Ikulu yagharimia kuchafua upinzani


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 03 November 2010

Printer-friendly version

IKULU imefadhili matangazo ya kuwachafua wagombea urais wa vyama vya upinzani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, MwanaHALISI limearifiwa.

Walengwa wakuu wa matangazo hayo ya Ikulu walikuwa wagombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa na wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba. 

Matangazo hayo ni yale yaliyochapwa katika vyombo mbalimbali vya habari wiki iliyopita, yakidaiwa kutolewa na muumini mmoja wa dini ya kikristo wa kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) jijini Dar es Salaam. 

Pamoja na mambo mengine, matangazo hayo yalieleza kuwa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Jakaya Kikwete, ni chaguo la Mungu na kwamba wanaotaka kumng’oa madarakani wanashindana na alichokipanga Mungu.

Pia, mhubiri anayedaiwa kutoa waraka huo ambao ulilipiwa ili uchapwe magazetini kama ulivyo, Innocent Bilakwate, anasema vyama vya upinzani pamoja na viongozi wa dini wanahatarisha amani ya nchi. 

Kwa kawaida, matangazo yanayotoka katika vyombo vya habari huwa yanalipiwa gharama kulingana na ukubwa wa tangazo lenyewe na MwanaHALISI lina ushahidi usio na shaka kuwa Bilakwate hakulipia matangazo yaliyotoka magazetini.

Hata hivyo, gazeti hili lina ushahidi kuwa baadhi ya magazeti yaliyotoa tangazo hilo yalielekezwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Salva Rweyemamu.

Mmoja wa watumishi wa miongoni mwa magazeti yaliyochapa tangazo hilo alilithibitishia gazeti hili kuwa ni Salva aliyewaagiza kutoa tangazo hilo.

“Salva ndiye alitutaka kulitoa hilo tangazo. Nasikia hata mtu anayetakiwa kulipia tangazo hilo alisemwa na Salva mwenyewe kwa hiyo hili jambo lina mkono wa Ikulu,” kilisema chanzo cha habari cha gazeti hili.

Alipozungumza na gazeti hili juzi jioni, Salva alikiri kumfahamu Bilakwate “kwa muda mrefu” lakini alikana kuhusika na kuchapwa kwa tangazo hilo magazetini.

“Mimi ningeomba tuelekeze akili zetu kwenye kampeni na uchaguzi unaofanyika siku chache zijazo. Hizo taarifa hazina ukweli.

“Mimi sijahusika kwa namna yoyote na uchapwaji wa hayo matangazo unayosema. Ninamfahamu Bilakwate, kwa nini usimpigie na kumuuliza iwapo mimi ninahusika na lolote?” alihoji Salva.

Gazeti hili lilifanikiwa kuzungumza na Bilakwate kwa njia ya simu juzi jioni na akakiri pia kumfahamu Salva tangu akiwa mwandishi wa habari wa gazeti la RAI.

Alipoulizwa ilikuwaje akakubali tangazo lake lilipiwe na Ikulu wakati yeye alidai alizungumza kwa niaba yake binafsi alijibu, “Sikiliza ndugu mwandishi, mimi nilizungumza na waandishi wa habari pale MAELEZO na nikaeleza yale niliyokuwa nayo moyoni.

“Kesho yake nikashangaa kuona magazeti yakiwa yamechapa taarifa yangu kama ilivyo. Mimi sikuzungumza na gazeti lolote kutaka wanitolee tangazo.

“Ila, kama kwa jinsi hiyo ujumbe wangu utakuwa umefika kila mahali, si kitu kibaya kwangu. Lakini sijui kitu kuhusu nani ametoa matangazo hayo na alikuwa ana nia gani,” alisema.

Bilakwate alisema hata hivyo kwamba hafahamu iwapo kile alichokiandika yeye ndicho hasa kilichotoka kwenye matangazo ya magazetini kwa vile hakupata nafasi ya kuyapitia matangazo hayo.

Lakini muumini huyo analalamikia matangazo hayo kuwa yamemletea tabu dhidi ya waumini wenzake wa TAG ambao hawajafurahishwa na kitendo cha matangazo hayo kutoka katika magazeti mengine na si kwenye gazeti la kanisa lao la “Jibu la Maisha.”

MwanaHALISI lina taarifa kwamba risiti za malipo ya matangazo hayo zilielekezwa kulipwa kwa jina la mmoja wa viongozi wa juu wa CCM aliyekuwa katika timu ya kitaifa ya kampeni.

Miongoni mwa magazeti yaliyochapa tangazo hilo ni lile la Kiswahili la serikali la HabariLeo ambalo Salva anadaiwa kuwa na ushawishi mkubwa kwake.

Ni katika gazeti hilohilo la serikali ambako kulichapwa mahojiano kati ya chombo hicho na Aminieli Mahimbo, mtu aliyejitangaza kuwa mume wa mchumba wa Dk. Slaa, Josephine Mushumbusi.

Gazeti lingine la serikali la Daily News linalotolewa kwa lugha ya Kiingereza, nalo liliwahi kuandika maoni ya mhariri yaliyosema kuwa Slaa hataweza kuwa rais wa Tanzania mara baada ya uchaguzi huu.

Katika tangazo hilo la Bilakwate, muumini huyo alinukuu vifungu mbalimbali vya Biblia katika kujenga msingi wa hoja zake.

Pamoja na mambo mengine, Bilakwate anasema, “Watanzania huu si wakati wa majaribio, nchi haijaribishwi kama baadhi yenu mnavyosema. Je, maafa yatakayotokea kwa miaka mitano Watanzania tutakuwa tayari kuyabeba?”

Anasema Watanzania wasidanganywe na watu wanaotaka kuondoa “amani na utulivu katika nchi yetu. Mungu amesema atatupatia kiongozi bora na mwenye viwango.

“Mungu anasema japo yapo mapungufu kwa kiongozi anayemtaka, bado ataendelea kumsaidia na nguvu zake zitakuwa juu yake ili kwa mkono wa Mungu kiongozi huyo aweze kutenda makuu katika nchi yetu na anamtaka kiongozi huyo amtegemee Mungu aliyemweka na anayeweza kumwondoa, vinginevyo kuna kitu kitamtokea.”

Aidha, Bilakwate anasema, “Mungu anasema, hakuna mamlaka isiyotoka kwake, iwe nzuri au mbaya ameiweka yeye kwa kusudi lake. Wewe ni nani unayenena mabaya juu ya viongozi aliowaweka watuongoze?” 

Waraka huo wenye maneno 1,547 unawashutumu pia viongozi wa dini wanaohubiri siasa katika majukwaa ya kidini ukisema damu za watakaoathirika na uvunjifu wowote wa amani zitakuwa mikononi mwao.

“Maneno yanayosemwa na baadhi ya viongozi wa dini, kama Watanzania watayakumbatia na kuyakubali kwa sababu yametoka kwa viongozi wao wa dini zao, basi wajiandae kwa vita kubwa itakayotokea katika nchi yetu siku si nyingi,” inasema sehemu ya waraka huo.

Bilakwate alimweleza mwandishi wa habari hizi kuwa hajui kila ambacho mwandishi anazungumza na kuongeza:
“Mimi ni mtumishi wa Mungu naweza kuzungumza na yeyote na chochote. Sasa sijui kuna uhusiano gani kati ya mazungumzo yangu na watu na hayo matangazo yaliyotoka kwenye vyombo vya habari.”

Alisema iwapo mwandishi anataka, basi amuulize kuhusu mazungumzo yake na waandishi wa habari au hilo tangazo lake na si alizungumza nini au na nani. 

“Sidhani kama kuna kosa kuzungumza na rais au mtu yeyote anayefanya kazi Ikulu,” amesema Bilikwate.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: