Inzi wavamia vita vya ufisadi


editor's picture

Na editor - Imechapwa 29 September 2009

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

KATIKA siku za karibuni vita dhidi ya ufisadi vimechukua mwelekeo mwingine. Vinapiganwa hata na watu ambao rekodi za usafi wao zinatia shaka.

Wapo wanasiasa ambao sasa wanasimama majukwaani wakihubiri mapambano dhidi ya ufisadi, wakati wanafahamika kuwa hata kuingia kwao madarakani kulijaa rafu.

Vita hivi sasa vimefanywa kama wimbo. Baadhi ya watu ambao hivi karibuni wamejitokeza na kutoa kauli za kuiunga mkono, wanaonekana kuwa na malengo maalum ya kupotosha mwelekeo wa mapambano yenyewe.

Kwa mtazamo wetu, kundi linalojiingiza katika vita litaongezeka zaidi, kwa kuwa sasa mapambano haya yanaonekana kuwa mtaji wa kisiasa zaidi, yaliyolenga uchaguzi mkuu wa mwakani.

Kwa namna mmoja vita hivi sasa vimeingiliwa na wasanii wanaoyatumia majukwaa ya siasa kutamka maneno dhidi ya ufisadi lakini kauli zao hazitokani na dhamira zao za dhati.

Tunachukua fursa hii kuwaasa Watanzania kuwa macho. Waangalie matapeli wanaovitumia vita hivi kwa maslahi yao binafsi; wengine wakijaribu kutaka kujitakasa kisiasa baada ya ama kuingia madarakani kwa njia chafu, au kutumia madaraka yao vibaya.

Tunasema Watanzania wawe macho na watu wa aina hii kwa kuwa wanaingia kwa kasi kubwa katika mkumbo wa kulaani ufisadi. Ni siku chache zijazo kundi la wanaojifanya wapambanaji litakuwa kubwa likiwa limebeba hadaa.

Kwa hiyo, kila mwananchi pale alipo, anao wajibu wa kuwachuja wahubiri wa vita hivi. Bila kufanya hivyo mapambano haya yatapoteza mwelekeo na kukosa hamasa.

Ikumbukwe kuwa "wapiganaji" hawa wapya wanajiunga na vita hivi wakiwa na malengo maalum. Siyo vibaya kwa wapiganaji kuongezeka, lakini tunaoona wanaingia mtumbwini, wana dhamira ya kutaka kumeza kundi la wapambanaji wa dhati na kufifisha kabisa nguvu zao.

Kila mwenye dhamira njema anao wajibu wa kukataa "inzi wa kisiasa" wanaolenga kuchafua vita vitakatifu dhidi ya ufisadi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: