Ikulu ibaki ofisi takatifu


editor's picture

Na editor - Imechapwa 19 August 2008

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

IKULU ni ofisi yenye hadhi kubwa. Hadhi yake inatokana na kuwa ndio mahali pa kuthibitisha taswira nzima ya nchi na watu wake. Ikulu ndio makao makuu ya rais na chimbuko la maamuzi mazito ya kitaifa na kimataifa.

Inapotokea ofisa, karani au hata tarishi wa ofisi hii ametenda kinyume cha matakwa ya umma, haraka itabainika kwamba ikulu imeingiliwa.

Ni matarajio ya kila mtu kuona ofisi hii, kwa maana ya watumishi wake, wanatenda kwa nidhamu ya hali ya juu na kwa umakini.

Mwaka 1995 Mwalimu Julius Nyerere aliasa kwamba ikulu hakuwezi kukaliwa na watu wachafu. Wakati ule alishangaa kuona wanachama wa CCM wameonyesha uchu wa kutaka kuingia ikulu.

Aliwakemea na kulazimika kutumia nguvu kubwa kuwazuia wote alioamini watachafua mahali patakatifu. Alifanikiwa, ingawa yule aliyemuamini alikuja kubadilika baadaye.

Tunasikitika kwa yanayotokea sasa katika ikulu yetu na hasa yale yanayotendwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano, Salva Rweyemamu.

Ikulu inageuzwa ofisi ya kuonyesha umahiri katika “vituko.” Tusemeje zaidi ya hivyo wakati kila kukicha tunashuhudia vituko? Kitendo cha kuhangaisha waandishi kama vile hawana kazi nyingine zaidi ya kusubiri habari za Ikulu, utakiitaje kama si kituko?

Juzi Jumatatu, waandishi wa habari waliitwa haraka kushuhudia Timu ya Rais ikikabidhi ripoti ya uchunguzi kuhusu ufisadi uliogunduliwa katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA). Na kwa sababu anazozijua hakulipa taarifa gazeti hili, MwanaHALISI.

Baada ya muda mfupi, waandishi waliambiwa tukio hilo limeahirishwa. Hawakueleza sababu.

Haukupita muda, Salva akapiga simu kwa wahariri mbalimbali akijulisha kwamba rais amepokea ripoti. Kama ilivyokuwa awali, MwanaHALISI hatukufahamishwa lakini tulipata taarifa mapema kupitia vyanzo vyetu makini.

Hatujachukia chochote kwa kutoarifiwa maana yanapita mengi tunawekwa kando. Kikubwa tunachoshukuru ni kuona Mwenyezi Mungu aliyeumba mbingu na ardhi na vyote viliomo ndani, anatuwezesha watendaji wa Hali Halisi Publishers (HHP) kufanya kazi kama tunavyopanga.

Tukio hilo linaonyesha ndani ya ikulu kuna udhaifu mkubwa wa mawasiliano kati ya rais na watendaji wake. Tusemeje maana haiwezekani Ikulu ikafanya mambo kwa kubahatisha.

Tunasikitika. Tunataka ikulu ibaki ofisi ya umma, si kwa maslahi ya kundi fulani. Kama wapeleka ujumbe kwa umma, hatutarajii kupokea habari zilizokwishaandikwa na ikulu kwa tukio lililotokea Magogoni. Na kwa jambo la ghafla tunaweza kuvumilia na kuelewa, lakini si hili la rais kukabidhiwa ripoti.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: