Ingekuwa vipi Otieno mbele ya Maximo?


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 09 June 2009

Printer-friendly version

KAMA angekuwa Mtanzania, bila shaka mashabiki wa soka nchini wangekuwa wameshamsahau beki mahiri Musa Otieno Ongao.

Sababu kubwa ni umri, kwani kwa sasa ana miaka 35, lakini ni mmoja wa nyota mahiri katika kikosi cha timu ya taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’.

Umahiri wake unathibitika kuitwa kwake na kocha Mjerumani anayeinoa Harambee Stars, Antoine Hey.

Kocha huyu hana masihara. Ndiye aliyewatema nyota wa Yanga, Boniface Ambani, Mike Barasa na hata Bernard Mwalala.

Si kwamba Ambani na wenzake wamepwaya, lakini mbele ya Mjerumani huyo hawana nafasi. Ikumbukwe hawa ndio lulu ya Yanga katika safu ya ushambuliaji.

Amewaacha vijana hao wasiozidi miaka 26, lakini akimrudisha mkongwe Otieno anayecheza soka Marekani katika klabu ya Cleverland City Stars iliyomuazima kutoka Santos FC ya Afrika Kusini.

Otieno aliyeanza kuichezea Harambee Stars tangu akiwa na miaka 19, ameitwa baada ya kuachwa kwa miaka miwili.

Hey amekunwa na nini kwa Otieno na wakongwe wengine kama Robert Mambo (31) anayeichezea ya GIF Sundsvall ya Sweden, Duncan Ochieng (31) na Edgar Ochieng (32) wa Mathare United?

Hakuna shaka kwamba, ameangalia zaidi uwezo na vipaji vya wachezaji, akiamini wataisaidia nchi yao kujaribu bahati ya kucheza fainali za Kombe la Dunia mwakani huko Afrika Kusini.

Kwa bahati mbaya Hey amekung’utwa 3-0 na Nigeria mwishoni mwa wiki, lakini hilo haliwezi kumkatisha tamaa, kwani Nigeria iko juu mno kisoka ikilinganishwa na Kenya.

Wakati haya tukiyashuhudia kutoka kwa jirani zetu Kenya, hapa nyumba Tanzania, timu ya taifa `Taifa Stars’ inasukwa upya, eti kwa madai wengi waliokuwa wanauonda kikosi hicho na hata kukiwezesha kufuzu kwa fainali za CHAN ni ‘wazee’.

Nani kasema kikosi cha Maximo kilijaa wazee kiasi cha kustahili kufumuliwa chote badala ya kuwachanganya na wengi wa damu changu kiweze kuwa endelevu?

Hata England, kuna damu mchanganyiko, za wazee kama Gary Neville (34), Emily Heskey (31), David James (38) na idadi kubwa ya wachezaji wanaonusa umri wa miaka 30. Mchezaji mwenye miaka 20, Theo Walcott ndiye mdogo zaidi.

Huko Italia, mabingwa hao wa Dunia kikosi chao pia kinaundwa na wazee wengi ambao wanatumia uzoefu wao kuipeperusha bendera ya Italia.

Angalia `wazee’ kama Fabio Cannavaro ana miaka 35, kipa Gianluigi Buffon (31), Gianluca Zambrotta (32),  Gennaro Gattuso (31), Mauro Camoranesi (32), Andrea Pirlo (30), Luca Toni (32) na wengine.

Hata hivyo, kikosi kimechanganywa damu changu kama za akina Marco Motta (23), Salvatore Bocchetti (22), Davide Santon (18) Alberto Gilardino (26), Giuseppe Rossi (22), waweze kujifunza kutoka kwa kaka zao.

Kwa staili hii, wana uhakika wa kuwa na kikosi kilichoiva kikweli kweli miaka nenda miaka rudi.

Kama wenzetu wanaona mbali kiasi hiki, inakuwaje hapa kwetu mchezaji anayekaribia miaka 30 aonekane mzee, tena asiye na msaada kwa timu?

Abdi Kassim (28) na wenzake kama Said Maulid `SMG’, Godfrey Bonny, Fredy Mbuna, Ivo Mapunda, walistahili kustaafishwa mapema kuitumikia nchi yao?

Katika hili, tunadhani kocha ameteleza, alipaswa na bado anapaswa kuchanganya damu.

Maximo hajachelewa, asiibomoe timu yake, lakini ajaribu kuchomekea wazoefu wengine ili hata kwa wakati huu anaojenga timu ya ushindi katika siku za usoni, bado Tanzania iwe tishio.

Itafurahisha kuona timu inajengwa, lakini kila kukicha Watanzania wakiwa wenye furaha kwa matokeo ya uwanjani kuliko staili hii ya ushindi wa kuvizia kama ilivyokuwa katika mchezo dhidi ya New Zealand.

Ni kweli Stars ilicheza vizuri dhidi ya New Zealand, hasa kipindi cha pili lakini inaonyesha bado ina safari ndefu ya kuweza kucheza kitimu, wote wakiwa na lengo moja.

Stars ya sasa haionekani kujiamini, ndiyo maana inakubali kufungwa mabao ya mapema, na inapoamua `kuchanganya uwanjani’, kila mmoja anatumia uwezo binafsi kuitafutia timu ushindi.

Kama ukweli ndio huo, hakuna sababu za kuwa na papara ya kuwakomaza haraka vijana hawa, hivyo wachanganywe na wenzao ili waendelee kujifunza na kukomaa katika soka halisi ya ushindani.

Ndiyo maana najiuliza, kama Musa Otieno angekuwa Mtanzania, Maximo angemtupia jicho kwa ajili ya kikosi chake? Tukubaliane kutokubaliana kwamba, umri usiwe kigezo cha kuwatema wakongwe, bali uwezo kwanza.

0
No votes yet