January Makamba ni wakala wa Dowans?


Isaac Kimweri's picture

Na Isaac Kimweri - Imechapwa 23 February 2011

Printer-friendly version
Tafakuri
January Makamba

BABA wa Taifa Mwalimu Nyerere, katika moja ya hotuba zake alisema, ikulu ni mahali patakatifu. Alitumia neno ‘takatifu’ si kwa bahati mbaya. Kamusi inazungumzia neno hilo kama kitu kisichokuwa na dhambi, kilichotakasika.

Kwa maono ya Nyerere ni kwamba, mtu yeyote ambaye ana mawazo ya kwenda ikulu  lazima wakati wote ajue mahali hapo ni pasafi, kwa maana ya matendo yake na mwenendo mzima wake ni lazima wakati wote uwe juu ya tuhuma.

Kukaa kwake ikulu kamwe kusihusishwe na dhambi yoyote, iwe ya kutenda mwenyewe kama vile ufisadi, au hata ya kusaidia kundi fulani katika jamii kutenda ufisadi au uchafu wowote.

Katika kutekeleza majukumu yake, Rais hakika hawezi kufanya kila kitu peke yake, atakuwa na wasaidizi. Hawa ni watendaji na washauri wa Rais; ndio wanaotekeleza kwa vitendo halisi yale yote anayoamua.

Haipendezi wala haivumiliki mtumishi wa umma ambaye anakaa ikulu, kwa maana ya kumsaidia Rais katika majukumu yake atajwe kwenye kashfa yoyote chafu; kwa maana ya mahusiano au uchafu wa ukwapuaji wa mali ya umma kwa njia za hila yeye binafsi au kusaidia kundi fulani la watu.

Kwa maneno mengine, wale wote wanaoteuliwa na Rais kumsaidia kazi ikulu,  lazima waishi kama watakatifu ili matendo yao yasije kuchafua mahali patakatifu—Ikulu.

Kwa msingi huo huo, wale wote waliofanya kazi ikulu watokapo, ni vema wakaonekana wakiendelea na utakatifu huo, ili umma usije kudhania kwamba wakiwa ikulu walijifunza utukutu au ubazazi.

Haya yote ninayazungumza baada ya kumtazama kijana mwanasiasa January Makamba, mbunge wa Bumbuli na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini.

January akiwa amekaa ikulu chini ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete tangu 2006 hadi 2010, ni matarajio ya wengi ikulu ilimlea na kumkuza kisiasa na kukomaa kwa uadilifu, ili kokote atakakokuwa ang’ae na kubeba ile taswira ya utakatifu.

Kwamba January ameibuka kwa kasi katika anga za siasa nchini, si jambo la kustaajabisha, lakini pia kusema kwamba kupaa na kung’aa huko kumechangiwa sana na kukaa ikulu si kitu cha kubeza au kubishiwa na yeyote anayejua kupambanua mambo kwa mapana yake.

Kwa haiba, January anaonekana kama kijana mwerevu, mcheshi na anayethubutu. Alijitahidi kujinadi kwa njia mbalimbali kujipenyeza kwenye jimbo la Bumbuli lililokuwa limekaliwa na William Shellukindo tangu mwaka 1995.

Alifanikiwa kupitia njia halali za kura kwenye mchakato wa kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). January hakupata mpinzani kutoka vyama vya upinzani, kwa hiyo jasho lake lilitoka kwenye kura za maoni tu.

Nyota ya January iling’aa zaidi mapema mwezi huu alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati nyeti ya Bunge ya Nishati na Madini. Kwa Kiswahili wanasema utuki yaani mambo yanayotokea kwa kufanana, nafasi ambayo pia alikuwa amekalia Shellukindo.

Kabla hata ya kuukwaa uenyekiti wa Nishati na Madini, alikwisha kumwandikia barua Waziri wa Nishati na Madini akilalamikia mgawo wa umeme, lakini pia alitaka ‘siasa ziwekwe kando’ katika kushughulikia suala hilo .

Barua hiyo, kwa njia ya ‘ki-spin doctor’ ilipenyezwa kwenye vyombo vya habari ilhali ilikuwa  waraka kwa waziri kama ushauri juu ya umeme.

Ninachotaka kusema hapa ni kwamba January hakutaka kuchukua njia ya dhahiri ya kutaka kuiwajibisha serikali kama vile kuwasilisha hoja binafsi bungeni kuhusu suala la umeme, ila alitaka njia za majadiliano ya ndani kwa ndani. Lakini cha ajabu barua yake iliibukia kwenye magazeti!

Muda si muda, January alivunja ukimya juu ya mitambo ya Dowans; alisema wazi kwamba alikuwa anaishauri serikali kuwashwa kwa mitambo hiyo, huku akijikinga kwenye jukwaa la ‘kuacha siasa katika masuala ya kiutendaji’.

Hoja hii, duru zinasema, ilipowasilishwa kwenye kamati yake, ilikumbana na kizingiti kikali. Mmoja wa wabunge walimtaka atangaze maslahi yake kwa jinsi alivyokuwa analisukuma suala la Dowans kwa hisia na nguvu kubwa.

Hakuna Mtanzania anayefuatilia masuala ya nchi yake asiyejua Dowans. Dowans ni mrithi wa mkataba wa Richmond ambao uliangusha baraza la mawaziri mwaka 2008. January alikuwa ikulu wakati kadhia hii ikitokea na kwa hakika alijua vilivyo hali hii ilivyomwathiri Rais wake.

Lakini pia January shaka anajua vilivyo kuwa Dowans ina kesi na TANESCO juu ya kulipwa fidia ya Sh. 94 bilioni, ambazo kila Mtanzania ameipinga; taifa limeingia taharuki kubwa juu ya fidia hii iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Ushuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC). Umma una hasira na jazba papo! January anafahamu haya yote.

Kubwa zaidi, January anajua  kuwa kuna mapingamizi yamewasilishwa Mahakama Kuu juu ya hukumu hiyo, na kwa ujumla wake kuna mambo mengi yenye wingu zito nyuma ya mkataba wa Dowans kwa sababu ‘uliporwa’ kwa Richmond katika mazingira ambayo TANESCO hadi leo wamepigwa butwaa.

Kwa maana hiyo, ingawa Dowans walizalisha umeme wa megawati 100 bado haijawa halali kwa Dowans kudai kuwa ni kampuni safi kwa sababu njia waliyoingilia nchini imejaa mbigiri na michongoma michungu.

Binafsi naamini kwamba January ambaye ni mwerevu na kijana jasiri anaielewa historia hii, lakini tatizo linaloibuka sasa ni pale anapojaribu kujitia eti anajenga zama mpya za siasa za Tanzania kwa kushindwa kujua kuwa historia ndiyo inayofinyanga kila kitu katika maisha ya binadamu.

Histioria ya kukaa karibu na waridi ndiyo imemfinyanga January kuwa hapo alipo leo; hizi ni pamoja na nafasi ya Baba yake, Yusuf Makamba, Katibu Mkuu wa CCM tangu mwaka 2007; pia kuwa msaidizi wa Rais Kikwete, masuala ya hotuba.

Ni kwa maana hiyo tunamkumbusha January kwamba hawezi kukwepa historia ya Dowans kama ambavyo hawezi kukwepa historia yake mwenyewe.

La mwisho ambalo ndilo linalobeba muktadha wa uchambuzi huu ni juu ya historia ya kufanya kazi ikulu na utakatifu; kwamba kazi anayoifanya sasa ni kama mtu aliyepewa kazi maalum ya kutumwa kusafisha Dowans.

Kusaidia malipo yatoke; kuhalalisha biashara yake na TANESCO, ndiyo maana ya lugha ya ‘kuacha kuingiza siasa katika mambo ya utendaji’. Hii ni kauli ya kutaka kufunika kombe ili mwanaharamu Dowans apite.

Ni nguvu za nani zinamsukuma kufanya haya yote kwa kisingizio cha ‘siasa mpya za kutokuingilia watendaji?’ Ushauri wa bure ni huu, January punguza kasi utashika kaa la moto mapema mno.

0
Your rating: None Average: 3 (3 votes)
Soma zaidi kuhusu: