Iweje Zanzibar nchi ndani ya Muungano


Joseph Mihangwa's picture

Na Joseph Mihangwa - Imechapwa 22 July 2008

Printer-friendly version

WANASHERIA wakuu wa serikali ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanashughulikia tafsiri sahihi ya kisheria kuhusu utata ulioibuka nchini wa kama Zanzibar ni nchi. Hii inafuatia tamko la Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alilotoa bungeni wakati akijibu swali.

Itakuaje wanasheria wakishindwa kuafikiana? Suluhisho pekee litapatikana suala hili likipelekwa Mahakama Maalumu ya Katiba.

Kwa mujibu wa Ibara ya 126(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, mahakama hii inaundwa ili 'kusikiliza shauri lililotolewa mbele yake na kutoa uamuzi wa usuluhishi, juu ya suala lolote linalohusika na tafsiri ya Katiba iwapo tafsiri hiyo au utekelezaji wake unabishaniwa kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar'.

Katiba ya Zanzibar, Ibara ya pili inatamka: 'Zanzibar is a State.' Maana yake Zanzibar ni nchi. Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiingereza – Kiswahili, Toleo la Tatu, iliyoandikwa na kutolewa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (TUKI), neno 'state' limetafsiriwa ni 'dola'; 'Serikali'; 'jimbo'.

Ibara ya kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya 1977, inaitaja Tanzania kuwa ni 'Jamhuri ya Muungano'; kwa lugha ya Kiingereza, ni: 'Tanzania is a United Sovereign Republic.' Neno 'State' halipo hapo. Kwa mujibu wa Kamusi ya TUKI, neno 'Sovereign' lina maana 'kuu', 'enye enzi', na 'Sovereignty' ni 'mamlaka' au 'utawala', wakati neno 'Republic' linamaanisha 'Jamhuri'.

Kwa hivyo basi, Tanzania ni 'Mamlaka au utawala wa Jamhuri ya Muungano'. Je, Mamlaka au Jamhuri ni dola au Serikali kwa maana ya 'state'? Je, ni nchi? Ni ipi 'nchi, kati ya 'state' na 'sovereign Republic'? Nini kilichokusudiwa chini ya Muungano huu, na utata uko wapi?

Msingi mkuu wa muungano na wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano na ile ya Zanzibar ni 'Mkataba wa Muungano' uliotiwa saini na waasisi wake, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Jamhuri ya Tanganyika na Abeid Amani Karume, Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Hii inaitwa 'Hati ya Muungano au 'Articles of Union.'

Chini ya mkataba huo, nchi hizi zilikubaliana kuunda 'Jamhuri ya Muungano' kwa hiari kwa kuachia baadhi tu ya madaraka/mamlaka yake ili yaingie na kushughulikiwa na Muungano na kubakiza mengine yote. Yafuatayo ni mambo 11 yaliyoingizwa kwenye Muungano: Katiba ya Muungano; Mambo ya Nje; Ulinzi na Usalama; Polisi; Uraia na Uhamiaji.

Mengine ni Mikopo na Biashara ya Nje; Utumishi katika Serikali ya Muungano; Kodi ya Mapato na Ushuru wa Forodha; na Bandari na Usafiri wa Anga.

Kwa kuwa Muungano ulifikiwa kidharura au 'zima moto', ilikubaliwa kuwa Katiba ya Jamhuri ya Tanganyika irekebishwe kwa kuingiza masuala hayo 11 ya Muungano na kutumika pia kama Katiba ya muda ya Muungano hadi Muungano huo utakapopata Katiba yake katika mwaka mmoja.

Ibara hii inaonyesha: Jamhuri ya Tanganyika haikufa kufuatia Muungano huo, hoja inayopewa nguvu na Ibara 5 ya Mkataba huo isemayo: 'Sheria za Tanganyika zilizopo na zile za Zanzibar zitaendelea kuwa na nguvu katika nchi hizo' wakati wote wa uhai wa Muungano huu.

Mkataba huo unatambua kuwapo kwa Makamu wa Rais wawili wa Jamhuri ya Muungano, mmoja kutoka Zanzibar ambaye pia ndiye Rais wa Zanzibar, na mwingine kutoka Tanganyika. Kazi zao zimefafanuliwa kwa mujibu wa Katiba ya Tanganyika na ya Muungano kuwa ni 'mmoja atakuwa msaidizi Mkuu wa Rais kwa shughuli za Muungano Zanzibar na ndiye pia Rais wa Zanzibar na Mkuu wa Serikali ya Zanzibar; na mwingine atakuwa msaidizi mkuu wa Rais kwa shughuli za Muungano upande wa Tanganyika na ndiye pia kiongozi wa shughuli za Serikali Bungeni.'

Kama ilivyo mikataba yote ya kimataifa, Mkataba wa Muungano ulitakiwa kuridhiwa na Mabunge ya nchi hizo mbili ili uwe na nguvu za kisheria na kuweza kutumika. Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi Zanzibar yaliridhia Mkataba huo 25 Aprili1964 na kuupa Muungano huu jina la 'Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar' (kif .4) ambapo, pamoja na mambo mengine, Mabunge hayo yalimpa Rais uwezo wa kuifanyia marekebisho Katiba ya Tanganyika kwa njia ya AMRI za Rais (Decrees) ili iweze kukidhi mambo ya Muungano (kif. 5(2). Hapo ndipo utata wa Muungano ulipoanzia.

Marekebisho ya kwanza kwa njia ya AMRI ya Rais (The Transitional Provision Decree, 1964) yaliyochapishwa kama Taarifa ya Serikali (GN) Na 245 ya 1/5/1964, yaliwahamishia watumishi wote wa Jamhuri ya Tanganyika kwenye utumishi wa Jamhuri ya Muungano kana kwamba shughuli zote za Tanganyika zilikuwa za Muungano, na ikaagizwa 'sheria za ajira za Jamhuri ya Tanganyika zilizopo zitatumika pia katika utumishi wa Jamhuri ya Muungano', na Mahakama Kuu ya Tanganyika ikawa ndiyo Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano.

Amri hiyo ilielekeza pia kutumika kwa mhuri wa Serikali ya Jamhuri ya Tanganyika kama pia mhuri wa Jamhuri ya Muungano, hadi hapo Bunge la Muungano litakapopitisha mhuri wake. Amri ilielekeza kuwa 'mali zote na haki kwa mali za Jamhuri ya Tanganyika za aina yote, na mali zote na haki kwa mali za Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zinazomilikiwa au kutumika kuhusiana na mambo ya Muungano zitamilikiwa na Jamhuri ya Muungano'.

Tatizo hapa ni kuwa wakati Tanganyika ilikabidhi kila kitu kilichokuwa chake kwenye Serikali ya Muungano, Zanzibar ilichangia zile tu zinazohusiana na taasisi za muungano na kuruhusiwa kumiliki mali zote nyingine. Ni bahati iliyoje kwa Zanzibar kurithi utajiri wote wa Tanganyika ndani ya Muungano, wakati ikiendelea kumiliki mali zake zote bila ya kuingiliwa?

Amri ya pili ya Rais iliyochapishwa kama Taarifa ya Serikali Nam. 246 ya 1/5/1964 ilifanya marekebisho yenye utata zaidi unaoendelea hadi leo. Chini ya kifungu 4(2) ilielekezwa, 'Mamlaka kuhusiana na mambo yote ya Muungano ndani na kwa ajili ya Jamhuri ya Muungano, na kwa mambo mengine yote ndani na kwa ajili ya Tanganyika, yatakuwa chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano'.

Ndiyo kusema utawala kuhusiana na mambo ya Muungano, na mamlaka kuhusiana na mambo yote ndani na kwa ajili ya Jamhuri ya Tanganyika, yameunganishwa na kuwa chini ya rais wa Jamhuri ya Muungano, na hapo hadhi ya Tanganyika ikafutika kinyemela.

Na kwa kuwa sasa kila kitu cha Jamhuri ya Tanganyika kilikuwa mali ya Muungano, ndiyo kusema Tanganyika ndiyo iliyogeuka kuwa Muungano, na Muungano kuwa ndiyo Tanganyika; Bunge la Jamhuri ya Tanganyika likawa Bunge la Muungano, Rais wa Jamhuri ya Muungano akawa Rais pia wa Tanganyika, na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Tanganyika akawa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano asiye na nchi, wakati Zanzibar iliruhusiwa kuendesha mambo yake kama nchi huru, isipokuwa kwa mambo ya Muungano tu.

Na kupitia Amri nyingine (the Transitional Provision No 2 Decree, 1964) ya 1/5/1964, iliagizwa jina 'Tanganyika' lisomeke na kumaanisha 'Jamhuri ya Muungano', katika vitabu vyote vya sheria', na neno 'Serikali ya Tanganyika na mambo yote yanayohusiana na Jamhuri ya Tanganyika' nayo yasomeke kumaanisha 'Serikali ya Jamhuri ya Muungano'.

Hapa ndipo dhana ya serikali mbili ndani ya Muungano ilipoanza kujitokeza. Kwamba Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar, badala ya mtazamo wa awali wa kuwapo Tanganyika, Zanzibar na Serikali ya Muungano.

Pamoja na Zanzibar kuanza kuhofu kumezwa na Tanganyika, kimisingi nchi hiyo ilionekana kama mgeni ndani ya Muungano aliyealikwa kuja kufaidi na kufurahia 'vinono' vya mwenyeji wake Tanganyika bila ya kuvitolea jasho.

Pengine ni hofu hii iliyomfanya Karume atofautiane na Nyerere juu ya muundo sahihi wa Muungano na hiyo ikaua uteuzi wa Tume ya kuandika Katiba ya Muungano. Pia Bunge la kupitisha Katiba hiyo halikuitishwa Aprili 1965 kama ulivyoelekeza mkataba hadi mwaka 1977.

Juhudi za kufifisha au kufuta kabisa nafasi ya Tanganyika kwa maamuzi ya mtu mmoja kupitia Amri za Rais (Decrees), zilifanikiwa kwa kiasi fulani, lakini 'Mkataba wa Muungano' na Sheria ya Muungano kama zilivyo, zilikuwa na zinaendelea kugoma kwa muundo wa sasa.

Hata Katiba Mpya (Act No. 43) ya 1965 iliyotungwa kwa mujibu ya matakwa ya serikali ya kuanzisha serikali ya kidemokrasia ya chama kimoja, iliendelea kutambua muundo wa Serikali Tatu na kuwapo Tanganyika.

Ushahidi ni Ibara ya 20, iliyosema 'Rais atateua Mkuu wa Mkoa kwa kila Mkoa ndani ya 'Tanganyika' na Ibara ya 25 iliyosema 'Tanganyika itagawanywa katika majimbo mengi ya uchaguzi kwa kuzingatia idadi ya watu kwa kila jimbo?.'

Na kuhusu utumishi wa Mahakama, Katiba ilisema, 'Kutakuwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama ndani na kwa ajili ya Jamhuri ya Muungano ndani ya Tanganyika?.' Ndiyo kusema muundo wa Shirikisho ulitambuliwa kisheria tangu 1964 hadi ulipofutwa kinyemela na Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya 1977, lakini Mkataba na Sheria ya Muungano zinagoma.

Tatizo hili si la kisiasa kama wengi tunavyodhani, bali ni la kikatiba na hivyo lazima litatuliwe kikatiba kwa kuangalia chimbuko, madhumuni na muundo wa Muungano uliokusudiwa. Je, ulilenga kuunda Serikali moja, mbili au tatu?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: