Ikulu yanuka ukabila


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 24 March 2010

Printer-friendly version
Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo

RAIS Jakaya Kikwete sasa anatikiswa kwa tuhuma kwamba ikulu imekumbwa na ukabila, MwanaHALISI limeelezwa. Taarifa zinasema tuhuma hizo tayari ziko mezani kwake na zinamhusu mtendaji mkuu wa ikulu.

Anayetajwa kuhusika na ukabila ni Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo ambaye inadaiwa analinda watu wa mkoa anakotoka – Iringa.

Lakini Luhanjo alipopigiwa simu kutaka kauli yake alijibu kwa sauti ya ukali, “Kwani kama wewe ni mwandishi wa MwanaHALISI ndiyo unipigie simu saa hizi?”

Hiyo ilikuwa Jumamosi saa mbili usiku.

Alipoelezwa kwamba gazeti liko tayari kukutana naye wiki hii wakati wowote atakapokuwa tayari, Luhanjo alijibu, “I will not talk with you for anything (Sitazungumza lolote na wewe).” Alikata simu.

Hata hivyo chanzo cha taarifa hizi kinasema, “Luhanjo amejiimarisha kweli na anaweka watu wake kila eneo na wanataka kujenga himaya yao.”

Luhanjo anahusishwa na upendeleo wa ukabila katika hatua ya serikali kuipa zabuni kampuni ya Peacock Hotels Limited kuendesha mradi wa hoteli katika jengo la Millennium Tower, Kijitonyama, Dar es Salaam.

Inadaiwa Luhanjo ana mkono katika kubeba Peacock Hotels ambayo mmiliki na mkurugenzi mtendaji wake, Joseph Mfugale pia anatoka Iringa.

Lakini Mfugale anakana kubebwa, akisema “Tulishindana tukashinda na kulipa dhamana, tena milioni nyingi – dola 165,000 (Sh. 171 milioni).”

Alisema tatizo la fedha za dhamana walizotoa ni kwamba kulitokea mpango wa kuziiba ili tenda apewe mtu mwingine.

“Waliposhindwa mpango wao, mkurugenzi wa raslimali aliamua kujiuzulu na sasa nasikia amepata kazi mahali pengine,” alidai Mfugale.

Mfugale anasema fedha za dhamana zililipwa kupitia benki ya CRDB, tawi la Kijitonyama.

Millennium Tower inamilikiwa na Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa (LAPF), ulio chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Mbali na Luhanjo, mwingine anayedaiwa kumbeba Mfugale ni Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Maimuna Tarishi ambaye pia anatoka Iringa.

Tarishi ni mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya LAPF. Inadaiwa Mfugale aliwasilisha malalamiko kwa watendaji wa juu wa serikali kwa kile alichodai, “kuhujumiwa katika zabuni.”

Tarishi hakupatikana kutoa maoni yake juu ya madai hayo. Katibu muhtasi wake aliyeko Dodoma alijibu kuwa Tarishi yuko Dar es Salaam na kwamba “simu yake ya mkononi aliisahau Dodoma.”

Awali nyaraka za zabuni za Mfugale ziliwekwa kando kwa madai ya kukosekana dhamana ya benki, jambo ambalo alilalamikia.

Imedaiwa kuwa baada ya Mfugale kulalamika, Luhanjo aliagiza uongozi wa TAMISEMI kufuatilia malalamiko hayo.

Katika malalamiko yake, Mfugale anatuhumu Julius Mfukwe, ambaye alikuwa mkurugenzi wa vitegauchumi wa LAPF, kuchomoa nyaraka zake za dhamana za benki ili kubeba mmiliki wa Hotel ya Paradise.

Tayari Mfukwe ameacha kazi katika mfuko huo na sasa ameajiriwa na Mamlaka ya Bandari nchini (THA).

Alipoulizwa juu ya madai hayo ya Mfugale, Mfukwe alijibu kwa sauti ya upole, “Hii namba yangu umeipata wapi?”

Alipoambiwa kuwa yeye ni mtu mkubwa anayefahamika, alijibu, “Kaka, nakushukuru lakini sina la kusema.”

Alisema, “Mimi sipo huko tena. Siwezi kuongea chochote kinachohusu LAPF kwa kuwa si msemaji wao. Nakuomba uwatafute viongozi wa mfuko ndio watakueleza.”

Hata hivyo, kwa mujibu wa vyanzo vya taarifa kutoka serikalini, wakati wa ufunguaji zabuni ya kuendesha hoteli katika jengo hilo la Millennium Tower, Mfugale hakuwa ametimiza sharti la kuweka dhamana ya benki kama ambavyo tangazo la zabuni liliagiza.

“Zabuni ilifunguliwa hadharani na kuhudhuriwa na kila muombaji. Huyu bwana hakuwa ameweka bond kwenye zabuni yake. Baada ya kuona kwamba amepoteza sifa, akaanza kutafuta msaada,” kimeeleza chanzo cha taarifa.

Kabla ya kukodishwa kwa Mfugale, hoteli ilikuwa inaendeshwa na kampuni ya African Sky kutoka Afrika Kusini. Kampuni inadaiwa iliondoka na deni la dola 400 milioni.

Kwa utuki tu, Mkurugenzi Mkuu wa LAPF ni Eliud Sanga na Meneja Mkuu ni Injinia G. Matovola wote kutoka Iringa.

Kwa muda mrefu mkoa wa Iringa umetoa viongozi katika ofisi ya rais. Kwa mfano, Emilius Mzena, Augustine Mahiga na Hans Kitine wote kutoka Iringa, walikuwa wakurugenzi wa usalama wa taifa.

Aidha, Kitine na Peter Siyovelwa wamewahi kuwa mawaziri ofisi ya rais wanaoshughulikia usalama wa taifa.

Wengine ambao wanatoka Iringa na wako ofisi ya rais; na huenda kwa utuki tu ni Rajab Luhavi na Lumbila Fyataga ambao ni wasaidizi.

Miongoni mwa watu mashuhuri kutoka Iringa ambao wamo katika nafasi za juu kimadaraka nchini ni pamoja na Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu.

Kwa mujibu wa gazeti la kila siku la NIPASHE, Mchechu hakuwa miongoni mwa watu waliofanyiwa usaili kwa kuwa “hakuwa na sifa” ya kupewa kazi aliyoomba.

Mchakato wa kumpata mkurugenzi mkuu wa NHC, ulisimamiwa na kampuni ya Price Water House Cooppers na uligharimu serikali zaidi ya Sh. 82 milioni.

Hata hivyo, pamoja na kwamba Mchechu aliomba nafasi hiyo, hakuwa short listed (kuwa miongoni mwa waliopitishwa kwa kufanyiwa usaili).

“Kwa hiyo serikali imetumia mamilioni ya shilingi za umma kwa kazi ambayo haikuwa na tija, kwa kuwa aliyeajiriwa hakufanyiwa usaili,” ameeleza mjumbe mmoja wa bodi iliyomaliza muda wake.

Amesema serikali imelipa kampuni ya ushauri ya Price Water “lakini kazi yote iliyofanyika imetupwa kapuni.”

Taarifa za baadaye zimesema kuwa uongozi wa NHC tayari umeidhinisha Mchechu kulipwa mshahara wa dola za Marekani 11,000 (Sh. 14 milioni) kwa mwezi, jambo ambalo linatajwa kuwa linaweza kuangamiza hata shirika lenyewe.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa, Mchechu ameacha malipo ya dola 16,000 kwa mwezi katika Benki ya Biashara Afrika (ABC) ambako alikuwa anafanyakazi.

Haikufahamika kwa nini ameamua kuacha kazi penye mshahara mkubwa kuliko ule atakaokuwa anapata NHC.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: