Ikulu inapotumika kumfurahisha Rais


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 22 December 2010

Printer-friendly version

MUSSA Lunyeka Dotto, amesafiri kwa kutumia baiskeli kutoka Chabulongo, wilayani Geita, mkoani Mwanza hadi ikulu jijini Dar es Salaam kumpongeza rais Jakaya Kikwete kwa kutangazwa kuwa mshindi wa kiti cha urais kwa mara ya pili.

Ndivyo picha za kituo cha telelevisheni cha taifa (TBC1) kilivyoripoti wiki mbili zilizopita.

Akiwa ikulu, Mussa alipokelewa na wasaidizi wa rais na baadaye alibahatika kukutana na kufanya mazungumzo na rais mwenyewe.

Hata hivyo, haikuelezwa Mussa alitumia siku ngapi kufika ikulu; alipumzika wapi; nani aligharamia safari yake; amelipwa kiasi gani na yupi aliyemhakikishia kuwa akifika tu, atakutana na rais?

Lakini kwa namna alivyofanikiwa kukutana na kiongozi wa nchi, wengi imewashangaza. Ukiangalia kwa makini, haraka utabaini kuwa kijana huyo aliandaliwa kufanikisha mpango maalum wa watu wanaotaka kumjengea taswira rais kuwa anapendwa.

Hata hatua yake ya kukutana na rais inathibitisha madai hayo. Ni kwa sababu, kwa miaka mingi sasa, kumekuwa na malalamiko kutoka kwa watu mbalimbali, wakilalamikia urasimu mkubwa wa kumuona rais.

Kumbe ukitaka kupiga soga na rais, wafuate wapambe wake na waeleze unataka kumpongeza, haraka utapata miadi ya kukutana na mkuu wa nchi.

Kingine ninachokiona ni ukweli kuwa rais wetu anapenda fakhari na televisheni inamsaidia kufanikiwa.

Akipiga suti yake aliyoichanganya na tai, huku akichati na mgeni yeyote hata kama hakuna cha maana wanachokizungumza, inavutia.

Angekuwa mtu mwingine ningesema anasumbuliwa na ushamba. Ananatia raha. Naogopa kusema rais wetu ni mshamba, lakini si kosa na simvunjii heshima kurudia kusema anapenda kuonekanaonekana.

Nilipoona picha hiyo, nilirudisha kumbukumbu zangu kwa Bibi Johari Salum Msuya, mkazi wa Kinondoni asiye na makazi ya kudumu baada ya wajanja kumpora nyumba aliyokuwa amepewa na serikali.

Mwaka 1993, Bibi Johari alipewa nyumba Na. 3, Block 31A, mtaa wa Karafuu, Kinondoni baada ya mmiliki wake kikongwe wa Uganda, Juma Tasibihi, kufariki dunia bila ya kuwa na mrithi.

Bibi Johari aliomba nyumba hiyo na baada ya kuthibitishwa na serikalia kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, alikabidhiwa. Ilikuwa chini ya Kabidhi Wasii Mkuu wa Serikali, anayetunza mali zote zisizokuwa na mrithi.

Miaka minne baadaye, alitolewa mkuku na wajanja waliolaghai mahakama kwa watumishi wake kusaidia kesi ya mirathi iliyobuniwa na hatimaye akajitokeza eti alinunua nyumba hiyo kwa warithi wake.

Hadi sasa Mahakama ya Kinondoni inakana kuwahi kusikiliza na kuamua kesi ya mirathi kuihusu nyumba hiyo. Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo alisaini barua Kumb. Na. PCK/KMD/CR/5 ya 19 Februari 2003 kuijulisha rasmi serikali kwamba “Mahakama hii haijapata kusikiliza kesi ya mirathi inayofunguliwa na mlalamikaji aitwaye Kissumo. Suala hili linahitaji kufanyiwa utafiti wa kina.”

Bado nyumba hiyo haijarudishwa kwa Bibi Johari. Haijarudishwa licha ya Mahakama Kuu kuthibitisha uhalali wa nyumba hiyo kupitia kesi Na. 418 ya mwaka 1999 iliyofunguliwa na Kabidhi Wasii Mkuu wa Serikali.

Gazeti hili, likitumia vielelezo mbalimbali vya kiserikali limechapisha makala mbili kufichua uhalifu uliofanywa kwa msaada wa ofisi ya Kabidhi Wasii Mkuu lakini bado hakusaidia kuwazindua wasaidizi wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, wizara inayohusika na utawala bora, wala Ikulu.

Maisha ya Bibi Johari yameendelea kuwa ya kubahatisha akitegemea huruma za wasamaria wanaomsaidia makazi pamoja na mwanawe Mohamed Dudu, mwenye ulemavu wa viungo.

Historia ya Bibi Johari inaanzia mbali. Alianza kusaidiwa kama mama fukara aliyepata mtoto mlemavu akiwa wilayani Monduli na kundi la watu mashuhuri likiongozwa na Edward Moringe Sokoine, aliyekuwa waziri mkuu.

Alilazimika kuhamia Dar es Salaam ambako Mohamed alipangiwa kuwa karibu na madaktari ili kusaidiwa baada ya kutomudu kuendesha baiskeli ya walemavu. Aliandaliwa uangalizi maalum kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili chini ya Dk. Profesa Philemon Sarungi.

Ofisini kwetu MwanaHALISI, tunapokea Watanzania, vijana na wakubwa, waliodhulumiwa na kuathirika kimwili na kiakili na hawakusaidiwa walipolalamika ofisi za wilaya, mikoa na wizara.

Walibeba mizigo ya nyaraka hadi Dar lakini wakashindwa kukutana na viongozi wakuu kama Waziri Mkuu, sembuse rais wa nchi.

Baadhi yao wamelia mbele ya wafanyakazi wa MwanaHALISI wakihoji inakuaje Ikulu ishindwe hata kujibu kupokea malalamiko ya mwananchi na labda inayafanyia kazi.

Lawama kama hizo zimeifika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRGG) na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP).

Kwa mfano, IGP amekalia malalamiko ya familia ya kina Selelii wa Shinyanga ambao ndugu yao aliuawa siku moja tangu kukamatwa na polisi wa kituo cha mkoa akiwa nje ya kwao.

Kuna ushahidi usio shaka alikamatwa pamoja na muuza duka jirani yake ambaye aliachiliwa jioni yake. Yeye hajarudi kwao hadi sasa.

Selelii hakufikishwa mahakamani wala gerezani ambako ndugu zake walifika kumtafuta. Asubuhi yake, Polisi walikataa kupokea chai aliyopelekewa kituoni na ndugu zake.

Si mkuu wa kituo, Kamanda wa Wilaya, Mkoa na Ofisa Usalama wa Wilaya aliyesaidia familia hiyo ingawa walipokea malalamiko. IGP aliandikiwa rasmi suala hilo mwaka jana lakini hakuna hatua ya msaada iliyofuata.

Familia ya kina Mgeleka wa Ibiri wilayani Uyui, mkoani Tabora ilimpoteza mzee wao, Mgeleka Yussuf, aliyeuawa kwa kupigwa risasi na kijana aliyepakiwa kwenye pikipiki.

Mauaji yalifanywa karibu na nyumbani kwake na vijana waliofahamika lakini kwa kuwa zilikuwepo njama zilizoandaliwa vizuri na wapinzani wake wa kisiasa na katika chama cha ushirika, vijana hao hawakushitakiwa.

Familia imetishwa kila aina. Ikatakiwa kuacha kufuatilia mauaji hayo ya Desemba 2008. Gazeti hili lilichapisha malalamiko yao lakini haijawa kitu hata walipomfuata IGP na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Matukio hayo machache yanaonyesha namna gani raia wanavyokutwa na shida kubwa lakini wakakosa msaada wa viongozi wakuu wa serikali.

Wahusika wa matukio hayo, wangependa kukutana na IGP, Waziri Mkuu au Rais, lakini wapi? Yao ni matatizo yanayohitaji ufumbuzi, siyo kutaka kupiga soga na rais.

Watanzania wengi wana matatizo yanayowaumiza lakini kwasababu wakimfikia rais yatamchefua, wanafungiwa mageti.

Ni upuuzi Ikulu kutumika kumfurahisha kiongozi wakati kuna wananchi wanaoumia na hawajasaidiwa na mfumo wa serikali.

Nilidhani rais ni taasisi muhimu kwa wenye shida au wanaolenga kusaidia uchumi wa nchi na ustawi wa jamii. Kumbe inatumika kufanya mzaha na kujifakharisha.

Ikulu igeuke ofisi kweli kwa ajili ya kusaidia watu kuishi vizuri, hasa kwa kuwa wamekosa msaada wa mawaziri, wakuu wa mikoa, wilaya na kata. Sherehe za utukufu hazina maana yoyote kwa viongozi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: