Iandaliwe kura ya maoni kuhusu Muungano kwanza


Nyaronyo Kicheere's picture

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 04 May 2011

Printer-friendly version

MWALIMU wangu wa sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) amekerwa na makala yangu ya wiki iliyopita iliyozungumzia muswada wenye magamba wa marekebisho ya katiba iliyochapishwa katika gazeti hili.

Muswada huo uliokataliwa bungeni na wadau wengine, sasa unatarajiwa kurejeshwa bungeni Juni mwaka huu baada ya kufanyiwa marekebisho yanayoelezwa kuwa yatakidhi haja ya kuunda tume ya kusimamia mchakato wa uandikaji wa katiba mpya nchini.

Hata hivyo, mwalimu wangu huyo ambaye ni profesa, hakutaka nitaje jina lake gazetini. Aliandika, “…Nyaronyo, nimesoma makala yako katika MwanaHALISI leo. Je, umesoma kwa makini clause 9 (fungu la tisa) ya muswada?

“Je, kweli inatoa makatazo hayo unayosema? Je, ni nani anayetajwa katika clause hiyo? Na je unaweza kuwa na makatazo (prohibition) bila kuweka kosa na adhabu?”

Nilimjibu kwamba mimi nilikerwa na matumizi ya maneno ‘inviolability’ na ‘sanctity’ ambayo kwangu yalimaanisha wanaoendesha mchakato wa marekebisho ya katiba wasihoji kuwepo au kutokuwepo mambo yaliyotajwa katika kifungu hicho cha 9

Naye alisema anakubaliana juu ya maana yake. Lakini akahoji, “Ni nani anatakiwa ayazingatie na wakati gani? Ni kwa sababu nakufahamu na sikosi kusoma makala nikiona jina lako.”

“Nimejiuliza tumekosea nini katika kufundisha statutory interpretation mpaka wanafunzi wetu wengi wawe na tafsiri hasi kwa clause ambayo mimi nikisoma sioni makatazo, bali misingi ya kuzingatiwa na tume. Je, hiyo misingi ndiyo basic structure doctrine ambayo imo katika hukumu ya Jaji Lugakingira ya Mtikila?”

“Samahani kwa kukuonea! Nikiri hoja zangu zaidi ni kwa wanasheria wengine! Nafuu sana wewe umesema mtu hazuiwi kuhoji tofauti na wengine waliosema wananchi wamefungwa midomo. Tume itakayoundwa nadhani inatakiwa iyazingatie hayo wakati wa kutoa mapendekezo katika clause 9(b).

“Tafsiri yangu, hayo yanatakiwa yaboreshwe lakini yasifutwe kabisa. Niulize tu kama idadi kubwa ya Watanzania watasema hawataki Muungano kabisa, je unadhani tume itaendelea na mchakato wa kutengeneza katiba mpya au utakuwa mwisho wa mchakato huu na sasa itabidi uanze mchakato wa kujadiliana mkataba wa kuvunja Muungano?

“Mataifa mawili mapya yatazaliwa na hayo sasa ndiyo yaanze upya kwa michakato ya katiba zao. Nitakutafuta tubadilishane mawazo! Mimi naona masuala mawili ndiyo yatakuwa magumu. Muungano na suala la mahakama ya kadhi.”

Nami nilimuuliza kuwa anadhani kutatokea nini iwapo wananchi wataukataa muungano? Alinijibu, “Katiba ya sasa itaendelea kwa sababu nchi ina katiba.”

Akatoa mfano wa Kenya, kwamba kura ya maoni ilipokataa katiba mpya mwaka 2005 ya zamani iliendelea.

Nimejifunza mengi kutokana na majibizano na mtaalamu huyu wa sheria wa Chuo Kikuu cha Dare s Salaam ambaye ninamheshimu sana.

Funzo mojawapo ni kwamba profesa huyu wa sheria ama alikuwapo muswada ukiandikwa au alishiriki kuandika muswada ule uliokataliwa.

Kama hakuwapo na wala hakushiriki, basi yeye ama alitoa ushauri juu ya namna ya kuandaa huo muswada au yeye ni miongoni mwa jopo la wataalamu lililotoa ushauri wa mambo gani yaingizwe kwenye muswada uliokataliwa.

Ukisoma vizuri maandishi yake inaelekea profesa huyu anakerwa na watu wanaopinga “muswada wake.” Kwake yeye muswada wa serikali ambao wananchi wanaupinga una mapendekezo mazuri ndiyo maana anasema mambo kwenye kifungu cha 9 (muungano, serikali ya mapinduzi, urais, bunge nk) yanastahili kuboreshwa na siyo kuondolewa.

Ndipo hapo nami najiuliza kwa nini yasiondolewe kama wananchi hawayataki? Kwa nini tume izingatie mambo hayo wakati wa kuandika rasimu ya katiba mpya badala ya kuzingatia yale ambayo wananchi wanayoyataka?

Kimsingi nakubaliana naye kwamba muungano utakuwa jambo gumu katika mchakato huu wa kuandika katiba mpya, lakini namshangaa kwa nini anasema mahakama ya kadhi nayo itakuwa jambo gumu kwenye mchakato huu? Je, ugumu unakujaje wakati kinachotakiwa ni makubaliano na maridhiano?

Ni muhimu kuwepo na namna ya kuwauliza wananchi kwa kila jambo linalobishaniwa. Kwa mfano, wananchi waulizwe na wawe huru kujibu kama wanataka mahakama ya kadhi au hapana. Kama wengi wakiitaka itakuwa hivyo, lakini wengi wakiikataa basi itabidi iachwe.

Nikiri kwamba mwalimu wangu alinishtua aliponihoji kitu gani kitatokea kama wananchi wengi wataukataa muungano. Hili ni jambo ambalo nilikuwa bado sijaweza kulitafakari sana na kwamba sasa nimepata shaka kubwa kama tutapata katiba mpya kabla ya uchaguzi ujao kama watu wengi wataukataa muungano.

Muungano ukikataliwa maana yake mchakato wa kuandika katiba mpya utasitishwa na hivyo uchaguzi wa 2015 utatukuta na katiba ya sasa yenye viraka vingi na ambayo inawapa wenye magamba ndani ya CCM mwanya wa kuiba kura kadiri ya uwezo wao!

Muungano ukikataliwa tutakuwa na misiba miwili. Msiba wa kwanza wa kupoteza Utanzania wetu na wa pili wa kulazimika kuendelea na katiba tusiyoitaka lakini itakayokuwapo kisheria hadi hapo itakapobadilishwa na wakazi wa taifa jipya la Tanganyika.

Kuukataa muungano ni sawa na kumsusia mlevi pombe.  Wote tunafahamu mlevi akisusiwa pombe huinywa yote tena kwa furaha. Hapa mlevi ni CCM ambaye akisusiwa muungano atafurahi sana maana atapata sababu ya kuahirisha kuandika katiba mpya.

Fikiria kikao chini ya mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete, Yusufu Makamba, Celina Kombani, mwanasheria mkuu wa serikali, Jaji Frederick Werema, Nnape Nnauye, Wilson Mukama, Stephen Wassira na wengineo halafu ikatolewa hoja ya katiba; haraka watasema, “…Wananchi hawataki muungano itabidi sasa tukae chini tufanye mchakato wa kugawana mali na madeni ya serikali ya Muungano.”

Miaka itapita wakizunguka huku na kule, wakiiba hiki na kile, wakihujumu mali hii na ile na kufanya ufisadi hapa na pale lakini katiba mpya bado!

Watasema kwa midomo mipana kuwa baada ya kugawana madeni na mali inayohamishika na isiyohamishika, tuangalie namna ya kuandika rasimu ya tume ya kuandika katiba mpya ya taifa jipya la Tanganyika.

Kuukataa muungano maana yake uchaguzi wa 2015 utaendeshwa na Tume ya Uchaguzi ya Jaji Lewis Makame inayoweka mbele maslahi ya CCM kabla ya kuangalia kama kuna wagombea wengine wanadai haki.

Tume ya uchaguzi ya Jaji Makame inayopata hesabu za kura kutoka Musoma, Kagera na Nanyumbu kabla ya kupata za Kariakoo na kuzijumlisha huku ikisaidiwa na intelijensia ya usalama wa taifa iwezayo kutabiri watakaofanya fujo kesho na majenerali wanaojua watakaopinga matokeo keshokutwa!

Ni vema kwanza kufanyike kura ya maoni kwanza ili wananchi waamue kama wanataka muungano au hatuutaki.

Kama wengi watataka kuendelea na muungano ndipo tuendelee na mchakato wa kuandika katiba mpya na kama wengi wataukataa basi kila taifa (Tanganyika na Zanzibar) lianze mapema mchakato wake wa kuandika katiba yake peke yake ili uchaguzi wa mwaka 2015 kila taifa liingie kwenye uchaguzi na katiba yake.

Mwandishi wa makala hii, Na Nyaronyo Kicheere ni mwanasheria, mwandishi wa habari na msomaji wa gazeti hili. Anapatikana kwa simu Na. 0785788727, imeil: kicheere@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: