuu.

Anasema serikali imekuwa ikikabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa vijana kutokana na Umoja wa Vijana (UV-CCM) kushindwa kufanya kazi zake.

“Umoja wa vijana wa CCM umeshindwa kutimiza wajibu wake,” anaeleza kwa nia ya kushawishi ufadhili.

Pamoja na kuomba ufadhili CCM, Martine analalamika kwamba baadhi ya vijana wa chama hicho “wameachwa solemba” pamoja na kujitolea kwa hali na mali katika kampeni za kumwingiza madarakani Rais Kikwete.

Anawataja baadhi ya wanafunzi walioachwa solemba kuwa ni pamoja na Mnanyi kutoka chuo kikuu cha Dodoma, Alex kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Luhajo kutoka Mbeya. Anawataja kwa jina mojamoja.

Aidha, Martine anamwagia sifa Kingunge Ngombale –Mwiru na makamu mwenyekiti wa chama hicho, Pius Msekwa kwa alichoita jitihada zao katika mkutano wa vijana uliofanyika kwenye ukumbi wa Ubungo Plaza, siku chache kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu.

Hata hivyo, mwandishi wa waraka analaumu chama kujisahau. Anajitapa kwamba ni yeye aliyesaliti wanafunzi wa vyuo vikuu nchini waliokuwa wanadai haki zao za msingi.

“Hapo ndipo tulipounda jukwaa la vijana ambalo leo hii limekuwa kama kinga na ngao ya CHADEMA kwa kuweka vijana wasiopungua 35 katika halmashauri na wabunge sita,” anaeleza Martine.

Anasema baada ya uchaguzi mwelekeo wa chama umekuwa mgumu; hakuna namna yoyote ya kukabiliana na hali hiyo wakati UV-CCM imejiweka kando.

Kuhusu mipango ya CHADEMA, Martine anasema chama hicho kimeunda kamati tatu ambazo zitafanya kazi ya kuhakikisha vijana wote walioingia vyuo vikuu nchini wanakuwa wafuasi wake.

Katika kampeni hiyo anataja wanachama na viongozi kadhaa wa chama hicho kuwa wanahusika katika utekelezaji wake.

Kwa mfano, katika mkoa wa Dar es Salaam anawataja mbunge wa viti maalum, Suzan Lyimo, mbunge wa Kawe, Halima Mdee, mbunge wa Ubungo, John Mnyika, Barton Gwakisa, Innocent Ngowi na Sauda Hemed.

Katika mkoa wa Dodoma anawataja Mtui, Mchange, Baraka, Hango mwenyekiti aliyemaliza muda wake (hataji majina ya pili), mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe na mbunge wa Singida Mashariki Tindu Lissu.

Mkoani Mwanza, Martine anawataja waliomo katika mpango wa kuingiza wanafunzi wa vyuo vikuu katika CHADEMA kuwa ni mbunge wa Nyamagana, Ezikea Wenje, Hawa Abdallah na Mussa Nyalagwinda.

Naye, mbunge wa viti maalum wa chama hicho, Lucy Owenya, Anderson Rwela anayemtaja kuwa ni katibu wa ushirika wa CHADEMA na mwanachama wa chama hicho aliyemtaja kwa jina moja la Kimemeta, ndio waliopangwa kufanya kazi mkoani Kilimanjaro.

Mkoani Mbeya, wanaotajwa ni mwenyekiti wa chama hicho, Shambwe Shitambala, mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi na mwenzake wa Mbozi Magharibi, David Silinde.

Anasema nyuma ya mipango hii ya kukuza uelewa wa jamii, kuna nguvu ya wafanyabiashara na baadhi ya wakuu wa shule.

Kwa mujibu wa mwandishi wa waraka, viongozi wa serikali za wanachuo wamepokea utaratibu wa CHADEMA kupitia Profesa Mwesiga Baregu na Dk. Kitila Mkumbo.

Bali MwanaHALISI lilipowasiliana na Profesa Baregu na Dk. Mkumbo, walikana madai hayo wakisema, “hayana ukweli na yametolewa na mtu mwenye njaa.”

“Namfahamu mwandishi wa waraka huo ambao nami nimeupata. Ni kijana mmoja ambaye hana kazi na ameandika hayo ili kuweza kujikimu kimaisha,” amesema Profesa Baregu.

Martine anaandika kuwa kwa sasa, hakuna vijana ambao tayari wameandaliwa kugombea nafasi za uongozi katika vyuo vikuu nchini.

Hata hivyo, mwandishi anasema, “ …jambo la kutia moyo wengine nimewaweka mimi madarakani kwa msaada wa Ridhiwani.”

Martine anasema utekelezaji wa anachoomba ni mgumu na wa “hatari.” Bali anatoa pongezi kwa baadhi ya viongozi wa UV-CCM akiwemo Ridhiwani, Aggrey Marealle na makamu mwenyekiti taifa, Beno Malissa kwa msaada wao kwake.

Wengine wanaomwagiwa sifa, ni Kingunge Ngombale–Mwiru anayesema amekuwa wa msaada mkubwa kwake hata kumfanya arudishe matumaini ya “…kumsaidia Rais Jakaya kikwete…”

Mwandishi anadai lengo lake la sasa ni kukisaidia chama chake ambamo amekulia.

Kuhusu mtandao wa shule, mwandishi huyo anadai kuwa CHADEMA kinatengeneza mtandao wa shule zote nchini. Hataji kazi ya mtandao anaodai kuwa CHADEMA wataunda.

Bali anasema, kazi hiyo itaanzia mkoa wa Kilimanjaro na kuenezwa katika mikoa ya Mwanza na Kagera.

Anatoa ushauri kwamba ni vema CCM kikawa makini kutokana na vijana hao kuwa ndio mtaji unaogeuka kuwa mwiba kwa CHADEMA katika siku zijazo.

“Kwa kuwa mpango wote tunao na kwa kuwa kila siku mipango ya chama huenda na utekelezaji, nawaombeni sana kuanza kufanya kazi katika vyuo vyote na shule ili kuwe na ripoti ya wapi tumetoka na wapi tunakwenda,” anaeleza.

“Shukurani za dhati ziende kwa makada wa Moshi na Hai waliojitahidi sana kutimiza wajibu wao, ila ugumu na makovu bado yako palepale,” anasema.

Martine anasema, “Sasa ni wakati wa kuamka…ni kama mfumo wa kijasusi…hii iwe wakati vyuo vinafunguliwa na katika mahafali. Nalazimika kufanya hivyo ili CHADEMA wasije nitoa roho.”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: