Jaji Makame ametuletea nini kutoka Kenya, Zimbabwe?


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 06 May 2008

Printer-friendly version
Asiendekeze utii wa tume za uchaguzi kwa watawala
Ayachukue yaliyo mazuri katika katiba ya Mugabe katili
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya  Uchaguzi (NEC), Jaji Lewis Makame

NILIMUONA Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Lewis Makame, akichekacheka na kutabasamu, huku amefunga mikono, mbele ya Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, wiki moja baada ya uchaguzi wa nchi hiyo mwezi uliopita.

Jaji Makame alikuwa katika jopo la 'wageni' wa Rais Mugabe siku hiyo, miongoni mwa waangalizi wa uchaguzi huo.

Katika kipindi hicho hicho, tayari taarifa zilikuwa zinasema kwamba Rais Mugabe ameshindwa na mpinzani wake mkuu, Morgan Tsvangirai, aliyegombea urais kwa tiketi ya Movement for Democratic Change (MDC).

Sasa imeshakuwa dhahiri kwamba Rais Mugabe alishindwa, licha ya jitihada za awali za chama chake na tume ya uchaguzi ya Zimbabwe kufanya juhudi za kuficha ukweli.

Shinikizo la wananchi na mataifa makubwa limeifikisha tume hiyo kukubali ukweli kwamba ikitangaza matokeo yanayompa ushindi Rais Mugabe, kungetokea fujo zisizomithilika nchini humo.

Kwa nini nimeanza kwa kumtaja Jaji Makame? Nataka kujua alikwenda kufanya nini Zimbabwe? Je, amejifunza nini ambacho atakileta Tanzania?

Wasiwasi wangu unatokana na ukweli kwamba Tanzania imekuwa na urafiki wa kinafiki kwa muda mrefu na Mugabe. Sababu zipo nyingi, mbali na zile za kihistoria zinazotokana na mchango wa Tanzania kwa Mugabe na wapigania uhuru wengine wa nchi hiyo.

Urafiki huo, ambao kimsingi ulijengeka wakati wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, umekuwa ukitumiwa vibaya na viongozi wetu walioshika madaraka katika miaka ya karibuni wakati Mugabe amepoteza mvuto kwa wananchi wake, na ameongoza mikakati mahususi ya kuwatesa wanaompinga ili abaki madarakani.

Marais Benjamin Mkapa na Jakata Kikwete wameshirikiana na viongozi wengine wa Afrika wa enzi zao kumtukuza Mugabe na kushangilia udikteta wake, katika mazingira ambayo Mwalimu Nyerere asingeyavumilia.

Kwa kushindwa kumshauri vema na hata kumkemea Mugabe, marais wetu wamesaliti dhamira asilia ya uongozi wa Tanzania katika ukombozi wa Waafrika kutoka kwenye utumwa, unyonge na unyanyaswaji.

Kilele cha shangilio la viongozi wetu kwa Mugabe ni pale alipokuja Dar es Salaam, mwaka juzi, wakati wa mkutano wa viongozi wa nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC).

Rais Kikwete alimtukuza Mugabe vya kutosha. Inadaiwa alimpatia malazi Ikulu kwa muda wote aliokuwa nchini, huku marais wengine wakitafutiwa malazi hotelini.

Hii tabia ya viongozi wetu kuwatukuza "majambazi" kiasi hiki ndiyo inawafanya wananchi wa Tanzania wahoji uadilifu wa viongozi wetu.

Zaidi ya hayo, uchaguzi huu wa juzi ambao Jaji Makame alikwenda Zimbabwe kuangalia, umekuwa tata kiasi cha kuwafanya viongozi wote wa Afrika ? isipokuwa Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga ? kuonekana walezi wa ubabe na udikteta wa Mugabe.

Viongozi wote wa Afrika, hata majirani wa Mugabe ambao wanaguswa moja kwa moja na matokeo ya mgogoro wa kisiasa na kiuchumi wa Zimbabwe, wameshindwa kutoa kauli ya kumuonya Mugabe asidhulumu haki ya wananchi waliomkataa.

Mataifa makubwa ya Ulaya na Marekani yamekuwa yakitoa matamko makali dhidi ya vitendo vya Mugabe na ZEC (Zimbabwe Electoral Commission) vya kuficha matokeo ya kura kwa zaidi ya mwezi mzima, huku serikali ikiwatisha na kuwadhulumu wananchi ili kuleta hofu katika uchaguzi wa marudio.

Mbali na matamko hayo, mataifa hayo yamekuwa yakishawishi viongozi wa Afrika kuweka msimamo mkali dhidi ya Rais Mugabe.

Rais Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) amekuwa katika shinikizo kubwa la mataifa makubwa tangu alipokuwa Marekani kwenye kikao cha Umoja wa Mataifa.

Ajabu ni kwamba Kikwete hadi leo hajatoa tamko dhidi ya dhuluma ya Mugabe na ZEC kwa watu wao. Viongozi wengine wa SADC wameishia kufanya kikao na hatimaye kumuomba Rais Thabo Mbeki "andelee kusuluhisha mgogoro wa Zimbabwe" katika mazingira ambayo hayahitaji usuluhishi zaidi ya ZEC kumtangaza mshindi wa kweli.

Ni Odinga tu aliyetamka kwa ujasiri mkubwa kwamba "zama za udikteta Afrika zilishapita" na kwamba kama Mugabe hataki kuondoka, viongozi wa Afrika wasiogope "kutumia hata nguvu za kijeshi kukomesha udikteta" wake!

Laiti Odinga angekuwa ndiye Mwenyekiti wa AU, mambo nchini Zimbabawe yangekuwa tofauti na yaliyo sasa.

Rais Kikwete ambaye majuzi tu aliamuru majeshi yetu kwenda Comoro kumuondoa rais aliyechaguliwa madarakani, anashindwa kutumia madarakaka yake leo kuwashawishi viongozi wenzake kutumia nguvu hiyo hiyo dhidi ya Mugabe.

Ina maana anafurahia hayo yanayofanyika Zimbabwe? AU anamwogopa Rais Mugabe kiasi kwamba hawezi kuwaongoza viongozi wenzake kumgusa?

Mchezo mchafu unaofanywa sasa na ZEC ndio ulifanywa na Tume ya Uchaguzi ya Kenya (ECK) mwishoni mwa mwaka jana.

Tofauti pekee iliyopo ni kwamba ZEC imechelewesha matokeo ili kuipa serikali ya Mugabe nafasi ya kujiandaa upya, kutisha wapiga kura na kujiandalia uchaguzi wa marudio.

Ile ya Kenya ilikimbilia kutangaza kwamba rais aliye madarakani ndiye mshindi, katika mazingira ambayo kila mmoja alijua rais hakushinda.

Kama ilivyo kwa mwenyekiti wa ZEC Jaji George Chiwese na mwenyekiti wa ECK Samuel Kivuitu, mwenyekiti wa NEC Jaji Makame ni mtu muhimu katika mustakabhali wa nchi yetu unapofika wakati wa uchaguzi.

Ndiye mtu ambaye anaamua kufanya ya Kivuitu au ya Chiwese na kumtangaza yeyote amtakaye kwa hesabu itakayokuwa mbele yake au itakayotoka kinywani mwake.

Kibaya zaidi, na tofauti na Zimbabwe na Kenya, katiba yetu hairuhusu huyo aliyetangazwa mshindi kupingwa popote, hata mahakamani.

Kwa mantiki hiyo, Jaji Makame au mwenyekiti yeyote wa NEC ana uwezo wa kuumba rais. Na kwa tume zetu hizi zinazoongozwa na majaji wenye mapenzi na vyama tawala, ni idhahiri kwamba mshindi wa uchaguzi anakuwa kichwani mwa mwenyekiti wa tume hata kabla ya uchaguzi kufanyika.

Kutokana na sababu za kihistoria, wengi (kama si wote) wa wenyeviti wa wa tume za uchaguzi katika nchi za Afrika ni wanachama wa vyama vinavyotawala.

Jaji Makame hajawahi kuwaambia Watanzania kwamba amejivua uanachama wa CCM. Hivyo, hata anapokuwa kwenye kiti chake hicho, moyo wake uko kwenye chama chake.

Uanachama huu, na hasa kwa kuwa yeye ndio mteule wa rais, ni jambo linalomfanya mwenyekiti wa tume kuwa na "utii" usio wa lazima, ambao unakuwa sehemu ya maisha yake hata anapokuwa mbele ya viongozi wa aina ya Mugabe.

'Mkao' wa Jaji Makame mbele ya Mugabe ? ambaye wakati huo alikuwa tayari ameshindwa ? ulikuwa utii usiomithilika, tena kwa kiongozi asiye na madaraka yoyote kwake.

Jambo lililo wazi ni kwamba utii huu ni tabia njema, wala si jambo la kubezwa. Hata hivyo, viongozi wetu wanautumia vibaya utii wa wateule wao, hasa wateule hao wanaposhindwa kuwa washauri wazuri wa kitaaluma kwa waliowateua.

Watanzania wangetarajia kwamba Jaji Makame amejifunza kutoka Kenya. Maana yake ni kwamba hata siku moja asiiruhusu tume yake kufanya yaliyofanywa na Kivuitu.

Haya hayajatokea kwetu, lakini haieleweki kwamba mtu wa utii wa aina ya Jaji Makame akiagizwa na rais kwamba "hebu tangaza kwamba nimeshinda" atakataa na kumtangaza mshindi halisi!

Tunatarajia kwamba Jaji Makame amejifunza kutoka Zimbabwe jambo moja la ziada. Kwamba katiba yetu ina kasoro, hasa katika suala la kuruhusu mshindi apite kwa asilimia ndogo ya kura (chini ya asilimia 50) ilimradi ndiye anaongoza; na hili la kuzuia kipingamizi dhidi ya mshindi wa urais anayelalamikiwa.

Si dhambi kwa Jaji Makame kuishauri serikali kwamba hakwenda Zimbabwe kutalii, bali kuchota mafunzo; na kwamba licha ya ubabe na ukatili wa Mugabe, katiba yao katika hili ni nzuri kuliko yetu, na ni vema kama viongozi wetu wanajiamini na wanajiheshimu wachukue mafunzo hao.

Katiba irekebishwe, mshindi wa urais apate kura zinazozidi asilimia 50. Asipofikia hapo, uchaguzi urudiwe. Na akishatangazwa, kama kuna watu wana duku duku na ushindi wake, wasizuiwe kwenda mahakamani.

Hapo ndipo tutajivuna kwamba tunafuata, walau kwa viwango fulani, utawala wa kisheria. Hapo ndipo wajumbe wanaotokla nchini kwenda kuangalia chaguzi za nchi nyingine watatuambia kwamb hawatumbui pesa zetu kwa kuzurura na kustarehe tu, bali ziara zao zina manufaa kwa taifa.

Hapo ndipo tutakuwa tumefanya jambo moja la maana, ambalo limewashinda viongozi wetu wa kuchaguliwa. Tumeshindwa kumkemea Mugabe kwa sababu tunajua kwamba anayofanya kwao ndiyo tunayofanya hapa kwetu, isipokuwa kwa viwango tofauti.

Lakini hili la kuchota mafunzo kutoka Kenya na Zimbabwe halihitaji kauli ya wanasiasa. Wajumbe tunaowatuma huko, akina Jaji Makame wanaweza kulipenyeza kwa wahusika likasukumwa hadi mahali pake. Huu utakuwa ni utii mwema si kwa watawala bali kwa wananchi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: