Ikulu yapuuzia afya ya Kikwete


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 23 December 2009

Printer-friendly version
Mwenyewe akata anga na mbuga
Atenda kinyume cha daktari wake
Rais Jakaya Kikwete

AFYA ya Rais Jakaja Kikwete imo hatarini kufuatia kupuuza masharti ya daktari wake ya kupunguziwa kazi na kupumzika, MwanaHALISI limeelezwa.

Miezi mitatu iliyopita, daktari wa rais, Dk. Peter Mfisi alisema rais ameshauriwa kupumzika, kupunguziwa safari na kwamba ratiba yake ya kazi ingerekebishwa kulingana na afya yake.

Hata hivyo, katika siku za karibuni, rais ameendelea kukata mbuga kana kwamba hajawahi kupewa tahadhari au hajakumbwa na masahibu.

Shughuli za rais zifuatazo na kwa tarehe zinazokaribiana, zinaonyesha ama kupuuza au kutokuwa makini kuhusu hali ya afya ya mkuu wa nchi.

Kwa mfano, tarehe 5 Novemba rais Kikwete alihudhuria kongamano la wadau wa maendeleo lililofanyika nchini Italia kwa siku mbili kabla ya kwenda Misri, 10 Novemba 2009. Alirejea nchini siku tatu baadaye.

Rais Kikwete aliondoka nchini 15 Novemba 2009 kwenda Italia ambako alihutubia mkutano wa kimataifa wa chakula duniani. Aliondoka huko 19 Novemba 2009.

Tarehe 20 Novemba 2009, rais alipokea Kombe la Dunia katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam na siku iliyofuata alienda mkoani Arusha katika maadhimisho ya miaka 10 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kikwete alikuwa Arusha hadi 24 Novemba 2009.

Siku mbili baadaye rais aliondoka kwenda ziara ya kikazi nchini Jamaica, Trinidad na Tobago kabla ya kwenda nchini Cuba.

Kutoka Cuba, Kikwete alinyosha moja kwa moja hadi Marekani. Alirejea nchini wiki moja iliyopita.

Alhamisi iliyopita, Rais Kikwete alianza ziara ya kikazi katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha. Akiwa mkoani Kilimanjaro, Kikwete alifungua Chuo cha Utalii cha Mweka na kwenda eneo la Mamba Miamba, wilayani Same ambako watu 24 walifariki kutokana na kuporomokewa miamba.

Rais Kikwete aligoma kutumia usafiri wa helikopta ili kumrahisishia safari kati ya Mamba Miamba na Arusha, mwendo wa saa sita kwa gari.

Akiwa mkoani Arusha, pamoja na kufungua hoteli ya kitalii ya Snowcrest, Kikwete alikwenda chuo cha kijeshi, Monduli ambako alitunuku vyeo vya Luteni Usu kwa maofisa waliohitimu.

Baadaye Jumapili asubuhi rais aliondoka kuelekea mkoani Ruvuma ambako aliongoza maombolezo ya mwanasiasa mkongwe nchini, Laurance Gama.

Imefikia wakati baadhi ya wafanyakazi ikulu wamedai kuwa rais hapumziki kwa kuwa wanaopanga safari zake wananufaika na safari hizo kwa posho na marupurupu mengine.

Msemaji wa ikulu, Salva Rweyemamu aliliambia MwanaHALISI juzi Jumatatu, kuwa rais “ndio ameanza mapumziko wiki hii,” karibu miezi mitatu tangu apewe ushauri wa mtaalam wa afya yake.

Rweyemamu hakusema iwapo ni rais aliyekuwa anakaidi mapendekezo ya mtaalam au washauri wake ndio wamekuwa wakishinikiza aende kila mahali.

Dk. Mfisi alisema Oktoba kwamba uchovu uliokithiri ndio ulikuwa chanzo cha Rais Kikwete kupoteza nguvu huko Mwanza, tarehe 4 Oktoba mwaka huu, ambapo alishindwa kuendelea na hotuba na kuripotiwa kuanguka.

Alisema, “Mimi na wenzangu katika Ofisi Binafsi ya Rais (OBR) tumejifunza na tumeazimia kuwa waangalifu zaidi katika kupanga ratiba ya kazi za rais.”

Hata hivyo, tangu itolewe taarifa hiyo, 8 Oktoba 2009, Kikwete amekuwa “kiguunjia,” akikata anga na nchi kavu.

Siku tisa baada ya tukio la Mwanza (Oktoba 13) Rais Kikwete alianza safari ya siku mbili mkoani Mara ambako alikwenda kwa shughuli za kuzima mwenge na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo.

Kabla ya kwenda Mwanza ambako rais alikumbana na masahibu hayo, 2 Oktoba 2009, Kikwete alikwenda Arusha kufungua mkutano wa Wabunge wa Jumuiya ya Madola.

Baadae jioni ya 2 Oktoba 2009, rais alishiriki hafla ya chakula cha jioni alichowaandalia wabunge wa bunge hilo. Aliondoka saa sita usiku kwenda kupumzika.

“Hatuna hakika alilala saa ngapi, kwani najua akiwa na kazi huchelewa sana kulala,” ilisema sehemu ya taarifa ya Dk. Mfisi.

Taarifa zinasema 3 Oktoba 2009, Kikwete alifanya kazi mfululizo ambapo alikutana na viongozi na wananchi mbalimbali wa mkoa wa Arusha kabla ya kuondoka jioni yake kwenda Mwanza.

“Alipofika Mwanza alikuwa na mazungumzo na wenyeji wake usiku ule mpaka saa nne ya usiku. Tulipofuatilia tuligundua kuwa hata siku hiyo nayo alichelewa sana kulala kwani walipoondoka wageni, yeye aliendelea kushughulikia hotuba yake mpaka karibu na alfajiri,” taarifa ya serikali ilisema.

Kwa mujibu wa vyanzo vya MwanaHALISI, 17 Oktoba 2009, Rais Kikwete alihudhuria harambee ya kuchangia ujenzi wa kiwanda cha Tangawizi, kilichopo katika wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro. Harambee iliandaliwa na mbunge wa Same Mashariki (CCM), Anne Kilango Malecela.

Tarehe 26 Oktoba 2009, Rais Kikwete alianza ziara ya siku sita ya kikazi katika mikoa ya Iringa na Mbeya. Akiwa katika mikoa hiyo, rais alizungumza na wananchi, kukagua miradi ya maendeleo na kufanya mikutano kadhaa ya hadhara.

Siku nne kabla ya rais kuanguka, aliondoka New York nchini Marekani. Hiyo ilikuwa 30 Septemba 2009.

Taarifa ya serikali ikikariri Dk. Mfisi ilisema kwamba Rais Kikwete aliondoka nchini humo saa nane za usiku kwa saa za Tanzania. Aliwasili nchini tarehe 1 Oktoba 2009.

Inaelezwa kwamba wakati akirejea nyumbani, Rais Kikwete alisimama mjini London, Uingereza na Nairobi nchini Kenya ambako aliunganisha ndege. Safari ya jumla ya Kikwete kutoka Marekani hadi Tanzania ilichukua saa 24.

MwanaHALISI lilipomuuliza Rweyemamu juu ya mapumziko ya rais, alisema ni kweli rais alishauriwa kupumzika, na kwamba ameanza kutekeleza ushauri huo juzi Jumatatu, karibu miezi mitatu baada ya kuishiwa nguvu.

“Ni kweli rais alishauriwa apumzike na ameanza kupumzika leo (juzi Jumatatu),” alisema Salva katika mahojiano yake kwa njia ya simu na MwanaHALISI.

Alipoulizwa atapumzika kwa muda gani, Salva alisema, “mpaka utakapokwisha mwaka huu na kuingia mwaka ujao.” Salva hakusema mahali ambako rais atapumzikia.

Katika mazingira ya kuaza kujihami kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwakani, hakuna uhakika kwamba rais atapumzika kwa maana ya neno hilo.

“Hata kama hakuhutubia mikutano ya hadhara au kwenda safari ndefu, atabughudhiwa kwa ugeni wa watu mbalimbali wanaofika kumwona nyumbani,” ameeleza mmoja wa maofisa ikulu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: