Igunga kwafukuta


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 28 September 2011

Printer-friendly version
BAKWATA aibu tupu
Uchaguzi Jumapili hii
DC ageuka ‘bubu’
FATUMA  Kimario, Mkuu wa wilaya ya Igunga

FATUMA Kimario, mkuu wa wilaya (DC) wa Igunga, siyo muislam, MwanaHALISI limeelezwa.

“Kama ni muislam basi ni muislam kwa jina tu. Lakini anaishi na mkristo wa madhehebu ya kikatoliki na wamezaa pamoja watoto wanne,” ameeleza mtoa taarifa.

Kwa mfano, mtoto wao mmoja wa kike, Vivian Kimario anatarajiwa kufunga ndoa na mwanamme kutoka madhehebu ya kikristo, Oktoba mwaka huu.

Kimario na mke wake Fatuma wana makazi Mbezi Beach jijini Dar es Salaam. Familia yao ina watoto wawili wa kike na wawili wa kiume.

Bili ya maji ya shirika la Maji Safi na Majitaka la Dar es Salaam (DAWASCO) inaonyesha majina kamili ya mteja wao kuwa ni Fatuma Losingilo Kimario.

Wiki iliyopita ulizuka ubishi mkubwa mjini Igunga kwamba DC Fatuma ni muislam na kwamba “amevuliwa hijabu” kinyume cha maagizo na kanuni za dini yake.

Hilo lilitokea baada ya baadhi ya vijana waliodaiwa kuwa mashabiki wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kumfuma DC akifanya mkutano na viongozi wa mashina na kata ndani ya nyumba karibu na mkutano wa hadhara wa chama hicho.

Taarifa zimeeleza kuwa mkutano huo wa DC Fatuma ulilenga kukutana na viongozi wa vijiji. Kumbukumbu za mahudhurio zinaonyesha walioitwa walikuwa ni pamoja na madiwani wa CCM, mabalozi wa mashina, wazee maarufu na viongozi wa sungusungu.

Vijana hao wanadaiwa kumkamata Fatuma, kumweka chini ya ulinzi na kumkabidhi kwa polisi. Kawaida DC ndiye mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilayani.

Katika hali isiyotarajiwa, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na wanaojiita wanazuoni wa kiislamu nchini (HAY-AT), walijitokeza na kudai kuwa “muislam amedhalilishwa.”

Walidai kuwa mtandio aliokuwa ameweka kichwani lilikuwa vazi la “hijabu” na kwamba amevuliwa “vazi lake tukufu.”

Kauli hiyo ya BAKWATA Dar es Salaam, kupitia Sheikh Seleman Kilemile ilishika kasi na kufanya BAKWATA Igunga kuingilia kati na kusema mgombea wa CHADEMA asichaguliwe.

BAKWATA na wanazuoni wa kiislamu waliwapa viongozi wakuu wa CHADEMA siku tatu, kulaani kile walichokieleza kuwa kitendo cha wafuasi wao kumdhalilisha “muumini wa kiislamu.”

Sheikh Kilemile aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Jumanne iliyopita, “Shambulio lolote la hijabu ni dhidi ya Uislamu na waislamu kwa umoja wao, hawawezi kuvumilia.”

Mtoa taarifa amelieleza gazeti hili kuwa watoto wawili wa familia ya Kimario ambao ni wavulana “wanafuata madhehebu ya kiislamu” na wengine wawili ambao ni wasichana – Vivian akiwa wa mwisho – wanafuata madhehebu ya Kikristo.

Mwandishi alipotaka kupata maelezo ya DC Fatuma kuhusu taarifa hizi, kupitia simu ya mkononi Na. 0784855842, alijibiwa “Jamani, haya mambo mbona yanakwenda mbali? Mimi sijui kwanini yafike huko…haya mambo ni ya familia, familia yangu haijasema lolote…”

Alipokazaniwa, Fatuma alisema, “Naomba muiache serikali ifanyie kazi mambo haya jamani. Mimi sitaki kusema lolote. Naomba jambo hili lishughulikiwe na serikali. Nasema sina la kusema. Niacheni…” akazima simu.

Naye Kimario alipoitwa kupitia simu yake ya mkononi Na. 0784261114, alijibu: “Mimi si mhusika kwa sababu mimi si public figure (kiongozi au mtu mashuhuri)

“Yeye DC ndiye anayejua ndoa yetu ilivyo. Naomba nenda kwake. Halafu mimi sioni sababu ya mambo haya ya private (binafsi) kuanza kufuatiliwa na ninyi waandishi,” alieleza.

Kauli ya BAKWATA na wanazuoni imeibua majibu makali kutoka kwa CHADEMA. Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ambaye pia ni mwanasheria wa chama hicho, Profesa Abdalla Safari ametuhumu viongozi hao wa kidini kutumiwa na CCM kuchonganisha CHADEMA na waislamu.

Kufuatia kukamatwa kwa DC, polisi waliwakamata wabunge wawili wa CHADEMA, kuwaweka rumande mjini Tabora na kuwafungulia mashitaka mahakamani.

Wabunge hao ni mbunge wa Maswa Mashariki, Sylvester Kasulumbayi na mbunge Viti Maalum, Suzan Kiwanga. mwingine aliyefunguliwa mashitaka ni kaimu kamanda wa Baraza la Vijana la CHADEMA (Bavicha) Wilaya ya Igunga, Anwar Kashaga.

Mashitaka wanayokabiliwa nayo ni kumtukana CD kwa kumuita malaya, shambulio la kawaida, kumweka chini yaulinzi kinyume cha sheria na kumuibia simu yenye thamani ya Sh. 400,000.

MwanaHALISI lilitaka maoni ya viongozi wa madhehebu ya kiislam juu ya mazingira ya ndoa ya DC Fatuma.

Ustaadhi Amir Said Amir, mmoja wa wanazuoni waliosomea sheria za kiislamu nchini Libya amesema, “Tatizo watu wengi wanadhani uislamu ni jina. Uislamu ni imani na matendo mema.”

Amir amesema kila mtu anaweza kujiita muislamu, lakini kama hafuati misingi, hata kama amevaa hijabu, siyo muislam.

Sheria ya kiislamu inasema ndoa ya kiislamu itafungwa kwa kuzingatia muongozo wa kurani na maelekeo ya Mtume Muhammad (S.A.W).

Kwa mujibu wa maandiko matakatifu ya Kuraani (suratul Mumtahinah aya ya 10),  mwanamke wa kiislamu ambaye ameolewa na asiyekuwa muislamu, basi ametoka katika dini hiyo (murtaddah).

Naye mwanazuoni mashuhuri nchini, Sheikh Issa Ponda alipoulizwa kuhusu suala hili, alisema, “Kwanza, hakuna ndoa kati ya muislamu na asiyekuwa muislamu. Mtu akifanya hivyo atahesabika anafanya zinaa.”

Kuhusu mwanamke wa kiislamu au mwanamme kubadili dini, Sheik Ponda amesema, “Hilo ni kosa kubwa sana. Mtu wa aina hiyo, anakuwa ameleta mfano mbaya kwa uislamu. Anastahili kuadhibiwa kwa kupigwa mawe hadi kufa kutokana na kuritadi (kuondoka kwenye uislamu).”

Baadhi ya viongozi wa dini wamesema hatua ya viongozi wa BAKWATA na wanazuoni kukimbilia kulaani, imetokana na shinikizo la viongozi wa CCM.

0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: