Ikulu katika mgogoro


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 15 September 2010

Printer-friendly version

KATIBU wa Rais Jakaya Kikwete, Prosper Mbena, ameingia katika mgogoro. Ametajwa kumpigia kampeni mgombea ubunge, Innocent Kalogeris anayewania nafasi hiyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kalogeris anawania ubunge katika jimbo la Morogoro Kusini, mkoani Morogoro.

Taarifa zinasema Mbena amekuwa akiwasiliana na mgombea huyo mara kwa mara na kumnadi kwa baadhi ya wananchi, wakiwamo viongozi wakuu wa chama na serikali.

Lakini gazeti hili lilipowasilina na Mbena ambaye ni msaidizi wa karibu wa Rais Jakaya Kikwete, alikana madai hayo.

Alisema, “Jamani waelimisheni watu. Sheria za nchi si zipo? Kama mtu kafanya makosa si atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria?

“Mimi nipo ofisini kwangu Dar es Salaam. Hiyo kampeni napiga vipi? Hili ni tatizo la elimu. Watu wasitumie majina ya wenzao kufanya mambo yao. Mimi naomba tufikie mahali wananchi waeleweshwe kwamba sheria ni msumeno,” alisema Mbena.

Mbali ya kutajwa kuitisha vikao vya viongozi na baadhi ya wakazi wa jimbo hilo ambavyo vinadaiwa vimekuwa vikiendeshwa Dar es Salaam na Morogoro, Mbena amekanusha kufahamu lolote katika hilo.

Hata hivyo, MwanaHALISI limefahamishwa na watu waliokaribu na Kalogeris, kwamba mwanasiasa huyo ambaye ametokea kuwa DJ – mchezesha disko – amekuwa akitumia jina la Mbena na ikulu kutishia wapinzani wake wa kisiasa.

Tuhuma kwamba Kalogeris anatumia jina la Mbena zimepamba moto mwishoni mwa wiki, baada ya kutokea tafrani kubwa kati yake na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilayani humo.

Chanzo cha taarifa kinasema Kalogeris aliingilia mkutano wa kampeni wa CHADEMA uliopangwa kufanyika katika Kata ya Kawa, ambako mgombea udiwani wa chama hicho, Rajabu Mbwaduke alijeruhuhiwa vibaya baada ya kushambuliwa na wafuasi wa CCM, akiwamo Kalogeris.

Akizungumza na MwanaHALISI juzi Jumatatu, Rajabu alithibitishia gazeti hili kushambuliwa na Kalogeris kwa kile alichoeleza, “msaada wa ikulu.” Tayari tukio hilo la shambulio limeripotiwa polisi.

Inaelezwa kwamba ugomvi huo ulitokea majira ya saa kumi jioni baada ya viongozi wa CCM kuvamia mkutano wa kampeni wa CHADEMA.

“Wale mabwana walikuwa hawana ratiba hapa. Walikuja kutuomba tuwaachie uwanja wetu. Tulipowakatilia wakaanzisha vurumai,” anaeleza kiongozi mmoja wa CHADEMA.

Anasema, “Lakini kwa mshangao mkubwa ilipofika majira ya saa kumi jioni walivamia mkutano wetu. Wao walikuwa na mkutano kijijini Kituga.”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: