Iko wapi AU?


editor's picture

Na editor - Imechapwa 24 February 2010

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

MATUKIO ya kishetani yanayoendelea nchi kadhaa za Afrika yanathibitisha jambo moja kubwa: Umoja wa Afrika (AU) haujamudu vema wajibu wake.

Kutoka Magharibi, Afrika ya Kati hadi Mashariki na Kusini mwa bara la Afrika, tunashuhudia mitafaruku mingi inayotokana na utawala mbaya.

Nchini Niger na Guinea hakuna utulivu, kwani wanajeshi ndio wanaoongoza serikali. Katiba zote zimesimamishwa na taasisi za serikali zimezuiwa kutumikia raia.

Jeshi limepindua serikali ya Rais Mamadou Tandja wa Niger kwa maelezo kwamba kiongozi huyo alitaka kung’ang’ania madarakani kwa kulitumia bunge baada ya muda wake wa kikatiba kumalizika Desemba mwaka jana.

Ivory Coast inakabiliwa na mvutano kati ya serikali na upinzani kufuatia hatua ya Rais Laurent Gbagbo kuvunja bunge baada ya kuchelewesha uchaguzi mkuu.

Hali ni ya mashaka eneo la Maziwa Makuu. Kuna taarifa kuwa kuna mbinu zinazotiwa nguvu na ukoloni mamboleo za kutaka kuigawa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ili kutengeneza “kijinchi” kingine kwa ubia kati ya Rwanda na Rais Joseph Kabila.

Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika nako hakuna utulivu mwanana. Zimbabwe haijakaa sawa; shauri ya mivutano katika serikali ya umoja.

Ni hali kama hiyo inaikumba Kenya. Utekelezaji wa mipango ya serikali ya pamoja umekuwa matatizoni.

Yaleyale yaliyotokea nchini Madagascar mwaka 2007, yamesababisha mtafaruku na hatimaye mapinduzi kutokana na watu kuchoka kuwaona viongozi wao wananenepa kwa ufisadi wa madaraka.

Pale viongozi halali wanapowageuka raia na kujifanyia mambo watakavyo, ikiwemo kuvunja misingi ya katiba, huu Umoja wa Afrika unakuwa wapi usikemee?

Inashangaza kusikia kila mwaka viongozi wa Afrika wanakutana Ethiopia, makao makuu ya umoja, au kwingineko na bado wanasiasa wakorofi wanaoendesha vibaya nchi zao wanaendekezwa na kulindwa.

Wakati mwingine inakera kubaini sehemu nyingine za dunia zinawahi kukemea uvunjaji katiba unaofanywa na viongozi wa Afrika, huku Umoja wa Afrika ukifuatia baadaye.

Ni kama vile umoja hauna wenyewe wakati sivyo ilivyo. Waafrika wanaopenda nchi zao wapo wengi na wanafuatilia kwa karibu uhuni wa watawala wao.

Wakazi wa Afrika wamechoka migogoro na wanataka umoja uonyeshe uzito wake. Uwe na mfumo utakaofuatilia na kuchukua hatua haraka pindi unapoona uongozi usio makini, badala ya kusubiri kuja kulaani mapinduzi ya kijeshi na nguvu ya umma.

0
No votes yet