Iran ni vita ya Bunge, Ahmadinejad


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 02 November 2011

Printer-friendly version
Rais Mahmoud Ahmadinejad

BUNGE la Iran limeongeza shinikizo la kumwita na kumhoji Rais Mahmoud Ahmadinejad huku wabunge wengi wakijiandikisha kutaka rais huyo ashtakiwe.

Vyombo vya habari vimeripoti kwamba kusudio hilo lililodumu kwa miezi minne, lilitupwa hivi karibuni, lakini limepata nguvu mpya baada ya wabunge wengi zaidi kutia saini waraka wa kutaka Ahmadinejad afike bungeni.

“Mpango wa kumbana Ahmadinejad warudi wabunge wengi watia saini” kilisema kichwa cha habari cha gazeti la kila siku la Siasat-e Rouz. Magazeti mengine yalikuwa na habari hiyo yakionesha kutotulia kwa mgogoro wa ndani wa kisiasa katika taifa hili.

Bunge hilo linalodhibitiwa na wabunge wenye mrengo wa kihafidhina, awali walikusudia kuwasilisha samansi ya kumwita Juni baada ya wabunge 100 kati ya 290 kutia saini katikati ya shutuma dhidi ya sera za Rais Ahmadinejad, udhalimu na kutowaheshimu wabunge.

Lakini, baada ya Kiongozi wa Kidini wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei kutoa wito wa umoja kwa mihimili ya uongozi,  Bodi ya Bunge ilisita kuwasilisha samansi kufuatia wabunge wengi kujitoa.

Kutia chumvi kwenye kidonda, Bodi imeshupalia kuwa barua hiyo itapelekwa kwa rais.

Mbunge mmoja maarufu na mpinzani wa muda mrefu wa Ahmadinejad, Ali Motahari aliwasilisha barua ya kujiuzulu kwenye Bodi akipinga hatua ya Bunge kusita kumwita rais.

Hatua ya Motahari iliwatia ari washirika wenzake kwani bado kuna saini za wabunge 74, moja zaidi ya 73 ambazo gazeti la Sharq linasema zinahitajika kikatiba.

"Hatua ya bodi kusitisha kesi lilikuwa kinyume…na liliwaudhi sana wabunge,” alikaririwa Mbunge, Sharif Hosseini na shirika la habari la Fars.

Mara zote Bunge limekuwa na msimamo mkali dhidi ya Ahmadinejad lakini liliongeza presha Aprili mwaka huu alipotaka kumtimua waziri wa intelejensia ambaye ana wajibu wa kusimamia chaguzi. Hatua hiyo ilizuiwa na Khamenei.

Watu wenye msimamo mkali wanamshutumu Rais Ahmadinejad kuwa ni mtumwa wa ‘fikra potofu’ za baadhi ya washauri wake wanaotaka kudhoofisha mamlaka ya kiongozi wa kidini katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.

Wabunge hao wamewashutumu pia wasaidizi wake kwa kuhusika katika ubadhirifu wa dola 2.6bilioni suala ambalo liko chini ya uchunguzi.

Wabunge sita walitia saini wakitaka kuchunguzwa kwa maofisa watano maswahiba wa Ahmadinejad ambao wanahusika katika kesi hiyo. Wasaidizi hao wa rais ni pamoja na Esfandiar Rahim Mashaie na Gavana wa Benki Kuu, Mahmoud Bahmani, gazeti la Etemad limeripoti.

Wachambuzi wa mambo wanasema kwamba Khamenei atakuwa anafurahia kudhoofishwa kwa Ahmadinejad lakini hataki kujiweka katika hatari ya kuona mageuzi yakifanyika na kumtoa rais huyo ikulu wakati umebaki muda usiozidi miaka miwili.

Khamenei amependekeza kwamba katika miaka ijayo Iran inaweza kuondoa utaratibu wa kumchagua rais moja kwa moja, badala yake mkuu wa nchi achaguliwe na Bunge. Hata hivyo, wakosoaji wanasema utaratibu huo utadhoofisha demokrasia nchini humo.

Motahari alisema kwamba kumwita Ahmadinejad ili ahojiwe kusionekane kuwa ni kupuuza mfumo wa serikali ya Iran.

"Hatua hii itasababisha uwepo uelewano mkubwa kati ya serikali na bunge ... Mambo yote yatajadiliwa kwa maslahi ya mfumo," aliwaambia waandishi wa habari juzi Jumatatu.

Spika wa Bunge Ali Larijani amemwalika Ahmadinejad kuhudhuria kikao cha Bunge jana ili ashuhudie Waziri wa Uchumi, Shamseddin Hosseini anapohojiwa ikiwa ni sehemu ya kumshtaki yeye, hayo yakiwa mapambano mengine kati ya serikali na Bunge.

0
No votes yet