Jaji Warioba kutendewa kama Jaji Kisanga?


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 27 June 2012

Printer-friendly version
Gumzo
Matumizi ya Tume Sh. 40 bilioni yaweza kuteketea bure

BENJAMIN Mkapa, rais mstaafu, aliwahi “kumzodoa” Jaji Robert Kisanga kwa kumwambia “…hili hatujakutuma.”

Ni wakati ule Mkapa alipomteua jaji kuwa mwenyekiti wa tume ya kuratibu maoni ya wananchi – White Paper – juu ya maeneo mbalimbali ya kisiasa na kiuchumi.

Ambacho Mkapa alisema hakumtuma Jaji Kisanga kilikuwa ukusanyaji maoni ya wananchi kuhusu muundo wa serikali wanaotaka.

Tume ya Jaji Kisanga ilipendekeza kuwapo kwa muundo wa serikali tatu – Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Haya hayakuwa maoni ya jaji. Yalikuwa maoni ya wananchi na tume isingeyaacha bila kuyafikisha kwa muunda tume.

Mkapa alitupilia mbali maoni hayo. Akakumbusha hata hadidu za rejea alizoipa tume na kusema hakuna hata moja iliyotaka wananchi waulizwe juu ya muundo wa serikali wanayoitaka.

Leo hii, miaka 10 baada ya Mkapa kumzodoa Kisanga, amekuja Jaji Joseph Sinde Warioba. Huyu ni mwenyekiti wa kamati ya kukusanya maoni juu ya uundwaji wa katiba “mpya.”

Warioba, ambaye aliwahi kuwa waziri mkuu wa Jamhuri, anasema tume yake itakusanya maoni yote, ikiwa ni pamoja na yale yanayohusu muundo wa serikali ya muungano na hata yale ya wanaotaka Muungano uvunjwe.

Sasa, kwa kuzingatia yaliyomsibu Jaji Kisanga, swali ni hili: Je, Warioba ameamua kuasi aliyemteua au ameamua kuvunja sheria ya kukusanya maoni?

Je, Warioba ameamua kutupilia mbali hadidu za rejea na kauli ya rais juu ya maoni yanayotaka “kuvunjwa kwa Muungano?”

Je, Warioba atakuwa, ama ameamua kuungana na Kikwete kuwafanyia usanii wananchi juu ya ujio wa “katiba mpya?”

Baadhi yetu tunaamini kuwa tangu mwanzo Kikwete hakutaka katiba mpya. Hadi sasa hajataka katiba mpya. Anachotaka ni kubakiza katiba iliyopo na kuiita “Katiba Mpya.” Ushahidi juu ya hili ni mkubwa mno.

Kwa mfano, wasaidizi wake katika suala hili, yaani Mwanasheria Mkuu wa serikali na Waziri mwenye dhamana, walikwishatoa maoni yao (na pengine ya serikali), wakipinga haja ya kuwa na katiba mpya.

Haiwezekani kuwa walikurupuka kutoa matamshi yanayogusa suala nyeti kama hili. Walikuwa na ruhusa au walisoma dalili za mkuu wao wa kazi na ndipo wakasema walichosema.

Warioba anajua fika kuwa rais wake hakumtuma kukusanya maoni juu ya muundo wa Muungano kuvunjwa au kuwapo – serikali mbili, moja au tatu.

Anajua vema kuwa kamati yake haikupewa kazi ya kuhoji wananchi juu muundo wa sasa wa serikali; muundo wa Muungano wala nafasi ya makamu wa rais.

Hivyo hiki anachosema Warioba, kuwa “Tume yetu itakusanya kila maoni, yakiwamo yanayotaka Muungano uvunjike,” hakieleweki.

Akiapisha wajumbe wa tume yake, 13 Aprili 2012, Kikwete alisema wananchi hawataulizwa iwapo wanautaka Muungano au hawautaki. Bali wataulizwa, jinsi ya kuboresha Muungano uliopo.

Rais Kikwete amesema, "Ni lazima ieleweke, huu sio mchakato wa kujadili kuwepo kwa Muungano au kutokuwepo kwa Muungano. Huu ni mchakato wa kupata maoni ya katiba mpya ya nchi ambayo itajali mustakabali wa nchi na watu wake."

Amerudia kauli hii mara kadhaa katika mikutano na baadhi ya makundi yaliyokwenda ikulu kuonana naye, wakati anasaini muswada huo ili iwe sheria rasmi; na hata katika hotuba yake kwa wana CCM wenzake.

Kuna "Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011, Na. 8 ya mwaka 2012. Hii ndiyo inaweka kibano kwa wananchi. Inasema Muungano ni moja ya mambo yasiyohojiwa.

Kwa hiyo basi, tume ya Warioba inapaswa  kukusanya maoni ya jinsi ya kuboresha Muungano; siyo maoni ya mfumo gani wa Muungano unaohitajika au ulio bora. Hii ndiyo amri aliyopewa. Imekaziwa kwa sheria; kauli ya rais na hadidu za rejea.

Hapa hata Warioba amepewa kibano. Ili kupata maoni ya watu, siyo lazima uwe umeuliza swali. Hata kabla ya kuuliza swali, yeyote aweza kujitokeza na kutoa maoni juu ya lolote, hata lile ambalo halimo katika hadidu za rejea.

Maoni ya aina hiyo yakitolewa, mjumbe wa tume hawezi kuacha kuyanukuu. Akiyanukuu, Warioba hawezi kuacha kuyajumuisha na kuyawasilisha kwa rais.

Akiyawasilisha, aweza kuambiwa kuwa “…haya sijakutuma.” Je, maoni hayo yasinukuliwe au yawekwe tu kwa kumbukumbu za vizazi vijavyo; kwamba wananchi walikuwa wanataka hili lakini walikataliwa kusikilizwa; au yatupwe?

Warioba amekwenda mbali. Ameonyesha kuwa atayanukuu na atayawasilisha – kinyume cha sheria, hadidu za rejea na kauli ya “mwenye kaya.”

Ilitarajiwa Warioba amweleze rais wake, kwa macho makavu, kuwa kile anachoagiza – Muungano usijadiliwe – hakitekelezeki kisheria na kwa misingi ya haki za binadamu. Je, alimweleza? Walikubaliana?

Ilitarajiwa Warioba amweleze rais na rais akubali na kuiambia serikali yake kupeleka marekebisho ya sheria bungeni kuondoa kitanzi kwa watakaojadili yasiyoruhusiwa. Je, alimweleza? Walikubaliana?

Kama Warioba hakufanya haya; na kilichopo ni sheria, hadidu za rejea na maagizo ya rais, basi hawezi kuepuka kuambiwa, kama alivyoambiwa Jaji Kisanga, “…hili hatujakutuma.”

Hapajawahi kujitokeza fursa nzuri ya kujadili na kutoa maoni juu ya Muungano kama hii. Kwanza, Wazanzibari tayari wameanza safari ya kueleza hatima ya Muungano pale walipofanya marekebisho ya katiba yao na kutamka kuwa Zanzibar ni nchi.

Katiba ya Zanzibar , toleo la 2010 inatambua Zanzibar kuwa nchi ndani ya Muungano. Kutambulika huko kunawaondoa moja kwa moja raia wa Zanzibar katika mjadala wa katiba, iwapo mjadala huo hautajadili Muungano.

Kwa katiba ya sasa ya Zanzibar , serikali ya visiwa hivyo, ina mamlaka kamili ya kujiamulia mambo yake. Nje ya Muungano, raia kutoka Zanzibar hawana cha kujadili katika katiba hii.

Hawana uhalali wa kuingia kwenye tume ya kukusanya maoni ya Kikwete. Hawana uhalali wa kuingia kwenye bunge la Muungano wala uhalali wa kujadili katiba.

Nje ya mjadala unaohusu Muungano, hata tume yenyewe iliyopewa kazi ya kukusanya maoni, inakuwa imepoteza uhalali. Tume itakuwa imeundwa na rais wa Muungano, lakini asiyetaka wananchi wajadili Muungano (!)

Hoja ya kwamba hii ni katiba ya Muungano haijitoshelezi kwa sababu, Watanganyika hawana jukwaa la kwao la kuandaa kile wanachotaka kiingie katika masuala ya Muungano. Hapa ndipo inakuja haja ya hoja ya wananchi kutoa maoni kuhusu Muungano.

Sheria ya kuunda tume ya katiba mpya ilipigiwa kelele na watu wengi, na kwa sehemu kubwa, kelele zilijengwa katika dhana ya kuwa tume hii inaonekana kuwa tume ya rais badala ya kuwa tume huru inayoweza kuleta katiba mpya.

Sasa uhuru huu wa kupokea, kunukuu na hatimaye kuwasilisha maoni juu ya kuwepo au kutokuwepo Muungano, Warioba anaweza kuwa ameupata nje ya sheria, hadidu za rejea na kauli za rais? Au wamejadili kimyakimya na rais bali wananchi hawajaelezwa?

Je, Warioba anajua kuwa anapingana na sheria, hadidu za rejea na maagizo ya rais? Kama anajua hivyo, amepata wapi ujasiri wa kuendelea kushika bango la kukusanya hata maoni ya wanaopinga kuwepo Muungano?

Lakini Jaji Warioba anafahamu vema kuwa suala la katiba mpya halikuwa katika ilani ya CCM, ya miaka yote tangu chama hicho kizaliwe. Hivyo basi, Rais Kikwete anaweza kuwa anafanya kazi hii pasipo utashi binafsi wala utashi wa chama chake.

Kama hivyo ndivyo, na Warioba haungani na Kikwete, basi kila mmoja atakuwa anavizia mwenzake: Ngoja nione atafanya nini?

Kwa msingi huu, hatuoni katiba mpya inayokidhi matakwa na mahitaji ya wananchi. Rais anaweza kuzika maoni ya watu juu ya Muungano; na labda maeneo mengine; na Warioba anaweza kukaa kimya kwani atakuwa amemaliza kazi yake.

Umma unataka kujua mapema iwapo tayari kuna mwafaka kati ya Warioba na mwajiri wake (rais) juu ya anayosema na kauli za rais, hadidu za rejea na sheria.

Kuna wanaotaka sheria ya mchakato wa katiba irudishwe bungeni na kufanyiwa marekebisho; viondolewe vitanzi ndipo ianze kutumika; au Warioba na timu yake ya wajumbe 30, wajiuzulu kwani kazi yao haitakuwa ya mafao yoyote kwa umma.

Lakini kuna wanaosema tume iendelee na kazi; bali kila kitakachokusanywa kiwekwe wazi, ili kama rais hakihitaji, basi wananchi wakione na “kukitumia kutoa maoni zaidi juu ya jinsi wanavyotaka kujitawala na kutawaliwa.”

Ambalo halijafahamika ni Warioba amejiandaa vipi na kwa lipi, pale Rais Kikwete atakaposimama hadharani na kusema, “…hili hatukukutuma.” Tusubiri tuone!

Kilicho wazi ni kwamba Warioba hatapenda kubabaisha au kubabaishwa. Kwa umri wake, heshima aliyovuna kutokana na kazi alizofanya, nyadhifa alizoshika na hekima, asingependa kufanya ubabaishaji.

Nayo timu yake ya watu 30 inaonekana kuwa makini na hata kuweza kumshawishi kufanya maasi zaidi pale ambapo sheria imeweka vitanzi.

Kama Warioba na Rais Kikwete hawajakubaliana kuhusu suala la maoni juu ya Muungano, basi Tume ya Warioba ni “kundi la wanaharakati;” linalokwenda kutekeleza kadri umma unavyotaka.

Warioba akiweza hilo, atakuwa amejenga ngome kuu ya hoja isiyoshindika kwa visababu rojorojo; na hata kuhalalisha matumizi ya Sh. 40m bilioni ambazo tume itatumia katika kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: