Intelijensia ya polisi isiyo intelijensia


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 12 January 2011

Printer-friendly version
IGP Said Mwema

MFUMO wa watawala wa kukusanyia na kusafirishia taarifa, hasa za “usalama,” umeziba. Aliyeuziba anafahamika. Ni CCM au kwa jina maarufu la utani, “chama cha mapinduzi.”

Polisi, vyombo vingine vya ulinzi na usalama na serikali, huita mfumo huu intelijensia – yenye maana ya: a-kishushushu, a-kiakili, mahususi, a-kutafiti/kuchunguza, enye stadi, makini, nyemelezi, nusanusa, a-kuwahi.

Said Mwema, inspekta jenerali wa polisi (IJP), akiongea na vyombo vya habari mjini Dar es Salaam wiki iliyopita, alisema alikuwa na “taarifa za kiintelijensia” kuwa kutatokea vurugu iwapo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kitafanya maandamano mjini Arusha.

Maandamano yalianza. Yalikwenda kwa karibu kilometa mbili. Hakukuwa na vurugu. Hata kama zingekuwepo, tayari IJP alikuwa ameongeza askari kutoka Moshi, Manyara na Tanga ili kuimarisha ulinzi mjini Arusha.

Hivyo, kwa kilometa mbili za maandamano, intelijensia ya Mwema ilikuwa imefeli. Wananchi waliona. Polisi waliona. Viongozi wa CHADEMA walishuhudia.

Sasa katika hatua za kwanza za kilometa iliyosalia kuingia uwanja wa National Milling, ama kwa kuagizwa au kwa utashi binafsi, baada ya kuona hakukuwa na vurugu, baadhi ya polisi wakaanzisha ghasia – wakavuruga maamdamano ya amani kwa njia ya kuyazuia.

Hiyo haikutosha. Wakadondosha mabomu ya machozi; wakamiminia wananchi maji makali yachomayo machoni; wakafyatua risasi baridi na moto; wakajeruhi kwa rungu na risasi; wakaua.

Hii ni intelijensia au viziavizia? Mkuu wa polisi wa mkoa wa Arusha (RPC) ana intelijensia yake. Hakuwa na tatizo lolote na maandamano na mkutano wa hadhara. Bali intelijensia ya IJP inazuia maandamano, tena kwa kutumia vyombo vya habari.

Kwa kuzingatia yaliyojiri Arusha, ambako CCM imefanya mambo ya balimbonaha, – visa vya maiti kwenye lango la kaburi akijua hawatamwona tena – katika uchaguzi wa mbunge na baadaye katika mchakato wa kupata meya; haihitaji busara ya nyongeza kugundua kuwa polisi walikuwa wanafanya kazi ya CCM.

Ni polisi haohao wa Arusha ambao walimgeuza Godbless Lema kuwa gunia la kufanyia mazoezi ya ngumi kipindi chote cha kugombea ubunge jimbo la Arusha mjini hata baada ya kuwa mbunge.

Alikamatwa, alipigwa, aliswekwa rumande; alikamatwa, alitukanwa, alipigwa, alilazwa hospitalini; alikamatwa, alipigwa, aliswekwa rumande…hadi anatangazwa mshindi, alikuwa shujaa aliyejaa majeraha.

Intelijensia ya polisi, ikiongozwa na CCM, ilikuwa ikiona kuwa Lema ni hatari ya kukabiliana nayo mapema; kama ilivyoona kuwa waandamanaji wapigwe mabomu ya machozi na wengine wauawe “kabla hawajawa hatari.”

Iko wapi hatari katika kudai haki; katika kutoa maoni; katika kutaka maelezo kutoka kwa watawala; hata katika kupinga kauli au vitendo vya chama kingine cha siasa kinachotumia ubabe wa dola?

Intelijensia ya aina ya Mwema ndiyo iliona  waandamanaji, wakiongozwa na Chama cha Wananchi (CUF) Pemba mwaka 2001, wapigwe kwa risasi za moto na zaidi ya 20 wauawe kabla hawajawa hatari.

Wananchi, wenye vitambaa vyeupe mikononi na matawi na majani mabichi kuashiria amani; wakiimba nyimbo za harakati za kisiasa na kijamii, wana hatari gani kwa Buguruni, Arusha, Pemba, Mwanza au Tanzania nzima?

Ni itelijensia hiyohiyo inayosababisha polisi waingilie popote pale – maandamano ya wafanyakazi, migomo ya wanafunzi vyuoni na mikutano ya vyama vya upinzani – ili kuzuia kutokea “hatari” au “uhalifu” au “madhara.” Vyote vya kufikirika tu.

Bali intelijensia ya polisi imekomea pale inapodhibiti haki ya wananchi ya kujieleza; haki isiyostahili kuombewa ruhusa isipokuwa kutolewa taarifa tu juu ya kuwepo kusanyiko, mikutano na maandamano.

Basi intelijensia ya polisi haina maana. Kama ingekuwa na maana ingeona kuwa hawapaswi kuua wananchi Pemba, kwa kuwa utakuja muwafaka wa kuwaweka wagombanao katika serikali moja.

Leo hii, waliopoteza ndugu na marafiki katika maandamano ya haki, wanaionaje polisi na hata serikali? Kwamba polisi ina intelijensia au inaongozwa na maslahi ya CCM ya wakati uliopo.

Kwa nini intelijensia ya polisi na hasa Mwema, isione kuwa hatua ya katibu wa CCM mkoa wa Arusha kujifanya diwani wa Arusha wakati yeye ni mbunge viti maalum kutoka Tanga, ni hatari inayoweza kuleta hata umwagaji damu, kama ilivyotokea?

Kwa nini intelijensia ya polisi isitumike kuzuia kupiga, kuumiza na hata kuua wananchi wanaoandamana kwa kuelewa kuwa wananchi wenyewe wakiamua kujikinga, vitakuwa vita vikubwa?

Hivi kwa nini intelijensia ya polisi isitumike  kuzuia jeshi la polisi kugawanyika kutokana na vitendo kama kile cha Arusha; kwani pamoja na kwamba askari walikuwa kazini, kuna walioona hakukuwa na sababu ya kupiga, kumwagia “pilipili” na hata kuua raia waliokuwa wakiandamana kwa utulivu.

Kwa nini intelijensia ya polisi isitumike kuondosha kile kinachoweza kuwa mgongano – kwa kila mkuu kuwa na intelijensia yake kama ilivyokuwa Arusha?

Kwa nini intelijensia isitumike kuondoa kile ambacho kinaweza kuonekana baadaye kuwa ni kunyanyasana na kutoaminiana kazini ndani ya jeshi hili? Inahitajika heshima na uvumilivu katika uongozi ili jeshi la Mwema libaki moja.

Lakini pia kwa nini intelijensia ya polisi isione kuwa inatumbukizwa katika ghiliba na siasa za CCM kwa maslahi binafsi? Uzoefu umeonyesha kuwa maslahi ya CCM, karibu mara zote sasa, siyo maslahi ya taifa.

Iko wapi intelijensia ya polisi isiyoweza kuona na kukamata watu “wanaochanganya makaratasi,” kuunda makampuni na kuiba mabilioni ya shilingi kutoka Benki Kuu na Hazina?

Mbona intelijensia ya polisi haikuona hatari ya makampuni ya Meremeta na Deep Green ya kufukarisha nchi pale yalipokuwa yakichota mabilioni ya shilingi kutoka benki kuu na hazina?

Intelijensia ya polisi haioni kampuni ya Kagoda ikijiandaa na ikikwapua zaidi ya Sh. 40 bilioni kutoka benki kuu.

Haioni fedha hizo zikipitishwa katika benki kubwa nchini; kutawanywa katika matawi yake matano jijini Dar es Salaam na hatimaye fedha zote kuyeyuka?

Intelijensia ya polisi imeshindwa hata kutaja jina la mmiliki wa Kagoda wakati ndani ya mabenki ambako fedha zilipitia kuna saini na hata picha za wahusika.

Tuseme intelijensia hiyo haijapewa ruhusa ya kufikiri, kutafiti, kufuatilia na kugundua? Msiba huo!

Intelijensia ya mwizi na intelijensia ya benki vimeshinda intelijensia ya polisi; ya Mwema?

Iko wapi intelijensia ya polisi itueleze mchezo wa makampuni ya kufua umeme ya Richmond na Dowans; izuie taifa kupoteza mabilioni ya shilingi kufidia kisichoeleweka wakati waliosababisha madai wakiwa nje ya jela.

Hivi intelijensia ya polisi ni ya mambo ya siasa tu hasa zinazoonyesha kuipinga CCM na siyo hatari kubwa inayokabili taifa?

Kwa kutumikia chama kilichoko ikulu – kwa kujua au bila kujua; kwa kuhisi limetumwa au kwa woga tu lisijeonekana limekitelekeza – jeshi la polisi linamomonyoa hadhi yake.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)