Ikulu ya umma au mafisadi?


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 02 September 2008

Printer-friendly version
Rais Jakaya Kikwete

EPA na Richmond ni mchezo mmoja wenye waigizaji walewale. Hata Rais Jakaya Kikwete anajua hivyo.

Ni kutokana na uelewa huo wa rais, alipoona watuhumiwa katika Richmond wananing’inizwa, akateuwa walewale kumsaidia kuchunguza katika EPA.

Kwa hali hiyo, nani atabaki na chembe ya mashaka, kwamba Waziri Mkuu Mizengo Pinda, hawezi kupata ujasiri wa kukemea wahusika katika Richmond?

Februari mwaka huu, Bunge liliagiza serikali kuchukua hatua dhidi ya wote waliohusika katika kuliingiza taifa katika mkataba wa kinyonyaji wa Richmond.

Lakini taarifa ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, aliyoitoa bungeni Alhamisi iliyopita, kwa mara nyingine, imeonyesha sura halisi ya serikali.

Kwamba pamoja na Rais Kikwete kujitapa kwa wananchi akisema atajenga serikali makini, yenye uwezo wa kupambana na rushwa na ufisadi, anachokifanya ni kinyume na kile alichoahidi.

Ripoti iliyotolewa bungeni na Waziri Mkuu Pinda, imekuja miezi sita baada ya Bunge kuagiza serikali kuchukulia hatua watuhumiwa wa Richmond.

Badala ya serikali kuja na orodha ya wahusika waliochukuliwa hatua, inaishia kusema “wahusika tayari wameandikiwa barua za kujieleza na tayari wamefanya hivyo.”

Je, hiki kama si kilio cha kuonyesha kushindwa kutekeleza maagizo ya Bunge ni nini basi? Pinda anataka muda zaidi wa kushughulikia suala hilo. Hajasema muda gani – mwaka mmoja, miwili, mitatu, au muongo mmoja.

Je, nani asiyejua kwamba Richmond Development Company (LLC), kampuni ambayo haikuwa na uwezo hata wa kuweka balbu ya umeme wa majumbani, ilipewa kazi katika mazingira tatanishi? Waliosaidia kufanikisha hilo wanafahamika hata kwa majina.  

Serikali imesema, katika kutekeleza maagizo ya Bunge, kuwa imeagiza vyombo vya dola kuchunguza waliokuwa mawaziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha kama walihusika na vitendo vya rushwa.

Serikali haijasema kama aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa atachunguzwa. Kamati Teule ilisema Lowassa ndiye aliyeshinikiza na kutoa maagizo ya Richmond kupewa zabuni; na kwamba ndiye alikaidi maagizo halali ya Baraza la Mawaziri kwa kuamua kuipa kazi Richmond.

Kuna wakati Dk. Msabaha, Karamagi na Lowassa, walijikuta wakiwa “wasemaji wakuu” wa Richmond kana kwamba wanalipwa. Kuna wakati pia Lowassa  alitaka kuzuia wananchi kujadili Richmond.

Katika mazingira hayo je, haipaswi kuchunguza Lowassa kama kweli alifanya hayo bila kusukumwa na kitu chochote? Si uchunguzi huu ungesaidia kumsafisha Lowassa mbele ya jamii?

Lakini wakati serikali inasema inafuatilia kwa karibu suala hili, mpaka sasa bado wale wanaotuhumiwa wanaendelea na kazi zao kama kawaida.

Kwa mujibu wa taratibu na sheria za kazi, mtumishi yeyote ambaye anatuhumiwa huchukuliwa hatua ya ama kusimamishwa kazi wakati suala lake linashughulikiwa, kuondolewa madaraka kwa kipindi cha uchunguzi au hufunguliwa mashitaka.

Bali katika Richmond watuhumiwa wanaendelea na kazi zao kana kwamba hakuna lililotendeka. Baya zaidi ni kwamba unakuta rais ameteua watuhumiwa wa Richmond kushughulikia watuhumiwa wa EPA.

Siyo rahisi, kwa mtu makini, kuamini kuwa rais yuko makini katika suala la Richmond na EPA. Hii ndiyo maana pia Waziri Mkuu Pinda hawezi kufanya lolote isipokuwa kuuma na kupuliza.

Na hilo la EPA linaloshughulikiwa na watuhumiwa, bado halijapata ufumbuzi na huenda likamgharimu rais hadhi yake mbele ya jumuia ya kimataifa.

Mpaka sasa hakuna uhakika iwapo fedha zilizokwapuliwa zimerudishwa. Hii ni kutokana na mgongano wa kauli kati ya serikali na BoT.

Wakati Kikwete anasema tayari serikali imekusanya kiasi cha Sh. 53.7 bilioni, CCM walishatangaza kuwa zimekusanywa Sh. 64 bilioni na Waziri wa Fedha Mustafa Mkullo aliishatangaza kauli ya Kamati ya Rais kuwa zimekusanywa Sh. 60 bilioni.

Mkanganyiko wa EPA unaongezeka kutokana na kugundulika kuwa watu muhimu katika sakata hili hawakuhojiwa na Timu ya Rais iliyochunguza ukwapuaji.

Taarifa zinasema waliohojiwa ni watu wa kati na hivyo wengi wao hawana uwezo wa kurudisha fedha walizochotewa. Aidha, kuna madai kuwa badhi ya fedha hizo zilitumika katika kampeni iliyomuweka madarakani Rais Kikwete.
   
Utata huu ndio unafanya kuwepo mashaka makubwa juu ya akaunti ya siri ambamo rais anasema zitawekwa fedha zinazorejeshwa.

Vilevile serikali imesema hadi 31 Oktoba mwaka huu, kiasi cha Sh. 90 bilioni zitakuwa zimerejeshwa. Hii ina maana kwamba serikali haisemi juu ya Sh. 40.2 bilioni iwapo zitarudishwa au ndiyo imeridhia zitokomee.

Kuna jambo moja muhimu ambalo haliwezi kupuuzwa. Rais Kikwete hakuliambia bunge, taifa na dunia, kwa nini serikali ilikataa ushauri iliyopewa wa kuacha kulipa madeni.

Siyo siri kwamba mwaka 2004 kampuni ya Lazab  Freres, katika ripoti yake juu ya suala la madeni ya nje, ilishauri  serikali na BoT kuacha kulipa madeni ya EPA yaliosalia.

Kampuni hiyo ya ushauri katika taarifa yake ilisema, “Madeni ya EPA yamepitwa na wakati.” Huenda huu ndio ulitumika kama msingi wa kuchota mabilioni ya EPA.

Hadi hapa, imani ya wananchi katika serikali ni ya mashaka. Nayo imani ya wafadhili katika utendaji wa serikali inayoyoma.

Swali moja linabaki bila kujibiwa: Je, Rais Kikwete anaogopa wezi na mafisadi? Kwa nini? Urais wake umetekwa; na ikulu wanakaa waliochaguliwa na waliovamia?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: