Jaji Warioba hahusiki


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 08 February 2012

Printer-friendly version

JAJI Joseph Sinde Warioba, waziri mkuu mstaafu wa Jamhuri ya Muungano, amekana kudaiwa na serikali.

Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili kwa njia ya simu wiki iliyopita, Jaji Warioba alisema, hakuna mahali popote ambako nyaraka za serikali zinaonyesha alihusika kwenye udhamini wa mtu anayeitwa Charles J. Warioba, kwenye Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB).

“Kwanza, huyo anayeitwa Charles J. Warioba simfahamu. Kwa hiyo, kuhusisha jina lake na mimi, hakuna mantiki yeyote,” ameeleza Jaji Warioba.

Amesema, “Lakini pili, sijawahi kumdhamini mtu mwenye jina hilo na hivyo si jambo zuri kunihusisha na mtu ambaye hata kumfahamu simfahamu.”

Kauli ya Jaji Warioba ilikuja siku moja baada ya gazeti hili kuripoti orodha ya wanaodaiwa kuwa watoto wa vigogo au wanaoonekana kuwa na mahusiano nao ambao wanadaiwa mamilioni ya fedha.

Katika kukokotoa huko, ndipo jina la Charles J. Warioba lilikutwa na kuandikwa kuwa “linaweza kuwa lina uhusiano na Jaji Joseph Warioba.”

Kutajwa kwa jina la Warioba kulifuatia hatua ya bodi ya mikopo kutangaza kwenye tovuti yake www.heslb.go.tz  majina ya wanaoitwa, “wadaiwa sugu wa HESLB” ili kushinikiza waliokopeshwa kurejesha fedha wanazodaiwa.

Miongoni mwa waliotajwa kuwa ni wadaiwa sugu wa bodi hiyo, ni Rais Jakaya Kikwete ambaye tovuti in inaonyesha majina ya watoto wake wawili, Ridhiwan J. Kikwete na Salama J. Kikwete.

Wakati Ridhiwan alidhaminiwa kwa masomo ya shahada ya kwanza ya sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Salama alidhaminiwa kwa masomo aliyohitimu katika Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba Muhimbili (MUHACS).

Bodi imetoa siku 21 kwa wanaodaiwa wote kujisalimisha, vinginevyo watachukuliwa hatua za kisheria. Inakadiriwa watu zaidi ya 80,000 wanadaiwa na bodi hiyo.

Akiongea kwa sauti ya upole, Jaji Warioba alisema, “…nakuomba sana uchukue hatua ya kueleza hili kwa umma, ili wananchi wasije wakaaminishwa kwamba nami ni miongoni mwa wadaiwa wa serikali katika suala hili.”

Alisema, “Gazeti lako linaheshimika sana. Kuacha taarifa hii kuendelea kusambaa kutaniletea matatizo makubwa. Tafadhali sana jaribu kuweka sawa jambo hili.”

Alipoulizwa iwapo katika familia yake kuna mtu mwenye jina hilo, Jaji Warioba alisema, “Sina mtu kama huyo.”

(Tunasikitika kwa usumbufu ambao msomaji wetu, Jaji Warioba ameupata na tayari tumemwomba radhi – Mhariri)

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: