Ije mamlaka ya kukomesha rushwa Zanzibar


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 18 July 2012

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

SIJUI kama viongozi wakuu wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wasaidizi wao wanajua kuwa rushwa imetapakaa ndani ya utumishi wa umma.

Wala sijui kama wanajua kuwa ukweli huo ndio hasa ulioisukuma serikali kutunga sheria ya kuanzisha mamlaka ya kupambana na rushwa.

Basi kama hawajui, huo ndio ukweli na ukweli mtupu – katika utumishi wa umma kuna rushwa na athari zake zinaonekana wazi.

Wananchi wanalalamika hawapati huduma hii na ile; wanalalamika kwamba wanakwamishwa na ofisa huyu na yule; wanalalamika kunyimwa haki zao mpaka watoe kitu kidogo (KK).

Wiki iliyopita, waziri anayehusika na utumishi wa umma na utawala bora, Haji Omar Kheri aliliambia baraza kwamba mipango inakamilishwa ya kuanzisha mamlaka ya kupambana na rushwa.

Malalamiko ya wananchi sasa yamekuwa yakibebwa kwa ukakamavu mkubwa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Wajumbe kila wanapoipata nafasi wakati wa mijadala barazani, wanalalamika kwa kueleza malalamiko ya wananchi. Wanataja na mifano ya malalamiko hayo; wanataja shida wanazopata wananchi katika kupata huduma.

Kuna malalamiko ya maofisa wakubwa, wa kati na wadogo, kujiingiza kwenye mienendo ya kufuja mali ya umma – fedha na vifaa.

Ufujaji unafanywa kwa njia mbalimbali.

Utakuta ofisa wa wizara au taasisi ya serikali anatajwa kwa kutumia vibaya gari ya serikali. Labda anaendesha gari aliyopewa kiofisi mpaka usiku, ambao si muda wa kazi, na hana kibali.

Au anatumia gari ya ofisi kwa kazi zake binafsi, tena pengine ni za shughuli za biashara. Yawezekana anafanya hivyo kwa kutumia mafuta yaliyonunuliwa kwa fedha za serikali.

Utasikia ofisa mwingine anatajwa kushiriki kupanga, kutekeleza na kunufaika na mpango wa kuuza gari ya serikali kinyume na taratibu.

Waweza kusikia ofisa ameidhinisha malipo ya gari ya Sh. 150 milioni lakini thamani halisi ya gari inayonunuliwa ni Sh. 100 milioni.

Wakati fulani ofisa mmoja katika Idara ya Uvuvi aliidhinisha malipo ya Sh. 47 milioni ya gari iliyotumika ambayo bei yake halisi ilikuwa ni Sh. 22 milioni.

Kwa ufupi, ofisa huyu alitumia fedha nyingi kununua gari kongwe, ununuzi usiotakiwa kisheria serikalini.

Utasikia jengo la serikali limekodishwa kwa mwekezaji au mtu binafsi tu pasina kufuatwa utaratibu wa manunuzi unaohitaji sheria ifuatwe na kila anayetaka aombe rasmi.

Katika siku za mwanzo mwanzo, Rais Dk. Ali Mohamed Shein alipokuwa akizuru mikoani kukagua shughuli za maendeleo, alikutana na malalamiko mengi ya migogoro ya ardhi.

Rais Dk. Shein akasikika akisema kuwa wale maofisa wa serikali waliosababisha migogoro hiyo, waishughulikie wao wenyewe mpaka imalizike.

Huko nyuma, kuliwahi kubainika kwamba maofisa wa idara ya ardhi na usajili, walijigawia viwanja vya kujenga nyumba viwili mpaka vitatu kila mmoja vilivyokusudiwa kugaiwa kwa wananchi wenye shida.

Zipo tuhuma kwamba ofisa mmoja ndani ya Idara ya Ujenzi na Utengenezaji Barabara (UUB) katika Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano, ameigeuza mitambo ya ujenzi mali ya serikali, kuwa ni mali yake na anakodisha kwa wajenzi (wakandarasi) wa barabara.

Bado wananchi hawajasahau namna mawaziri kadhaa wa serikali iliyopita na waliopo walivyohusika kukodisha majengo ya serikali kinyume na sheria.

Wapo maofisa wa serikali wanatuhumiwa kutumia madaraka yao vibaya. Pengine ni kwa kufukuza watumishi wenzao bila ya kuzingatia kanuni za utumishi, ikiwemo kumpa mtumishi mtuhumiwa nafasi ya kujitetea kabla ya kuadhibiwa.

Wapo viongozi serikalini ambao wamegawa zabuni kwa njia ya upendeleo baada ya kuwa wamepata malipo haramu kwa waliopewa zabuni husika.

Bali wapo watendaji waliotumika kuvuruga uchaguzi na hivyo kusababisha wagombea walioshindwa kutangazwa kuwa wameshinda.

Tena, katika mwenendo kama huo, matokeo ya uvurugaji huo yamesababisha fadhaa kubwa katika nchi ikiwemo machafuko na vifo vya raia waliokuwa wakipinga uvurugaji.

Kuna utamaduni unaokua Zanzibar wa viongozi wa serikali kudharau amri za mahakama na hivyo kusababisha wale waliopata manufaa kutokana na amri hizo kukosa haki zao.

Mfano mzuri wa uovu huu, ni uamuzi wa kesi ya uvamizi wa shamba la mzee Abdalla Shariff wa Shakani, Wilaya ya Magharibi, Unguja, ambaye pamoja na kushinda kesi mwaka 1993 utekelezaji wa hukumu haujafanyika.

Mara kadhaa polisi wametafuta visingizio vya kutotekeleza hukumu hiyo huku mazingira yakionesha wazi kuwa wamepata maelekezo ya wakubwa serikalini.

Hukumu ya kesi hiyo ya madai imewakumba viongozi mbalimbali waandamizi serikalini na wafanyabiashara wenye uswahiba na viongozi wakuu wa serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Imekuwa ni mtindo kwa miaka mingi sasa Zanzibar, maofisa wa serikali kuruhusu wafanyabiashara kuingiza nchini vyakula vibovu na kuuzwa.

Wakati fulani, mfanyabiashara mmoja anayeagiza mchele, sukari na unga wa ngano, alivunja kufuli za ghala ambamo mchele mbovu ulifungiwa na serikali na kufanikiwa kuutorosha nye ya kisiwa cha Unguja ambako uliuzwa.

Bila ya shaka yoyote, mfanyabiashara huyo alifanikiwa baada ya kuhonga maofisa wa ngazi ya juu wa serikali waliokuwa na dhamana.

Kwa upande mwingine, kuna mazingira ya rushwa na ufisadi kukuta mtumishi wa umma anamiliki mali za thamani kubwa isiyolingana na kipato chake. Huo ni ufisadi.

Sasa yote haya ni uthibitisho wa jinsi rushwa na ufisadi vilivyoenea katika sekta ya utumishi wa umma. Mdudu huyu amekuwa akiumiza sana haki za watu.

Haki zimekuwa hazipatikani na mara chache zinapopatikana, huwa ni baada ya wananchi kuhonga maofisa wa serikali.

Baadhi ya maofisa wa serikali huthubutu kuomba waziwazi rushwa na wengine huchelewesha kwa makusudi utaratibu wa kuhudumia mwananchi ili kuvutia kupewa KK.

Nayaeleza haya ili kuonyesha kuwa tuna tatizo kubwa hili na linahitaji kushughulikiwa kwa umakini mkubwa.

Kadhalika, nimelenga kusaidia wale watakaokabidhiwa jukumu la kuongoza mamlaka mpya ya kupambana na rushwa kuona ni kwa vipi wanakabiliwa na jukumu zito.

Ni jukumu zito kweli; lakini lazima litekelezwe.

0
No votes yet