Ilani ya CCM inadanganya


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 15 September 2010

Printer-friendly version
Mgombea Urais wa CCM, Jakaya Mrisho Kikwete

ILANI ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2010 imesheheni takwimu zinazokinzana, imegundulika.

Katika ilani hiyo, ambayo anatumia mgombea Jakaya Mrisho Kikwete kuomba ridhaa ya kuendelea na urais, inaelezwa kuwa uchumi umekua kutoka asilimia 4.5 mwaka 2005 hadi asilimia 6.7 mwaka huu.

Lakini takwimu za serikali na washirika wake – Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha duniani (IMF) zinaonyesha kuwa kiwango cha asilimia 6.7 kilifikiwa mwaka 2005 na siyo mwaka huu.

Hata kiwango cha asilimia 4.5 ambacho inadaiwa ndicho utawala wa Kikwete ulianza nacho mwaka 2005, hakipo, kwani tayari wakati huo, serikali iliyokuwa inamaliza ngwe yake ilikuwa tayari imefikia asilimia 6.7.

Kwa hiyo, ilani ya uchaguzi ya CCM mwaka huu ilipaswa kuonyesha utendaji wa serikali – kufaulu au kushindwa – kuanzia asilimia 6.7 kwenda juu au kurudi chini. Haifanyi hivyo.

Ripoti ya WB ya mwaka 2007 kuhusu biashara na uchumi nchini ilisema, “…uchumi wa Tanzania ulikuwa ukikua kwa wastani wa asilimia tano hadi sita katika kipindi cha kuanzia mwaka 1995 hadi 2005.”

Basil Mramba, aliyekuwa waziri wa fedha katika serikali ya Mkapa, aliuambia mkutano wa mwisho wa bunge la bajeti (2005) mjini Dodoma, kwamba “uchumi wa taifa umekua kwa asilimia 6.7.”

Alisema, “Mheshimiwa Spika, utawala wa Awamu ya Tatu umepata mafanikio makubwa ya kiuchumi. Kwa mfano, uchumi umekuwa kutoka asilimia 4.2 mwaka 1996 hadi asilimia 6.7 mwaka 2005.”

Kwa mantiki hii, miaka mitano ya utawala wa Kikwete imekuwa ya makitaimu; bado uchumi uko palepale alipouacha rais mstaafu Benjamin Mkapa. Hii ina maana Kikwete ameshindwa kuinua uchumi wa nchi.

Kuhusu Mahakama ya Kadhi, ibara ya 108 (b) ya ilani ya mwaka 2005 iliahidi “kulipatia ufumbuzi” suala hilo, lakini hadi sasa imeshindwa kufanya hivyo.

Lakini suala hilo halimo kwenye ilani ya sasa ya uchaguzi. Bali suala hilo liliuawa pale Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe, aliposema serikali imeamua kuliacha kwa wenye dini yao (Waislamu) walishughulikie kwa vile serikali haina dini.

Naye, makamu mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa, amesema ilani haikuwa imeahidi kuanzisha mahakama hiyo; bali hatua ya kutaka Waislamu waianzishe wenyewe ndiyo ufumbuzi uliozungumzwa kwenye ilani.

Alibanisha kuwa serikali ilifanya kazi kupitia Tume ya Kurekebisha sheria ambayo ilishauri kwamba haitakuwa sahihi kwa Mahakama ya Kadhi kuundwa na serikali kwa kuwa ni suala linalohusu taratibu za dini ya kiislamu.

Hili linadhihirisha kuwa baadhi ya vipengele au sehemu kubwa ya ilani ya CCM huandaliwa bila kufanyiwa utafiti.

Ilani hiyo iliyomwingiza madarakani Kikwete pia iliahidi kupitia ibara ya 111 (f) kwamba itaanzisha na kutoa vitambulisho vya taifa katika kipindi cha kati ya mwaka 2005 hadi 2010. Hilo halijatekelezwa na serikali ya Kikwete na halimo katika ilani ya sasa.

Kwenye tasnia ya habari, ilani ya mwaka 2005 iliahidi kuinua ubora wa taaluma ya habari kwa kushirikiana na wamiliki wa vyombo vya habari vya binafsi.

Hata hivyo, katika kipindi hicho, magazeti mawili maarufu, KULIKONI na hili la MwanaHALISI, yalifungiwa na serikali kwa madai ya kuandika habari zilizodaiwa kukiuka maadili.

Ni katika kipindi hichohicho, magazeti ya binafsi yamekuwa yakipata shida kupata matangazo ya serikali huku yale yanayodaiwa kuwa na msimamo mkali dhidi ya serikali, yakinyimwa matangazo.

Katika kile wanachoita mafanikio ya kiuchumi, ilani ya mwaka 2010 inadai kwamba katika miaka mitano iliyopita, mfumuko wa bei uliendelea kuwa wa “tarakimu moja” – haukufikia asilimia10.

Bali taarifa sahihi zinasema mfumuko kwa sasa ni asilimia nane (8) wakati Kikwete akiingia madarakani ulikuwa asilimia nne (4).

Kuhusu vijana, ilani ya CCM inatamka katika ibara ya 80 (i) kwamba serikali itaandaa mafunzo maalumu kwa vijana, ya kupenda kufanya kazi na kuwa waadilifu ili waweze kuajirika.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: