Jaji Warioba asitetee mafisadi


Joseph Mihangwa's picture

Na Joseph Mihangwa - Imechapwa 14 April 2009

Printer-friendly version
Jaji Joseph Sinde Warioba

FIKIRIA hili. Wewe ni mwenye nyumba. Siku moja, wakati umelala fofofo, majambazi yanaingia ndani na kusomba kila kitu. Baada ya muda mfupi, unaamshwa na minyukano ya majambazi hayo, yakitwangana baada ya kuhitilafiana juu ya mgawo wa kile yalichopora.

Je, utaacha kupiga kelele ili majirani wakusikie?  Utakuwa mtu wa ajabu usipofanya hivyo.

Sababu ya kwanza ya kuita majirani, ni kutaka wajue yaliyokusibu na wakusaidie kurejesha ulichoporwa.  Pili ni kutaka kuona wale waliofanya kitendo hicho wanaadhibiwa kwa taratibu za jamii yako kwa kitendo hicho. 

Tatu, ni kutaka kuipa jamii yako mwamko dhidi ya matukio kama hilo, ili iweze kuchukua hatua thabiti kuondokana na hofu ya kama yale yaliyokupata.

Leo, kama kuna neno wakilishi linaloweza kuelezea hali ya mambo yanavyokwenda hapa  nchini, basi neno hilo ni “Mtafaruku” unaozaa hali tete kisiasa, kiuchumi na kijamii. Kwa nini?

Bungeni hali si shwari. Mwanzoni uwakilishi uligawanyika kwa misingi ya hoja za “wapinzani” na hoja za chama tawala, kama kwamba vyama vya siasa viko juu ya Katiba ya nchi. 

Lakini hata hivyo, wabunge wameanza kupata mwanga kwamba kuna Bunge moja tu la wabunge wote katika kuitetea Katiba ya nchi, bila kujali tofauti za kiitikadi.

Kwa sababu hiyo, mtafaruku unaoanza kuzaliwa sasa ni kati ya wabunge wenye kutetea wananchi na maslahi ya taifa kwa upande mmoja, na wabunge mamluki wenye kutetea ubinafsi na ufisadi. 

Hawa wanajifanya kukipenda chama madarakani kuliko taifa. Wanapenda Tanzania kutokana na kile wanachovuna, lakini hawawapendi Watanzania.

Baya kuliko yote ni hili la siasa kuhodhiwa na kikundi kidogo cha “wateule;” matajiri na watendaji wakuu serikalini;  kiasi kwamba hivi sasa utajiri unanunua siasa, na siasa inakamata (inapora) utajiri wa nchi.

Kutokana na nguvu ya kikundi hiki kukamata maamuzi ya serikali na chama tawala, kinaweza kupora rasilimali za taifa bila hofu ya kuwajibishwa, kikiwa kimehakikishiwa, “Msiogope, enyi kundi dogo, kwa kuwa baba yenu (yaani serikali, mfumo wa utawala) ameona vema kuwapa ule ufalme.”

Kundi hili dogo ni chanzo cha kuwagawa watu katika matabaka mawili: kikundi kidogo  ambacho kwa sababu ya kupora na kujimilikisha njia kuu za uchumi na siasa,  kinapata mali, nguvu na heshima isiyostahili.

Kundi la pili ni kubwa sana; ni la watu ambao haki na jasho lao ndilo linawapatia hao wachache mali yao na hali bora ya maisha kwa njia ya uporaji. 

Ule usemi kwamba “aliye nacho atazidishiwa, na asiye nacho atapokonywa hata kile kidogo alicho nacho,” sasa ndio unaofanya kazi.

Umma wa Kitanzania unaporwa vibaya na kundi hili dogo ambalo limehakikisha limezishika taasisi zote nyeti za taifa – Bunge, Serikali Kuu na limefanikiwa pia kupenyeza watu wake kwenye mhimili wa Mahakama.

Lengo la uporaji ni kugawana (kama tabaka) kile wanachopora; lakini ikitokea mmoja wao amejinyakulia kitita kikubwa zaidi ya wenzake, kwa uchu na ujanja, ugomvi unaweza kutokea, wakaanza kunyukana na hata kuuana wao kwa wao.

Ndivyo ilivyokuwa pia enzi za uvamizi wa Afrika karne ya 19(The Scramble for Afrika). Wazungu walipoona wangeweza kuuana kwa kugombea maeneo, walikaa mjini Berlin, 1884 – 1885, kuwekeana mipaka kwa vigezo vya maeneo ya ushawishi (Sphere of influence); mipaka ambayo imedumu hata baada ya uhuru.

Malumbano ya sasa ya wanasiasa nchini, hususani kuhusu uwekezaji na wawekezaji, kuanzia na ubinafsishaji usiojali miradi tata kama ile ya IPTL, Richmond/Dowans, TICTS; kashfa za ununuzi wa Rada, Ndege ya Rais na EPA, na mengine ambayo yanaonekana kuligawa Bunge, Serikali na Chama Tawala (CCM), yametokana na minyukano mizito ya washiriki wa uporaji huo.

Hawa wanagombea walichopora, wanachopora na watakachoendelea kupora, wakiamini kwamba, umma wa Kitanzania utazidi kulala, wakati ni kinyume chake.

Vyombo vya habari kama jicho, sikio, pua na mdomo wa jamii haviwezi kunyamazia minyukano ya majambazi haya; wawe vigogo wa chama, serikali, wabunge au wafanyabiashara mashuhuri. Jambazi ni jambazi tu, lazima lizomewe kama si kupewa kipigo.  Kwa nini? Shaaban Robert anatuambia:

“Kosa la mtu mdogo,
kutangazwa si muhimu,
Hasara yake kidogo,
kama la mwenda wazimu,
Kosa la mtu mkubwa (fisadi),
wajibu kutangaza,
Kwa herufi kubwa kubwa,
na wino wa kuangaza,
Dunia huharibiwa,
kwa makosa ya wakubwa,
Lakini husetiriwa,
kwa bidii yakazibwa,
Ni kinyume cha dunia,
wadogo kuadhirika,
Wakubwa wenye hatia,
wakazidi kutukuka.

Ni kwa sababu hii tunashindwa kuafikiana na Jaji Joseph Sinde Warioba kwa kauli yake ya hivi karibuni, ya kuvionya vyombo vya habari “kuepuka malumbano ya wanasiasa,” eti kwa kuwa hayawanufaishi wananchi. 

Warioba amenukuliwa akisema, “Inashangaza kuona viongozi wanaendeleza malumbano yasiyo na mwisho wakati wananchi wanakabiliwa na matatizo lukuki, na waandishi kuyakuza zaidi.”

Alisisitiza, “Kila gazeti ukisoma kila siku lina habari za wanasiasa, wakati huko vijijini wananchi wanalia; huu si uungwana… mnawanyima haki Watanzania wengi kupata nafasi ya kuzungumza katika vyombo vyenu.”
 
Namheshimu sana Jaji Warioba, lakini anaposema kwamba vyombo vya habari viache kupiga kelele au kuutangazia umma juu ya minyukano ya mafisadi, naanza kuamini kwamba huyu si Warioba tena tuliyemfahamu na kumheshimu.

Je, tuamini kwamba sasa naye yumo mbioni kutupa silaha na kuungana na kina Mzee Ngombale-Mwiru kuutelekeza umma wa Kitanzania kwa mafisadi, chini ya chama kisichomsemea mnyonge tena?

Vyombo vya habari haviwezi kutelekeza jukumu lake la kuona (macho), kusikia (sikio) na kutafsiri kwa usahihi yanayotokea katika jamii;  kunusa (pua) na kufuatilia uozo wote na kisha kuisemea (mdomo) jamii.

Na kwa sababu hii, tunaungana na Profesa Kulikoyela Kahigi, kuwatia nguvu wanahabari bila hofu ya kumwagiwa tindikali,

“Imbeni waimbaji na wanakijiji,
Imbeni juu ya haya, na mengineyo,
Lakini msisahau, kuimba juu ya hofu,
Na mikanganyiko, iwatatao watu mioyoni, Juu ya domo la wanasiasa,
na uhalali wa hali halisi
Imbeni, imbeni waimbaji,
Macho ya watu yazidi kufunuka,
Wajitome uwanjani watende.

Penye ukweli, uongo hujitenga. Hadi lini wananchi wataendelea kupumbazwa kana kwamba wamo usingizini, wasiweze kujitoma kwenye uwanja wa ukweli, wakatenda?

Wataendelea kuvumilia mpaka lini minyukano ya mafisadi hawa, wanaojifanya kukipenda chama, lakini hawalipendi taifa; wanaoipenda Tanzania, lakini hawawapendi Watanzania, ndipo (wananchi) waone kweli na haki vikitawala?

Hatuna shaka, kama asemavyo Shaaban Robert,

“Kweli  itashinda,
namna tunavyoishi,
Kweli haihofu tisho,
wala nguvu ya majeshi,
La uongo lina mwisho,
kweli kitu cha aushi,
Kweli itashinda kesho,
kama leo haitoshi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: