Ikulu imeshindwa, korti imeweza


Paschally Mayega's picture

Na Paschally Mayega - Imechapwa 15 September 2010

Printer-friendly version

HISTORIA imeandikwa. Mwana mwema, Anney Anney, yule mlemavu kutoka Arusha ameachiwa huru na mahakama ya Hakima Mkazi Kisutu.

Ni baada ya kuishi gerezani kwa zaidi ya miezi sita kabla ya kupata dhamana. Alikuwa anakabiliwa na kile polisi walichoita, “tuhuma za uchochezi.” Nilikuwapo mahakamani siku Anney alipokuwa anasomewa hukumu yake.

Kwanza, nikiri kwamba ilikuwa kazi ngumu mimi kutinga mahakamani. Je, ilikuwaje? Nikiwa nimejipumzisha chini ya mwembe wangu, tarehe 6 Septemba 2010, nilipokea simu kutoka kwa Anney.

Alisema, “Mwalimu kesho tarehe 7 ndiyo siku ya kusulubiwa. Naomba uje, uwepo wako walau kunifariji.”

Mungu wangu! Nilimwambia sawa bila kujua kama nimemkubalia. Nilijawa na wasiwasi mwingi katika kifua changu. Fikra zikawa za kukinzana kichwani mwangu. Nikafadhaika sana.

Unajua, katika hali kama hii mwanadamu, bila kudhamiria hujikuta amesahau kuwa Mungu ndiye muweza. Huelekeza matumaini yake kwa wanadamu anaowaona.

Mahakimu wetu ndiyo hawa. Baadhi yao hatujui ni wa dini gani ingawa tunakuwa nao katika nyumba zetu za ibada. Nikaikumbuka hukumu ya mahakama ya rufaa juu ya mgombea binafsi, mwili wote ukafa ganzi.

Nikaikumbuka hata hukumu iliyodhalilisha mahakama, “iliyotolewa usiku wa manane” ambayo ililenga kuzuia walimu wasigome. Nikachoka!

Nikakumbuka “hukumu ya John Tendwa” yule msajili wa vyama vya siasa katika shauri la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) dhidi ya mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete. Nikapatwa na msiba mwingine.

Hakimu anafikishwa mahali mpaka anaona aibu kuisoma hadharani hukumu aliyoiandika mwenyewe. Angalau yeye alionyesha kuona aibu. Wale wengine waliisoma hukumu yao kama mtoto anayesoma kitabu cha hadithi asiyoielewa.

Kesi hizi zilikuwa zinaigusa ikulu. Hii ya huyu mlemavu, nayo inaigusa ikulu. Atatoka wapi hakimu mwema kati ya hawa waliokwisha kututumbukia nyongo?

Nilipoziunganisha kumbukumbu za hukumu hizi nikajua mlemavu wetu atachukua miaka bila kuwa na kosa lolote!

Niliwaza atakapopatikana na hatia na kuhukumiwa adhabu kwa mashtaka ambayo hayana ukweli nitapata wapi nguvu za kurudi nilikotoka?

Je, iwapo hakimu atasema, “sioni kosa juu ya mtu huyu,” hivyo akaamua kumwachia huru, akili yangu itakubali kile ambacho masikio yangu yataiambia kuwa ndicho ilichosikia?

Nikasema: Liwalo na liwe. Nikaenda mahakamani. Nikapata nilichotaka. Kumbe mahakimu wema, ambao wanamtanguliza Mwenyezi Mungu katika hukumu zao bado wapo katika nchi hii.

Wachache tena wenye nyadhifa kubwa wameitia najisi taaluma yao, jambo ambalo limesababisha watu wengi kupoteza imani na chombo hiki. Wengi wanaona kuwa bila hela haki haitendeki.

Lakini nani anayesababisha matatizo haya? Jibu liko wazi: Ni vichwa ngumu. Wale ambao wanapata madaraka bila kutegemea.

Hawa wanapotenda, hutenda bila kufikiri, wakidhani wanawalinda mabwana zao kumbe wanaipeleka nchi katika machafuko na umwagaji wa damu.

Nilifika mahakamani siku iliyofuta. Nikashuhudia Hakimu A. Kibona akisema katika hukumu yake ya kihistoria, kwamba haoni kosa lolote juu ya mlemavu yule hivyo akaamuru kumwachia huru.

Hukumu ya hakimu mwema ikatofautiana na zilizotangulia ambazo watu makini walizisoma kabla mahakimu wenyewe hawajaziandika.

Nakala ya hukumu hiyo yenye kurasa 16 nimeisoma yote. Inasema, “Askari aliyemkamata alikiri kumkuta ikulu akiwa amekaa tuli katika kiti chake cha ulemavu huku akiwa hafanyi kitu chochote ambacho kingeashiria uvunjifu wa amani.

“Alipewa maji na kahawa akanywa. Alipoambiwa akaache ujumbe wa maandishi kwa rais ndipo alipokamatwa na kupelekwa ‘lockup’ ambako aliwekwa ndani toka Alhamisi mpaka Jumatatu. Siku nne mfululizo bila kupatiwa chakula chochote!” Unyama gani huu jamani!

Aliniambia walipojua kuwa amedhoofika kiasi cha kukubali chochote wakampa ofa ya kurudishwa nyumbani kwao Arusha kwa ndege na kurudishiwa fedha zake alizotumia kwa nauli ya kuja Dar es Salaam na malazi, akakataa.

Walipoona yuko radhi kufa kuliko kuisaliti nchi yake ndipo watesi wake katiri, walipomfungulia mashtaka ya uchochezi. Wakambambikia kesi ya kuhatarisha amani ya nchi.

Na alipokuwa gerezani alitengwa na wengine kwa madai kwamba ni mtu hatari sana kwa sababu alitaka kuipindua serikali. Siyo shetani peke yake anayeweza kuutenda uovu huu!

Mwenyewe anasema alikuwa akiwasihi polisi kila mara wasimuue kama walivyowaua wale wafanya biashara wa madini wa Mahenge. Kovu la serikali lisilopona! Wananchi watasemaje kwa hili?

Akaongeza, “Kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani na waliomkamata mtuhumiwa, nimeridhika bila kuwa na shaka yoyote kuwa mtuhumiwa alienda ikulu kumwona rais na si vinginevyo.”

Mwenyezi Mungu akubariki sana hakimu mwema. Yeyote aliyehusika katika unyama huu, hata kama anatembea na kuishi kati yetu ajue kuwa yeye ni sawa na mnyama. Kuvaa nguo si hoja!

Tunapowapima wagombea saba wa urais, lazima tuwapime kwa uwezo wao wa kuzuia na kuwakabili wanaotenda unyama wa aina hii.

Anayeshindwa kuulaani unyama huu na kuwanyamazia wanaotenda, tumkatae, tusimchague, hatufai hata kidogo, hata kama atatuahidi mbingu.

CHADEMA walipoibua hoja ya ufisadi katika nchi Samweli Sitta, yule Spika wa Bunge la Jamhuri alizuia hoja na kulazimisha wabunge wake kwenda mahakama ya wananchi.

Leo Sitta na walewale aliotuambia kuwa ni mafisadi wako pete na kidole. Kwa pamoja wanakula na kunywa nguvu ya wavuja jasho wa nchi.

Mwamuziki Lwambo Lwanzo Makiadi (Franco) wa Zaire (sasa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo) akishirikiana na Sam Mangwana waliimba, “Mwongo na Mulozi ni watu wa kuchoma.”

Hakimu amepima na kuchambua. Ameona na kujiridhisha kuwa yule kijana alionewa na wenye dola. Akakataa kupata dhambi ya milele ya kumtia hatiani asiye na kosa.

Jamani, mahakimu wakubwa! Yawapasa muelewe kuwa japo wananchi wengi hawajazamia katika sheria lakini uwezo wao wa kufikiri sawa sawa ni mkubwa. Mkiwafanya mafala watawadharau.

Mwandishi wa makala hii, Paschally Mayega amejitambulisha kuwa msomaji wa MwanaHALISI. Anapatikana kwa simu: + 255 713 334 239.
0
No votes yet