Jamani Mahanga anapigana vita ipi?


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 04 May 2011

Printer-friendly version
Tafakuri
Makongoro Mahanga

WAHENGA waliiasa jamii kwamba wachawi wana utamaduni unaofanana katika kufunika madhambi yao. Hulia sana kwenye msiba hasa anapokuwa ana mkono wake katika kifo husika.

Ni kawaida kwa mchawi kulia tena kwa kujionyesha alivyoguswa na msiba, aghalabu hujiweka mbele za watu ili wamwone anavyolia, alivyoguswa na msiba, yote ili kufunika kuwa na mkono katika kifo husika.

Hivi sasa, ndani ya chama tawala, CCM kuna vilio vingi; kila anayeibuka anajitia kuhubiri habari ya kujivua gamba kwa staili inayoonyesha kwamba kwa vyovyote vile hahusiki na shida, udhaifu na kila aina ya madudu yanayokabili chama hicho.

Miongoni mwa watu walioibuka mwishoni mwa wiki iliyopita kuendeleza falsafa ya wachawi, ni Makongoro Mahanga, mbunge wa Segerea. Huyu aliibukia katika tawi la Ugombolwa kata ya Segerea mwishoni mwa wiki, ambako aliwahutubia wanachama wa CCM. Kata hiyo kwa sasa inaongozwa na diwani kutoka CHADEMA.

Mahanga ambaye amekuwa akibebeshwa tuhuma nyingi juu ya kuyumba kwa CCM katika jimbo hilo, alitahadharisha kuwa chama hicho kisipojisafisha na tope la rushwa na ufisadi kama ilivyoagizwa na Halmashauri Kuu (NEC) kitapigwa mweleka kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Alikwenda mbali zaidi na kudai kuwa kupungua kwa kura za urais mwaka jana ni kielelezo kuwa chama kinaweza kuanguka, hivyo jitihada za makusudi zinahitajika kwa ajili ya kukinusuru.

Mbunge huyo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, alisema yanayotokea kwenye chama hicho kwa  sasa si dalili nzuri hivyo wanachama wasijidanganye kuwa CCM itatawala milele. Alilalamika kuwa bado wanasumbuliwa na makundi na alitaka yavunjwe kwani yakiachwa yaendelee mwaka 2015 watashindwa katika uchaguzi mkuu.

Mbunge na waziri huyo, anajenga hoja zake kwenye msingi wa matokeo ya uchaguzi ya mwaka 2005 ambayo CCM ilipata ushindi wa kimbunga wa asilimia zaidi ya 80 kwa nafasi ya urais, lakini mwaka jana ukashuka hadi asilimia 61. Kwa maana hiyo ni dhahiri kuna hatari kubwa mbele ya safari.

Ingawa Mahanga anaweza kuwa na hoja kwa maana ya kuporomoka kwa CCM katika kuungwa mkono, kwa maana kwamba hata Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) vyombo vya maamuzi ya chama hicho vikiwa vimekwisha kuthibitisha mporomoko huo, anatoa angalizo kana kwamba binafsi si sehemu ya tatizo ndani ya chama hicho.

Anaeleza kwamba hata ushindi wake ulikuwa wa mbinde, jimbo hilo likishikilia nafasi ya tatu kutoka mkiani kitaifa katika idadi ya kura, kiasi kwamba anadokeza kwamba kama wapinzani wangeungana asingeshinda ubunge.

Anataja chuki zilizopindukia ndani ya CCM kama moja ya sababu za chama hicho kupoteza mwelekeo. Anataja bila kutafuna maneno kwamba wanachama wanakihujumu chama.

Bado anaamini kwamba sekretarieti ya Yusuf Makamba ambayo ilijiuzulu yote si hatua ya ‘kujivua gamba’ ila ni mwanzo wa kuelekea kujivua gamba na isitafsiriwe kuwa mambo sasa yameshanyooka.

Pamoja na Mahanga kuonekana kujua tatizo ndani ya chama kwa kuwa “kujivua gamba ni pale ambapo viongozi watajirekebisha na kuhakikisha chama hakipati tena tuhuma za ufisadi” anakataa dhana ya kutimuana kwenye chama.

Anaamini kwamba CCM inaweza kubakia salama kwa sasa kwa kuendelea kukumbatia wote ambao wamekuwa chanzo cha ‘ufisadi’ kwa kuwa eti watajirudi.

Anaonekana kuukataa ufisadi, hasa pale anapoeleza kuwa rushwa imekuwa tatizo sugu ndani ya chama, lakini anaamini kwamba watoaji na wapokeaji rushwa waanaweza tu kuachwa wakajirekebisha na CCM ikabakia na nguvu.

Mwaka jana katika mchakato wa kura za maoni, miongoni mwa malalamiko yaliyoripotiwa katika jimbo la Segerea ni matumizi makubwa ya fedha, tangu kwenye mchakato wa kura za maoni hadi kwenye kampeni zenyewe.

Laiti kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ingelikuwa inafanya kazi yake sawasawa, leo tungekuwa tunazungumza mambo mengine kabisa kuhusu jimbo la Segerea.

Nilianza kuzungumzia hulka ya wachawi katika misiba ambayo wana mikono yao, kwa Mahanga, anajua vilivyo adhabu stahili ya kuikomboa CCM ni kujitenga na wote wenye tuhuma. Ni kuwaondoa kwenye chama na kama ingewezekana kuwachukulia hatua za kisheria.

Wapo watu wameichafua nchi kama si kuinajisi. Wameigeuza shamba la bibi. Hakuna mkataba mbaya utakaotajwa bila kuwagusa, kuanzia ya kuuza rasilimali za nchi mpaka za kuitumbukiza nchi katika mikataba mibaya.

Hawa wapo ndani ya CCM, wamefanya chama hicho kuwa kichaka cha kuficha na kulinda uchafu wao.

Ni dhahiri Mahanga anajua kinachotokea ndani ya CCM kwa sasa ni mapambano ya kitabaka kwa maana ya waliokamata madaraka, wenye fedha dhidi ya uasi na hasira ya umma ambao una nguvu ya kura.

Wenye nguvu za fedha wanajua fika kwamba fedha pekee haziwezi kusaidia chama hicho walau kwa sasa, kinakwenda na maji hasa pale fedha zenyewe zinapokuwa na harufu ya uvundo, kama Kagoda, kama rada, kama Meremeta, kama Richmond na Dowans.

Ndiyo maana wanajaribu sasa kuwaondoa wenye harufu ya mambo yanayofanana na hayo hapo juu ili kusaka huruma na kukubalika tena kwa wenye kura. Kwa bahati mbaya, Mahanga pia anajua kuwa wenye kura wameamka, wanajua wanavyodhalilishwa, wanavyotumika mwaka baada ya mwaka kuwa migongo na ngazi ya wakubwa kukwea na kubakia huko kileleni bila kurejesha chochote kwao.

Wenye kura wanajua kuwa waliojichimbia kileleni ni hatari kwa ustawi wao, kwa kuwa ni hatari wameanza kuonyesha dhahiri kuachana nao kwa vitendo halisi kama walivyoonyesha kwenye uchaguzi mkuu uliopita.

Kwa bahati nzuri pia Mahanga analijua hili, lakini anataka kuwe na makubaliano ya kusameheana kwa ujumla, bila kueleza kwa yakini waliokichafua chama hicho wataadhibiwa vipi ili walau wenye kura wawe na imani na chama hicho.

Mahanga anakataa kuunga mkono hoja ya kufukuzana, anataka kurekebishana, lakini hasemi walioifikisha nchi hapa ilipo, madeni, kukosekana uadilifu na watu kunajisi ofisi za umma kwa kujilimbikizia utajiri binafsi watafanywa nini.

Mahanga anataka kushiriki mapambano ya kukisafisha chama kikiwa kimevaa nguo zake, kisha atarajie kitakate. Anataka wachafu waendelee na hadhi, staha na kila walichojipatia kwa hila na aina zote za ghilba, kwa kisingizio kuwa wanajenga maridhiano bila kuadabishana.

Hiki ndicho nakiona kama kilio cha mchawi; anatamani machozi yake yafunike ubaya wake, kwamba jamii imwamini kwamba yu mwema sawa na watu wengine. Katika hali hii Mahanga ni lazima ajue hatafanikiwa, dawa ni moja tu, kunyoana ndiyo njia pekee, kinyume chake ni kudanganyana tu. Kima ni kura za 2015. Tusubiri. 

0
Your rating: None Average: 4.7 (3 votes)
Soma zaidi kuhusu: