Jaji Werema anajua asemacho?


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 03 August 2011

Printer-friendly version
Uchambuzi
JAJI Frederick Werema

JAJI Frederick Werema, yule mwanasheria mkuu wa serikali amesema bungeni kuwa kuna “wasiopenda maandamano.”

Ameahidi serikali kufanyia marekebisho baadhi ya sheria kwa shabaha ya “kuwalinda” wale wasiopenda maandamano.

Nani hapendi maandamano? Maandamano yapi? Kwa shabaha gani? Hapa ndipo Werema atakwama.

Kuandamana ni kutoa maoni kwa njia ya mjumuiko wa watu wanaotembea kwa lengo lao maalum.

Penye watu wanaoandamana kupinga kitu au hatua fulani, kuna wanaoshawishika na wanaojiandaa kuandamana kuunga mkono hatua inayopingwa na wenzao.

Nikweli kuna mbifemuki – wale wasemao lolote liwalo, wao hawajali. Ama hawaoni, hawasikii, hawana hisia; au walishaporwa uwezo wa kuona, kusikia na, au kuwa na hisia.

Hao watakuwa wamefanywa butu kwa vitisho na hata ndweo za watawala au wakubwa zao; kwamba kila kitu wafanyacho watawala ni kutoka kwa Mungu na kwamba wao, mbifemuki hawahitaji kuwa na maoni.

Hawa ndio Jaji Werema anasema anataka kuwalinda; wale waliopoteza fahamu kutokana na mabavu ya watawala au umasiki uliokithiri na usiobakiza mwanya wa fikra ya kujinasua.

Uzoefu unaonyesha kuwa hata wale waliopigika kwa kunyimwa elimu (maarifa); walioporwa kauli na waliopondeka kwa  njaa, vitisho, viboko na hata bunduki na silaha nyingine; wakipata uamsho huamka.

Hata wale waliokufa na kuzikwa, kwa maana ya kuwekwa kando na kutoweka katika mzunguko wa watoa kauli za utashi; wale wasiotarajiwa kuibuka tena –  “wakitekenywa” kwa kauli na vitendo vya matumaini, hurudia “utu wao.”  

Ni hao waliokuwa wametupwa katika jalala la historia; wale waliorejea utu wao – walioufuma kwa suluba kali – ambao husimama na kutamka kwa sauti za juu kuwa wamefufuka na hawafi tena; iwe kwa vitisho au hata kwa silaha.

Vizazi vya maandamano vilishagundua kwamba bila shinikizo, akili haipenyeki – iwe ya watawala madarakani au watawaliwa waliogubikwa na vitisho na dhiki zilizoletwa na ving’ang’anizi wa madaraka.

Kwa hiyo, kwa kauli ya Jaji Werema, hakuna haja ya uamsho. Hii ni kwa sababu uamsho “utafufua” wengi, utawapa uhai walioporwa, utawapa nguvu ya kujipigania, utawaunganisha na wengine waliohai; utajenga jeshi la “ukombozi.”

Hadi sasa tumekuwa tukishuhudia maandamano na mikutano mikubwa ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama cha Wananchi (CUF).

Ukweli ni kwamba hakuna anayeshurutishwa kuingia kwenye maandamano. Hakuna anayebebwa kwa malori na mabasi hadi mikutano hiyo kama wafanyavyo viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hakuna anayetoa ahadi ya kutoa fedha, fulana, kofia za kapelo wala leseni ya biashara kwa wanaoingia kwenye maandamano na kuhudhuria mikutano. Ni utashi. Utashi binafsi.

Maandamano haya yamevutia watu wengi. Kwa nini? Kwa kuwa yanamalizika kwa mikutano mikubwa yenye ujumbe maalum unaoamsha wananchi.

Maandamano na hatimaye mikutano ni madarasa makubwa na muhimu ya umma mpana ambapo sera zimefafanuliwa; ukweli umewekwa wazi; uongo umeanikwa, wanafiki wamezodolewa na hekima imetawala.

Kwa njia hii, akili za wengi zimefunguka kwani ujumbe unaotolewa ni wa kufikirisha. Kwa njia hii pia, watu wanajiuliza, wanafikiri na kupata majibu.

Lakini Jaji Werema anasema kuna wasiopenda maandamano. Tayari tumewajadili hapo juu – wale waliomo katika ufu wa fikra na ambao walishafanywa butu kwa vitisho na unyang’anyi wa fursa na haki.

Miongoni mwa “wasiopenda” maandamano ni baadhi ya walioko madarakani ambao wanawakilishwa na Werema.

Hawa ni tofauti na wale walioporwa fursa na haki. Hawa ni miongoni mwa waporaji fursa na haki za wananchi.

Wanataka kila mmoja awe kimya; atulie kama ng’ombe anayesubiri kukamuliwa. Wanataka wanyenyekevu. Wanataka wasiojua mambo – hasa mbumbumbu wa kusweka kama kondoo.

Kwa lugha sahihi, hawa wasiopenda maandamano na mikutano mikubwa ni wale wanaohubiri “umoja, amani na utulivu” kwa wenye njaa, wasio na kazi, wasio na tiba, wasio na elimu na wasio na uhuru wa kujieleza.

Kwao “umoja, amani na utulivu” ni kukaa kimya cha usiku wa manane, kutulia kama maji mtungini; kukubali kunyolewa kwa kigae cha chupa na kutii kila amri hata kama ni kujisalimisha kwa mauti.

Yote haya yanapingana na ari na shabaha ya maandamano na mikutano mikubwa ambayo tumekuwa tukishuhudia na inayoashiria uhai wa jamii, uhuru wa kufikiri na kutoa mawazo.

Asichoelewa Jaji Werema au asichotaka kukubali ni kwamba, penye wanaounga mkono kuna wanaopinga kinachoungwa mkono.

Kwa miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika, maandamano yamekuwa yakiandaliwa na watawala. Kila walipoona sababu au walipotaka kueleza msimamo wao, waliwaita wananchi barabarani na kwenye mikutano ya hadhara.

Maandamano na mikutano, kwa miaka yote hiyo, vimekuwa, siyo tu njia ya watawala kuonyesha wanachotaka na wasichotaka, bali pia njia ya kudhihirisha kuungwa mkono na wananchi waliojitokeza.

Hapa ndipo wamekuwa wakikosea. Umati unaoingia maandamano baada ya kufunga maduka, kufunga shule, kulazimisha wakulima kutoka mashambani, kubebwa kwa mabasi na malori na kushurutishwa na wajumbe wa nyumba kumi, madiwani na watendaji wa kata, hakika hayana uhalali.

Ni maandamano hayo tuliyozoea ambayo watawala hawaogopi, bali wanafurahia. Wameyapenda kwa kuwa yameendelea kubutisha akili na hayafikirishi.

Kinachoogopwa na Jaji Werema na waliomteua, siyo maelfu kwa maelfu ya wananchi wanaojitokeza kwenye maandamano na mikutano; ni ujumbe unaotolewa kwenye maandamano na mikutano.

Ujumbe mkuu ni kwamba “kumekucha.” Huu unakwenda mkono kwa mkono na kauli ya Chama Cha Waandishi wa habari Wanawake (TAMWA) – “Sidanganyiki.”

Mapambazuko haya ndiyo chimbuko la malalamiko, woga na kiwewe cha serikali. Ndiyo msingi mkuu wa kutaka kufanyia sheria marekebisho ili “kulinda wasiopenda maandamano.”

Ni bahati mbaya kwamba Jaji Werema anatoa kauli ya kutaka kudhibiti maandamano wakati wananchi wanaendelea kushinikiza kuwa na katiba mpya ambayo inatambua maandamano kuwa ni moja ya midomo ya jamii.

Kinachoahidiwa na Jaji Werema ni hatua za kuingilia uhuru na haki ya wananchi; kwani wakati wote waandamanaji wamepinga kile ambacho wasioandamana wanapenda au wamepongeza kile ambacho wasioandamana hawapendi.

Ni utashi. Ni kufurahia kwa vitendo, uhuru na haki ya mwananchi. Je, Jaji Werema anajua marekebisho yake ya sheria yanaweza kuleta sura gani?

Haki ya wananchi ya kufikiri na kutoa maoni, hata kwa maandamano, haitolewi na serikali. Inatambuliwa tu na serikali, kuheshimiwa na kulindwa.

Cheche ilizaa moto usiozimika na ulioleta maafa makubwa. Jaji Werema, kwa nafasi na umri wake, anajua hilo. Je, ana mbinu gani za kuzuia maafa? 

0
Your rating: None Average: 4.4 (5 votes)