Iran ‘yaitafuta’ Israel kwa mbali


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 22 February 2012

Printer-friendly version

IRAN imeendelea kuzikera nchi za magharibi baada ya juzi meli zake mbili za kivita kuranda katika bahari ya Mediterranean na kutia nanga bandari ya Tartous, Syria.

Televisheni ya taifa imeripoti kuwa meli hizo zililenga kuwapa mafunzo wanamaji wa Syria chini ya mpango uliotiwa saini na pande mbili hizo, mwaka mmoja uliopita.

Waziri wa Ulinzi, Ahmad Vahidi amekaririwa na shirika la Fars akisema: "Meli zetu zilipita kwenye mfereji wa Suez na ni haki ya Iran kupita katika maeneo ya kimataifa."

Habari nyingine zimesema kwamba meli za kivita za Iran ziliingia katika bahari ya Mediterranean baada ya kupita katika mfereji wa Suez Jumamosi iliyopita kwa lengo la kuonyesha “uwezo” wa Iran katika nchi za Mashariki ya Kati.

Hatua hiyo imekuja huku mvutano ukiongezeka kati ya Iran na Israel.

“Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limepita katika mfereji wa Suez kwa mara ya pili tangu mwaka mwaka 1979 yalipofanyika Mapinduzi ya Kiislamu,” alisema kamanda Habibollah Sayari.

Hakusema meli ngapi zilipita katika mfereji au lengo la mpango huo katika bahari ya Mediterranean ni nini.

Hatua hiyo ni tishio kwa majirani zake. Katika mlango wa Hormuz, boti za Iran zinaendelea kuzipa hofu kubwa meli kubwa za kubeba ndege za Marekani.

Wakati hayo yote yakifanyika, Waziri wa Ulinzi wa Israel, Ehud Barak Jumamosi alitoa wito Iran iwekewa “vikwazo vya kuiangamiza” kuilazimisha isalimu amri mpango wake wa nguvu za atomiki akisisitiza Iran ikifanikiwa kumiliki silaha za nyuklia itatibua utulivu Mashariki ya Kati.

“Iran yenye nguvu za nyuklia ni tishio kwa dunia siyo Israel tu … Nchi nyingine mashuhuri katika Mashariki ya Kati zitajaribu kumiliki pia silaha za nyuklia ; inaweza kuwa Saudi Arabia, au Uturuki au Misri,” Barak aliwaambia waandishi wa habari akiwa ziarani Tokyo.

“Ni lazima iongezeke kasi ya kuiwekea vikwazo na kuhakikisha inakwama na madhara makubwa ya hali hiyo ni uongozi kulazimika kukaa chini, wajiulize je, tunaweza kulipa gharama za kutengwa na sehemu kubwa ya dunia?”’ alisema.

Katika mahojiano mengine yaliyofanyika Jumamosi na kuchapishwa na The Daily Telegraph, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza William Hague alionya pia juu ya kampeni kubwa ya kumiliki silaha za nyuklia katika eneo la Mashariki ya Kati.

“Ikiwa watafanikiwa kuwa na nguvu za nyuklia, nafikiri hata nchi nyingine katika Mashariki ya Kati zitataka kutengeneza silaha za nyuklia,” alisema Hague.  

0
No votes yet