Ikulu aibu tupu


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 23 November 2011

Printer-friendly version

VIGOGO kadhaa waandamizi serikalini na katika bunge wamenufaika na mamilioni ya shilingi yaliyokusanywa kinyume cha taratibu na David Jairo, katibu mkuu wizara ya nishati na madini, MwanaHALISI limeelezwa.

Ripoti ya Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma iliyokuwa ikimkabili Jairo, ndiyo iliyoanika kigogo mmoja baada ya mwingine, jinsi walivyonufaika na fedha hizo.

Miongoni mwa vigogo walionufaika na fedha zilizochangishwa na Jairo kinyume cha maelekezo ya serikali na kupanga matumizi yake bila kibali cha Hazina, ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Spika wa Bunge la Jamhuri, Anne Makinda.

Kupitia taasisi zilizoko chini ya wizara yake, Jairo alikusanya zaidi ya Sh. 140 milioni kwa kile alichoita kufanikisha bajeti.

Nyaraka zinaonyesha Pinda na Makinda wamelipwa kutoka kwenye fedha hizo posho ya kujikimu ya Sh. 280,000 (laki mbili na elfu thamanini), kila mmoja baada ya kuhudhuria semina ya wabunge kuhusu umeme.

Viongozi hao wawili wa ngazi ya juu katika mihimili miwili ya dola – Bunge na Serikali – walilipwa fedha hizo, tarehe 26 Juni 2011.

Wakati Pinda na Makinda wakilipwa kiasi hicho cha fedha, wabunge wengine waliohudhuria semina hiyo walilipwa Sh. 110,000 (laki moja na elfu kumi tu) kila mmoja.

Mbali na Pinda na Makinda, wengine waliolipwa kiasi hicho cha fedha, ni Diana Chilolo, Makamu mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na John Joel, ambaye ni ofisa katika ofisi ya Bunge.

Kiongozi mmoja mwandamizi ndani ya serikali aliyezungumza na MwanaHALISI kwa sharti la kutotajwa gazetini amesema, “Sakata la Jairo, ni aibu kwa serikali mzima.”

Amesema, “Kwa nafasi yake ya uwaziri mkuu, Pinda analipiwa kila kitu na serikali, ikiwamo nyumba, chakula, mavazi na usafiri. Ni jambo la kusikitisha, kwamba waziri mkuu anakubali kupokea Sh. 280,000 kwa kitu kisichozidi dakika 40 na ambacho ni sehemu ya kazi zake. Labda ningemuelewa kama angelipwa sawa na wabunge wengine.”

Amesema, “Hata Makinda, hakustahili kulipwa fedha zote hizo. Huyu mama kwa nafasi yake ya spika wa bunge, analipiwa na serikali malazi, chakula, usafiri, mavazi, posho ya kujikimu, pamoja na posho ya kuhudhuria vikao vya bunge.”

Amesema, “Makinda analipwa pia posho ya kuendesha mikutano ya bunge. Haiingii akilini, taifa masikini kama hili, viongozi wake wanakubali kulipwa fedha zote hizo katika mazingira ambayo hayako wazi na yaliyojaa utata.”

Aidha, ripoti ya Bunge imeonyesha jinsi Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, naibu waziri, Adam Malima, katibu mkuu Jairo, pamoja na maofisa wengine wa ngazi ya juu kwenye wizara ya nishati na madini, jinsi walivyolipwa kiasi kikubwa cha fedha katika mazingira yenye mashaka.

Kwa mfano, Ngeleja na Malima, nyaraka zinaonyesha wamelipwa Sh. 4 milioni kila mmoja kutoka sehemu ya fedha ambazo Jairo alikusanya kama “entertainment allowance” (posho ya kufarijisha) “ili kuwawezesha kubadilishana mawazo/ kushauriana na wadau muhimu na wananchi wa majimbo yao, wanaofika Dodoma kuwaona kwa masuala mbalimbali ya maendeleo ya majimbo yao, katika kipindi cha bunge la bajeti.”

Kwa mujibu wa dokezo la tarehe 16 Julai 2011 lililotoka kwa I.H. Swai, mkurugenzi wa uendeshaji (DP), malipo hayo ya Sh. 4,000,000 yamelipwa 18 Julai 2011.

Kama hiyo haitoshi, 25 Juni 2011, Ngeleja amelipwa kiasi cha Sh. 400,000 kama posho ya kikao kwenye semina ya wabunge; tarehe 26 Juni 2011, amelipwa Sh. 800,000 kama “malipo maalum kwa viongozi” na amelipwa kiasi kingine cha Sh. 800,000 kama “posho ya kujikimu.”

Naye Jairo, kwa siku moja ya 25 Juni 2011, amelipwa kiasi cha Sh. 800,000 kama “posho maalum ya viongozi,” Sh. 3 milioni kama posho “maalum ya semina,” Sh. 400,000 kama posho ya kujikimu kwa maofisa wa wizara waliopo Dodoma, Sh. 80,000 kama posho ya njiani na Sh. 3.2 milioni kama posho ya safari.

Kwa siku moja, Jairo peke yake alikusanya jumla ya Sh. 7.4 milioni.

Viongozi wengine wa wizara hiyo, akiwamo Teresia Mghanga, Theophilllo Bwakea, Laula Kessy, Prosper Victus, Aloyce Tesha, Hawa Ramadhani, Haika Minja na Edward Ishengoma, nao walilipwa kama ambavyo Jairo amelipwa, igawa walitofautiana viwango.

Naye aliyekuwa kamishina wa madini, wizarani hapo, Dk. Peter Kafumu amelipwa kiasi cha Sh. 300,000 kwa ajili ya maandalizi ya bajeti.

Wakati wafanyakazi hawa wakijilipa fedha hizo kama posho ya kazi waliyokuwa wakiitekeleza Dodoma, wizara hiyohiyo ilikuwa imelipa wafanyakazi wote akiwamo Jairo stahiki zao kwa ajili ya kazi hiyo.

Kamati Teule ya Bunge iliundwa na Spika Makinda kuchunguza sakata la malipo ya mamilioni hayo ya shilingi kwa watendaji wa wizara ya nishati na madini.

Pamoja na mambo mengine, kamati ilichunguza “utaratibu wa uchangishaji wa fedha uliofanywa na wizara hiyo na kugundua kuwa haukuwa na uhalali wowote kwa mujibu wa katiba, sheria na kanuni za fedha za umma.”

Ripoti ya Bunge, mbali na kumueleza Jairo kuwa alivuka mipaka ya kazi zake, imemtuhumu Philemon Luhanjo, katibu mkuu kiongozi kwa kutosema ukweli kuhusu utaratibu huo.

Kamati Teule imesema fedha zilizotumika kutekeleza agizo la Jairo hazikutoka kwenye bajeti yoyote iliyowekwa kwa ajili hiyo.

Imesema, “Nyaraka halisi zinaonyesha fedha zilizokusanywa zimetumika kwa ajili ya malipo ya posho ya kujikimu kwa watumishi 69 wa wizara, posho ya vikao kwa watumishi 243 waliokuwa Dodoma, manunuzi ya chakula na manunuzi ya vifaa vya kuandikia.”

Malipo mengine ni “takrima kwa waziri na naibu waziri na manunuzi ya mafuta kwa ajili ya magari, matumizi ambayo yangeweza kugharimiwa na kasma husika za wizara bila kuhitaji kuchangisha.”

Mashirika ambayo yalimimina fedha kwa Jairo, ni Shirika la Umeme la Taifa (TANESCO) lililotoa Sh. 40 milioni, Shirika la Maendeleo Vijijini (REA) Sh. 50 milioni na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) lililotoa Sh. 50 milioni.

Mbali na fedha hizo, dokezo sabini lililoandaliwa na mhasibu wa wizara hiyo, Hawa Ramadhani, tarehe 30 Juni 2011, linaonyesha mashirika ya umma kama vile, REA, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), TANESCO na TPDC, kila moja lilitoa Sh. 22 milioni kufanikisha bajeti.

Hata hivyo, wakati taasisi zilizochini ya wizara hiyo zikitobolewa mifuko kwa kulazimishwa kutoa kiasi hicho cha fedha za kusaidia ufanikishaji wa bajeti, wizara ya nishati na madini imekusanya na kutumia kiasi cha Sh. 207 milioni kwa ajili ya mradi wa kufanikisha bajeti.

Kwa mujibu wa dokezo Na. 14 la Juni 2011, lililoandaliwa na A.K.F Murusuri, mchumi mkuu wa wizara, kwenda kwa mkurugenzi mwendeshaji, lenye Kumb. Na. EB 88/612/01/13, kiasi hicho cha fedha, ni maalum kwa ajili ya “kufanikisha uwasilishaji wa hotuba ya bajeti.

Dokezo linataja shughuli nyingine kuwa ni kugharamia vikao vya Kamati ya Menejementi na Maendeleo ya Kisekta (SDC) kujadili rasimu ya hotuba, kuchapisha vitabu vya hotuba, gharama za usafiri kwa watalaamu wa wizara watakaoshiriki uwasilishwaji wa hotuba hiyo na masuala mengine yanayohusiana kadri yatakavyojitokeza.”

Katika fedha hizo, waziri Ngeleja na Malima wamelipwa Sh. 2 milioni kila mmoja kama posho ya kujikimu kwa siku saba za bajeti. Kiasi hicho cha fedha, ni nje ya Sh. 4 milioni walizolipwa awali.

Waraka wa serikali Na. 3 wa mwaka 2011 uliotoka kwa Katibu Mkuu Hazina kwenda kwa makatibu wakuu, watendaji wakuu wa serikali na mashirika na taasisi za umma, Tanzania Bara, tarehe 7 Machi 2011, pamoja na mambo mengine, uliagiza kusitishwa mara moja utaratibu wa mashirika ya serikali kutoa fedha kwa wizara kwa kisingizio cha kusaidia bajeti.

Waraka huo uliosainiwa na Ramadhani Khijjah ulisema,“…Wizara haipaswi kupewa fedha za ziada kupitia mashirika na taasisi zilizochini yake.”

Waraka unasema, “Endapo kutatokea mahitaji yatakayolazimu kutumia fedha kutoka kwa mashirika au taasisi za umma chini ya wizara, ni lazima kupata kibali cha waziri wa fedha baada ya kushauriwa na mlipaji mkuu wa serikali (PMG) na msajili wa hazina kwa mujibu wa sheria ya fedha ya mwaka 2008.”

Mbali na utata wa malipo hayo, Kamati Teule imegundua gari moja la serikali lililipiwa lita  3,000 za mafuta, wakati gari hilo halikuwahi kufanya safari yoyote katika kipindi hicho.

Kwa hatua hii, wachambuzi wa kisiasa wanasema, ikulu ya Rais Kikwete imepata fedheha kwa kuwa ni Katibu Mkuu wake, Philemon Luhanjo aliyekuwa amemkingia kifua Jairo.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: