Jambele: Natamani kuwa Mbunge Ukonga


Editha Majura's picture

Na Editha Majura - Imechapwa 25 November 2009

Printer-friendly version
John Jambele

ANAONGEA kwa taratibu. Haonyeshi kuwa mwenye majigambo kama ilivyo kwa baadhi ya wanasiasa wenye rika kama lake.

Ni John Jambele (42), mzaliwa wa Magamba, Lushoto, mkoani Tanga. Ni mhasibu Ofisi ya Rais, katika Sekretariati ya Maadili. Huyu ametangaza kuwania ubunge jimboni Ukonga, Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam.

Hivi sasa jimbo hilo linawakilishwa na Milton Makongoro Mahanga (CCM) ambaye ni Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana anayemalizia kipindi cha pili cha uwakilishi.
 
Siku chache baada ya Jambele kutangaza nia yake ya kuwa miongoni mwa watakaoomba kuiwakilisha CCM kwenye uchaguzi mkuu ujao, Mahanga alikaririwa akisema,

“Waache wajitokeze tu. Hakuna harusi isiyokuwa na wasindikizaji; lakini bwana harusi ni mmoja tu.”

Jambele hajitangazii ushindi dhidi ya wagombea wenzake. Anaamini wanachama wa CCM wa Jimbo la Ukonga watatumia hekima na busara kuchagua mwakilishi mwenye sifa stahiki.

Sifa za mtu anayestahili kupeperusha bendera ya chama hicho zinaelezwa na Jambele kwamba zimeainishwa kwenye taratibu za uchaguzi na Katiba ya CCM.

Jambo hilo analieleza kuwa njia muafaka ya kukiondolea chama ugumu wa kupata ridhaa ya wananchi ili kuongoza Ukonga.

Mchakato wa uchaguzi ndani ya CCM unatarajiwa kufanywa baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuvunjwa rasmi mwaka kesho.

Katika mahojiano yake na MwanaHALISI wiki hii, Jambele anasema amekuwa akiishi jimboni Ukonga kwa miaka 25 sasa.

Pamoja na Uwanja wa siasa nchini kuashiria kuwa mgumu na wenye mapambano makali ya kisiasa, Jambele anasema hana hofu na hali hiyo.

“Sina hulka ya kukata tamaa wala kuogopa; hususan katika ninachoamini kuwa ni stahili yangu. Ni wapiga kura peke yake wanaoweza kuzuia nia yangu ya kuwakilisha chama changu na hatimaye kuwa mwakilishi wa Ukonga,” anaeleza Jambele.

Imezoeleka kusikia baadhi ya wagombea wakisema,“Nimeombwa na wananchi wa jimboni kwangu nigombee ili niwe kiongozi wao.” Kwa Jambele ni kinyume.

Anasema hakuombwa wala kushawishiwa na mtu au kundi la watu. Ametafakari kwa kina kabla ya kuchukua uamuzi huo.

Hata hivyo ameeleza kuwa kabla ya kutangaza nia ya kutaka kuchaguliwa kukiwakilisha chama hicho, aliafikiana na familia yake.

Jambele ameoa. Yeye na mke wake Flora, wana watoto wanne. Anawataja kuwa ni Jaqueline, Jeska, Julieth na Johan.

Alijiunga na CCM akiwa kidato cha pili, Shule ya Sekondari ya Magamba, wilayani Lushoto na kupata fursa ya kuwa Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM wa shule hiyo.

Anasema ingawa siasa lilikuwa moja ya masomo waliyokuwa wakifundishwa, fursa hiyo ya uongozi wa vijana ilimwongezea kupenda siasa.

Jambele anaeleza uwezo wake wa kuongoza jimbo la Ukonga kuwa unatokana, pamoja na mambo mengine, elimu, umri wake unaomruhusu kujichanganya na watu wa rika zote pamoja na afya bora na salama aliyonayo.

Hata hivyo anasema wameruhusiwa kutangaza nia tu. Anaahidi kuzungumza kwa kina na uwazi wakati wa kampeini ukiwadia.
 
Anasema hana fedha za kuhonga ili apewe upendeleo wa kuwa mwakilishi wa CCM Ukonga wakati wa uchaguzi mkuu mwaka kesho.

Pamoja na kwamba rushwa ni adui wa haki, Jambele pia anatambua ukubwa wa jukumu la mbunge kwa jamii. Anasema haoni sababu ya “kununua” jukumu hilo.

Lakini anasema anavyowafahamu wapiga kura wengi wa Jimbo hilo, hawana tamaa ya fedha za kuhongwa wakati wa uchaguzi. Anasema anatambua mahahitaji yao kuwa ni kupata mbunge mwenye kuwaheshimu, kuwasikiliza na kushirikiana nao kuleta maendeleo.

Kipengele kimoja miongoni mwa ahadi tisa za wanachama katika Katiba ya CCM kinasema, “Rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa.”

Kwa Jambele, dhana kwamba mfumo wa siasa ya ujamaa na kujitegemea umeshindwa ni dhana potofu. Anasema hatua ya serikali kuagiza viongozi nchini kujitenga na biashara, ni moja ya hatua za kurejea utekelezaji wa mfumo huo wa siasa.

Anaamini hilo litasaidia katika kupunguza kasi ya baadhi ya wanaotumia nyadhifa zao kujipatia utajiri kwa njia zisizokuwa halali.

Hapendezwi na siasa za “kupakana matope.” Anasema kuwa zinajenga chuki miongoni mwa watu. Anashauri wana CCM kuzingatia maadili na kuwa na umoja kwa maslahi ya taifa.

Anasema yeye ni “muumini” wa Azimio la Arusha lililoasisiwa 5 Februari 1967 chini ya chama cha Tanganyika African National Union, (TANU).

Jambele anarejea mara kwa mara kauli kwamba dhana ya kushindwa kwa mfumo wa ujamaa na kujitegemea ni potofu. Anasema Azimio la Arusha halikushindwa bali baadhi ya viongozi walishindwa au walikataa kulitekeleza.

Anataja nchi ya China kuwa ndiyo mfano mzuri wa kuigwa kwa matumizi sahihi ya mfumo huo wa siasa, ambao sifa yake kuu ni kufanya kazi kwa bidii.

Pamoja na mtikisiko wa uchumi unaoikabili dunia, anasema China inawekeza dola za Marekani trilioni 40 kwenye nchi mbalimbali duniani.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: