Ikulu yaacha Rais, yatetea Makamba


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 17 March 2010

Printer-friendly version
Uchambuzi
Januari Makamba

TUMESIKIA watetezi wa Rais Jakaya Kikwete. Wanasema "Rais Kikwete hajageuzwa mradi."

Lakini kila mwenye akili timamu, akiwamo Rais Kikwete, anajua kuwa wasaidizi wake wanatumia jina lake kwa manufaa binafsi.

Baadhi yao, ni marafiki zake wa karibu. Wengine ni wasaidizi wake na viongozi wateule ndani ya serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Alhamisi iliyopita, ikulu ilitoa taarifa kukana kile ilichoita, “Taarifa potofu” zinazotolewa na baadhi ya vyombo vya habari kumhusu Rais Kikwete.

Ikulu ilikuwa inajibu habari iliyochapishwa na gazeti la kila siku la Tanzania Daima la 11 Machi 2010, lililosema baadhi ya wasaidizi wa rais, “wamemgeuza Rais Kikwete mradi.”

Gazeti lilikuwa linanukuu kilio cha Joseph Mbilinyi, mkurugenzi wa kampuni ya Deiwaka Entertainment aliyetuhumu maofisa wa ikulu kumdhulumu mkataba kati ya kampuni yake na kampuni ya Kimarekani ya No More.

Alisema maofisa wa ikulu walitumia jina la Kikwete kufanikisha njama hizo.

Tarehe 13 Februari 2010, Kikwete alizindua mradi wa kutokomeza malaria kwenye viwanja vya Leader’s Club, jijini Dar es Salaam. Uzinduzi ulibeba kauli mbiu “Zinduka- Malaria Haikubaliki.”

Kigogo wa ikulu anayelalamikiwa na Mbilinyi, ni Januari Makamba, mmoja wa wasaidizi wa karibu wa rais. Huyu ni mtoto wa Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba.

Januari ndiye Mbilinyi anasema ametumia jina la rais kufanikisha malengo binafsi.

Kimsingi malalamiko ya jina la Kikwete kutumika kufanikisha ajenda za kisiasa na hata zile za kiuchumi hayakuanza leo.

Hata Kikwete mwenyewe amewahi kulalamika, kwamba kuna watu wanapita katika baadhi ya majimbo ya uchaguzi na kujinadi kwa kutumia jina lake.

Naye Januari aweza kuhitajika kujibu tuhuma ambazo bila shaka anazijua kwamba alikutana na baadhi ya waandishi na wamiliki wa vyombo vya habari kushawishi kutoandikwa kwa taarifa za wizi wa Benki Kuu (BoT) uliofanywa na kampuni ya Kagoda.

Madai ambayo Januari hajajibu yanasema amewahi kusema, “Nimetumwa na rais kuwaeleza muache kuandika Kagoda kwa kuwa fedha zake zimetumika kumuingiza madarakani.”

Mengi yamesemwa na kufanywa na yaweza kuthibitishwa. Je, mangapi hayafahamiki hata kwa rais mwenyewe? Hapa ikulu inamtetea nani na kwa mantiki ipi?

Katika mazingira haya, watu makini wanajiuliza, nini kimesukuma ikulu kutetea Januari badala ya Kikwete?

Mbona taarifa nzima ya ikulu imejaa shutuma na vitisho kwa vyombo vya habari na wananchi wanaolalamikia watendaji wa ikulu?

Kingine kinachoonekana katika taarifa ya ikulu ni rais kuachwa na shutuma zake kwa miaka nenda rudi. Kwamba anashindwa kushughulikia wanaomzunguuka.

Kwa mfano, hata pale Januari anapokiri kujipa kazi ya kutafuta kampuni ya kufanikisha uzinduzi, ikulu haisemi kwamba hiyo siyo kazi aliyopewa na mwajiri wake.

Ikulu haisemi na wala haitaki kusema, kwamba hatua hiyo inaweza kuwa imemchochea Januari, kama binadamu, kupatwa na tamaa na kutaka kujinufaisha.

Badala yake, taarifa inasema, “…Maofisa wote walioshiriki katika maandalizi ya uzinduzi huo, na kwenye uzinduzi wenyewe, walifanya hivyo kutekeleza maagizo ya rais ya kufanikisha shughuli hiyo na wala si kwa kujinufaisha binafsi.”

Je, nani mwenye uhakika kuwa Januari hakutumia nafasi hiyo kujinufaisha binafsi? Nani alikuwa moyoni mwake hadi kuamua kujiapiza kiasi hiki?

Wala ikulu haisemi uhusiano wa Januari na makampuni aliyoyatafuta. Haijadili uwezekano wa kutumia fursa aliyonayo kujinufaisha.

Ikulu haitaki pia kujadili hatua ya Januari ya kupuuza malalamiko ya Mbilinyi aliyoyapata siku tano kabla ya uzinduzi kufanyika. Haya haitaki kuyajadil.

Aidha, ikulu haisemi kama Januari alifikisha malalamiko aliyosikia kuwa Mbilinyi anataka kuzuia ufunguzi wa tamasha kwa kufungua kesi mahakamani kunakohusika, au aliamua kufa nayo yeye mwenyewe. Kama hakuyafikisha alikuwa na maana gani?

Je, kukalia malalamiko hayo hakutoshi kutilia shaka uamuzi wake? Je, kule kusema malalamiko ya Mbilinyi “hayawezi kuathiri ufunguzi” si kulitosha kumpeleka rais katika jambo ambalo tayari limejaa malalamiko?

Kimsingi malalamiko ya jina la Kikwete “kugeuzwa mradi” yametapakaa kila kona. Hata katika sakata la mkataba tata kati ya serikali na kampuni ya Richmond, tuhuma kwamba jina la rais lilitumika, zilikuwa wazi.

Ni pale baadhi ya wabunge waliponukuliwa wakisema, “rais aliagiza waziri wake mkuu, Edward Lowassa kulindwa hadi mwisho.”

Hata kujiuzulu ghafla kwa Lowassa kulitokana na taarifa hizo, kwamba Kikwete ameapa kufa naye.

Lakini baada ya Kikwete kukubaliana na uamuzi wa Lowassa wa kujiuzulu, wote waliokuwa wanadai Kikwete anamlinda Lowassa, waliishia kufunika nyuso zao kwa aibu.

Kwa upande wa pili, walikuwapo waliosema “tumetumwa na rais” kumtokomeza kisiasa Lowassa kwa hoja kwamba anataka kutumia mwanya huo kufanya mabadiliko serikalini.”

Hata Lowassa mwenyewe wakati alipokuwa kiongozi ametumia jina la rais kutekeleza alichokitaka. Si mara moja wala mbili, alikuwa anahubiri kuwa “nimetumwa na rais, ni agizo la bwana mkubwa, nimetumwa na mwenyekiti.”

Naye Yusuph Makamba anatuhumiwa kutumia jina la rais kufanikisha malengo yake. Ni Makamba aliyenukuliwa akimueleza George Mkuchika, naibu katibu mkuu wake kwamba “mwenyekiti amekasirika sana.”

Hii ni baada ya Mkuchika kumteua Daniel ole Parokwa kuwa katibu msaidizi wa CCM wilayani Hanang.

Katika chaguzi ndogo kadhaa zilizofanyika, vigogo ndani ya CCM wanatuhumiwa kutumia jina la Kikwete kukusanya fedha.

Malalamiko haya yalikuwa makubwa zaidi katika jimbo la Tarime, ambapo baadhi ya wafanyabiashara wamenukuliwa wakimlalamikia mtendaji wa chama kukusanya fedha kwa ajili ya chama kwa kisingizio cha kutumwa na mwenyekiti Kikwete.

Ndani ya jumuiya za chama – UV-CCM, UWT na Wazazi, hali ni hiyohiyo. Viongozi na wapambe wao wanatumia jina la rais kufanikisha mambo yao.

Kwenye uchaguzi wa Chipukizi uliofanyika mkoani Morogoro, tabia ya kutumia jina la Kikwete pia ilijitokeza. Baadhi ya wasaidizi wa rais walinukuliwa wakisema, “Rais ametutuma kumpitisha mtoto wake,” Khalfan Jakaya Kikwete.

Sasa swali la kujiuliza: Wakati haya yote yanafahamika, kwa nini Kikwete anaendelea kunyamaza? Majibu yako mengi. Lakini mawili ni makubwa.

Kwanza, Kikwete hana ushupavu wa kuchukulia hatua marafiki zake wa karibu hata pale ambapo tuhuma juu yao zipo wazi.

Hii ndiyo maana mpaka leo, Kikwete ameshindwa kufikisha mahakamani watuhumiwa wa rada, Kagoda na Richmond.

Suala hili ndiyo msingi wa madai ya wanasiasa na watumishi ndani ya serikali na CCM kutaka Kikwete asigombee tena kipindi cha pili cha urais iwapo tu hatabadilika.

Pili, baadhi ya yanayofanywa na marafiki zake mengi yanaweza kuwa na baraka zake au anayaunga mkono.

Ndiyo maana baadhi yao wanazungumza hadharani kuwa “huyu si mwenzetu” na kwamba “hahitajiki na bwana mkubwa na hayo ndiyo maelekezo yake.”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: