Jeshi ni mbeleko ya maovu ya viongozi


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 21 September 2011

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

TANZANIA imeendelea. Kila mwanasiasa au kiongozi ni mshauri wa waandishi wa habari.

Utasikia, “Waandishi wameshauriwa wazingatie taaluma na maadili ya kazi yao.” Huyo anayeshauri hasemi maadili yaliyokiukwa hadi kila mwanasiasa asisitize kuzingatia maadili. Ila kwa upande wa serikali, madai kama hayo huwa ni hatua moja kabla ya kuzima cheche za chombo fulani cha habari.

Wengi wanaokimbilia kutoa ushauri ni wale waliofanya madudu kama kuchukua kitu kidogo au kueleza siri za nchi, kama wanatapika, kwa wanadiplomasia, hivyo hawataki waanikwe.

Basi watakiwinda chombo kilichowaanika, watakisuta, watalaani kila siku ili ionekane kwamba kinaongopa, kinazusha na kinafanya uchochezi.

Katika baadhi ya masuala, viongozi fisadi wakiona wameshindwa kuzuia kalamu chokonozi, hutumia ‘mbeleko’ kama vile kusema, suala hilo ni la jeshi au usalama wa taifa.

Mfano, vyombo vya habari vilivyoibua na kushupalia kashfa ya uingizaji sukari vilifunikwa na mbeleko hiyo vilipoambiwa ni mali ya jeshi hivyo kudodosa zaidi ni kuingilia masuala ya jeshi.

Ukweli mafisadi walitumia tu kibali cha jeshi na ukweli ulipowekwa wazi, Idd Simba, ambaye alikuwa waziri wa viwanda na biashara, alilazimika kujiuzulu.

Mbeleko ya jeshi ndiyo imetumika kuzuia vyombo vya habari kudodosa ufisadi katika ununuzi wa rada. Ni kweli rada ni ya jeshi lakini viongozi waliopewa kazi ya kuinunua waliongeza ‘chenji’; bei ikawa juu mara dufu – huu ni wizi si usalama!

Wakati vyombo vya habari vilifanya kazi nzuri kuibua kwa lengo la kuzuia ufisadi huo, viongozi wetu, wanaojidai ni wazalendo, walilaani eti vinafanya uchochezi.

Suala la rada lilizua mjadala mzito Bunge la Uingereza na aliyekuwa Waziri wa Misaada ya Maendeleo ya Afrika, Clare Short alisema; "Siku zote ukweli utabaki kwamba mradi huu usio na maana ni ufisadi."

Hiyo ilikuwa nafuu kwa vyombo vya habari vya Tanzania kwani viliruka kiunzi cha mjadala kwamba rada haikuwa tu kifaa cha usalama wa nchi bali siasa na ufisadi. Taasisi ya kuchunguza makosa makubwa ya jinai ya Uingereza (SFO) ikasaidia zaidi kutaja wahusika na hapo ndipo akapatikana miongoni mwao Mzee wa Vijisenti.

Katika hali ya kushangaza mtu aliyepewa jukumu la kupambana na ufisadi kupitia Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hoseah, akajitokeza kudai SFO imemsafisha mzee huyo. Watanzania walishangaa.

Kilichosababisha Dk. Hoseah kupiga nakshi rushwa badala ya kupambana nayo kilifichuka Desemba 2010, mtandao wa WikiLeaks ulipoanika mazungumzo ya siri kati yake na mwanadiplomasia wa Marekani, Purnell Delly.

Mtandao huo maarufu kwa kuchapisha taarifa za siri, binafsi na maalum kutoka vyanzo tofauti, habari zilizovuja na watoa habari, ulimnukuu Dk. Hoseah akimwambia Delly, Julai 2007, jijini Dar es Salaam kuwa atawashtaki wahusika wote wa ufisadi katika ununuzi wa rada kutoka kampuni ya BAE Systems ya Uingereza.

Mwanadiplomasia huyo alikaririwa akisema, “Aliuita (Dk. Hoseah) mpango ule kuwa ‘mchafu’ na akasema ulihusisha maofisa kutoka Wizara ya Ulinzi na angalau ofisa mmoja au awali wa ngazi ya juu wa jeshi hilo.”

Hoseah alizungumza kwa huzuni kuhusu mwelekeo wa juhudi za taasisi hiyo na matarajio yake ya awali kushtaki “mapapa” wa ufisadi. Pia alisema anahofia maisha yake.

Mtandao ulimkariri zaidi Delly akisema: "Alitueleza kwa uwazi… kesi dhidi ya waziri mkuu au rais haziwezi kujadiliwa…” Hao inadaiwa “hawaguswi”.

"Alisisitiza kwamba Rais Kikwete hafurahishwi kabisa kuona sheria ikishughulikia kesi kubwa ambazo kwa vyovyote zitawahusisha maofisa wa ngazi ya juu serikalini." Hii inatokana na sababu kwamba “Kikwete hataki kuweka mfano” kwa kushughulikia watangulizi wake.

Dk. Hoseah aliibuka na ‘kuupotezea mbali’ mtandao huo au kwa lugha sanifu alitupilia mbali tuhuma hizo akidai ni uzushi. Kachero huyo akataka waandishi wa habari wawe makini na kalamu zao.

Lakini hata bila habari hizo kuandikwa na WikiLeaks suala la mgodi wa Kiwira limefichwa na serikali mpaka ikaamua kula hasara kulipa fidia huku na kule mradi tu kumwondoa Rais mstaafu Benjamin Mkapa katika kashfa hiyo.

Mkapa akishtakiwa ina maana Rais Kikwete ameridhia. Hiyo ndiyo sababu rais alikaririwa akisema hataki kuwa mfano mbaya. Suala la Richmond likayumbishwa na baadaye aliyekuwa Waziri mkuu, Edward Lowassa akajiuzulu. Kuna la zaidi? Hiyo Richmond si ikawa Dowans ambayo imebatizwa jina la Symbion Power na mama wa ubatizo ni Hillary Clinton?

Ili wanaharakati, wanasiasa na waandishi wa habari wasihoji zaidi viongozi wa serikali hii wakalisukumizia Jeshi mradi wa Meremeta. Wabunge wakihoji fedha za mradi huo wanasema fedha hizo ni kwa masuala ya jeshi.

Mwezi huu, mtandao huo umeanika habari mbili nzito: Moja kuhusu taarifa kwamba Ali Albwardy, mfanyabiashara wa Dubai aliyepigiwa upatu kununua Hoteli ya Kilimanjaro, alimhonga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Jakaya Kikwete suti tano. Pili, kwamba aliyekuwa CDF, Jenerali George Waitara alizuia Marekani kuweka nchini kituo cha mafunzo ya kijeshi.

Ikulu imekanusha na Jeshi limekanusha katika mtindo uleule wa kulaani, kufundisha namna ya kutafuta habari, kuandika na kushauri waandishi wazingatie maadili ya taaluma yao. Tunaheshimu taarifa hizo.

Lakini mbona hatusomi habari za Delly akikanusha au akiomba radhi kumpakazia Dk. Hoseah? Mbona hatusomi popote habari za Balozi, Michael Retzer akikanusha kutetea na Wikileaks kuhusu habari ambazo alimkariri meneja wa hoteli ya Kilimanjaro-Kempiski, Lisa Pile akidai bosi wake Ali Albwardy alimhonga suti tano Kikwete?

Serikali imechukua hatua gani dhidi ya viongozi ambao wakiwa nje au na wanadiplomasia wanatapika kila kitu na mambo ya siri kama yanavyoibuliwa na Wikileaks? Serikali italaani vyombo vya habari lakini inachukua hatua gani dhidi ya viongozi hawa wanaoeleza siri za nchi na kutuacha uchi? Hawa si ndio wanavujisha siri, mbona wanalindwa?

Serikali inaogopa nini kuwahoji  mabalozi hao au hata kutaka Marekani itoe msimamo kuhusu uzushi wa wanadiplomasia hao?

Aah! Dk. Hoseah aliyeshindwa kupambana na mapapa wa ufisadi, amekimbilia Taasi ya Elimu Tanzania (TET) eti kuomba wanafunzi wafundishwe ubaya wa rushwa.

Anadhani watoto ambao baba zao wameneemeka kwa ufisadi, wao watakataa? Anadhani watoto ambao mama zao wamevimbiana kwa ufisadi wataelewa somo hilo? Kwani watoto hawaoni au hawasomi kwamba mpaka leo Meremeta imefunikwa kwa mbeleko nzito ya jeshi? Mwanafunzi gani hajasikia viongozi wetu wakigoma kuwafikisha mahakamani wezi kupitia Kagoda, Deep Green Finance?

0789 383 979, jmwangul@yahoo.com
0
No votes yet