Imewezekana Marekani, Inawezekana Tanzania


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 11 February 2009

Printer-friendly version
Barack Obama

MACHO yetu yameshuhudia historia ikiandikwa na itasimuliwa vizazi na vizazi.

Uchaguzi na hatimaye kuapishwa kwa Barack Obama kuwa rais wa 44 wa Marekani vimeandika ukurasa mpya wa historia na mahusiano.

Kwa mara ya kwanza, mtu mwenye asili ya Afrika amechaguliwa kuliongoza taifa lenye watu wengi weupe – Marekani.

Wengine waliweza kuona jambo hili, lililotokea 20 Januari 2009 kuwa linawezekana lakini kwa miaka mingi baadaye. Wengine walifikiria hata miaka mia moja baadaye.

Lakini mtu mwenye njozi sahihi, Martin Luther King Jr., aliliona hilo likitokea chini ya miaka 40. Wamarekani wamekataa utawala wa Chama cha Repablikani, uongozi wake, sera zake, na misimamo yake.

Wamesema wanataka kuanza upya, chini ya chama kingine, chenye sera tofauti, chenye misimamo tofauti na chenye uongozi tofauti na ule uliopo; hata kama mgombea wa chama hicho ni mtu mweusi. Matakwa yao yameheshimiwa.

Waliokuwa na sera za vitisho na itikadi za hofu walijikuta wanasalimu amri mbele ya wenye sera za matumaini na itikadi za mabadiliko.

Tuliyoshuhudia yaweza kukosa maana endapo hatutayaangalia kwa mwanga wa watu wa Tanzania.

Je, kuikataa serikali iliyoko madarakani kwenye sanduku la kura ni kukosa uzalendo? Je, kuipinga serikali yenye vyombo vya dola na amiri jeshi mkuu ni kuleta chuki kwa wananchi?

Je, kumpinga rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuonesha kuwa uwezo wake wa kuongoza ni mdogo au maamuzi yake ni ya utata ni kumvunjia heshima? Je, serikali inapotoa matamko au sababu ya kufanya jambo wananchi wakubali tu na wasishuku au kuhoji zaidi?

Jibu tuliloliona Marekani, kwa maswali yote hayo ni moja, HAPANA!

Mtu anaweza kuwa mzalendo na asikubaliane na uongozi ulioko madarakani. Mtu anaweza kuipinga serikali bila kuwa kwenye chama cha upinzani. Mtu anaweza kuikosoa serikali na chama kilichoko madarakani bila kuonekana kibaraka wa maslahi fulani. Ndiyo, na sisi tunaweza.

Tunaweza kubadilisha mwelekeo wa taifa letu kwa kuamua kukataa uongozi na chama kilichoko madarakani. Tunaweza na tuna wajibu wa kushawishi watu wengi zaidi kwa nguvu za hoja, kwamba kutoendelea kwa Tanzania kunahusiana moja kwa moja na utawala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kufanya ushawishi wa aina hii siyo usaliti; siyo “kupandikiza chuki;” siyo “uhaini;” siyo “kutishia amani, umoja na mshikamano.” Ni wajibu wa kila mwenye dhamira njema na anayelitakia mema taifa letu.

Tunaposema hayo hatuna maana kuwa wana-CCM ni watu waovu, mafisadi na kwamba wote ni wachafu. La hasha! Hatuwezi na hakika hatupaswi.

Matukio ya karibu mwaka mmoja uliopita kule Bungeni na mjadala ambao umeendelea kitaifa, unatudhihirishia kuwa wapo wana-CCM ambao wanaipenda nchi yao.

Wapo ambao wako tayari kuweka hatarini majina yao, vyeyo vyao na majimbo yao ili kutetea maslahi ya taifa. Hata hivyo kundi hili ni la wachache na nguvu zao zinategemea sana hisani ya wale walio “juu.”

Tulichoshuhudia Marekani ni kuwa nguvu ya kutawala na mamlaka ya kutawala yaani hakimiya (sovereignty) katika nchi ya kidemokrasia, hutoka kwa watu (raia).

Watawala walioko madarakani hawako hapo kwa sababu walipigiwa kura na malaika au waliwekewa mikono na mizimu ya mababu. Tumewaweka sisi.

Watu wa Marekani walijua kuwa utawala wa Rais George Bush, kwa miaka minane ni matokeo ya wale asilimia karibu 50 ya Wamarekani waliompigia kura mwaka 2000.

Hakika utawala wake uliakisi matamanio, njozi, na maono ya wapiga kura hao na kimsingi ulitokana na waliompigia kura.

Vivyo hivyo hapa kwetu Tanzania. Kuna watu wanashangazwa na kiburi cha utawala na jinsi ambavyo rais anaweza akasema maneno ya kejeli kama aliyoyasema kule Pemba siku chache zilizopita.

Rais alinukuliwa akisema, “Tutamwendeleza kila mtu kwa sababu dhamana ya maendeleo ni yetu katika serikali. Hawa wengine hawana serikali. Kazi yao, na wabunge wao, na wawakilishi wao, ni kufoka tu. Sisi ndio wenye dhamana ya serikali na wala hatubagui”.

Bila shaka kuna watu waliompigia makofi kwa maneno hayo bila ya kuyapima kwa ukaribu.

Ukweli ni kwamba siyo jukumu la serikali kumwendeleza mtu yeyote yule. Natamanni nielezee hapa jukumu la serikali ni nini; lakini kwa vile watawala wamesahau fikra za Nyerere na hawana pa kushikilia.

Nawashauri watafute hotuba yenye kina sana ya Mwalimu isemayo “Serikali ni ya nini?” Labda wanaweza kukumbushwa jukumu la serikali.

Zaidi ya yote Rais anapofikia mahali na kusema jukumu la watu waliochaguliwa na wananchi kuwa ni “kufoka” tu, anakuwa ameonesha kilele cha kejeli za kisiasa na dharau kwa mchakato wa demokrasia.

Kama waliochaguliwa na wananchi kupitia tiketi za upinzani kazi yao ni “kufoka tu” na wao (kina Kikwete) ndiyo wenye dhamana ya serikali, sasa kwa nini asiamue kufuta vyama vya upinzani tu?

Kuna maana gani kutumia gharama kubwa ya uchaguzi na ruzuku kutoka fedha za walipa kodi kuwalipa “wafokaji?”

Tumeshuhudia wananchi wa Marekani wakiikataa serikali yao na kuileta nyingine. Siyo kwa sababu Bush hakujenga barabara, kuleta maji au umeme; bali wananchi wa Marekani waliamua kuikataa na kumchagua Obama na serikali mpya, kwa sababu wanahitaji mabadiliko zaidi.

Hivyo kuikataa CCM na serikali yake siyo kwa sababu hawakuleta visima viwili au vitatu au hawakujenga barabara inayoteleza “kama mgongo wa ngisi.”

Tunapaswa kuikataa kwa sababu serikali ya CCM ni chanzo na sehemu ya matatizo ya kutokuendelea kwetu.

Tukijumlisha majigambo yao yote ya “maendeleo,” Tanzania bado ni miongoni mwa nchi maskini zaidi duniani kwa kila kipimo.

Tumeona basi kuwa tunaweza kuikataa CCM, sera zake, itikadi zake na kuipenda Tanzania zaidi. Tunaweza kukataa chama kizima na kumkubali mtu mmoja mmoja kwa kuangalia sifa zao.

Ni kama alivyofanya Obama aliyemenyana na John McCain na kumshinda lakini baadaye akachagua mmoja wa wanachama wa Repablikani kuwa Waziri. Hili hata sisi tunaweza. Tunaweza kukiweka CCM pembeni na kuwakubali watu binafsi ambao tunajua ni wana-CCM.

Tunaweza kuipinga serikali. Hatulazimiki hata chembe kuimba sifa za serikali hiyo kama maroboti. Haya ni mapambano ambayo ushindi wake hauji kwanza kwenye sanduku la kura mpaka yapitie kwenye sanduku la akili.

Wananchi wakitaka mabadiliko wanaweza kuyaleta wao wenyewe. CCM inaweza kuangushwa baada ya wananchi kutambua kuwa ndiyo chanzo cha wazi cha kudumaa kwa Tanzania.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: