JK amechakachua mambo ya msingi


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 17 November 2010

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

KILA mbunge alikuwa na shauku ya kumsikiliza Rais Jakaya Kikwete, mshindi kwa asilimia 80.2. Kwa kiasi kikubwa aliteka hisia za watu na gumzo likawa atawapa matumaini gani mwaka 2005-2010.


Miaka mitano baadaye amepata madoa. Ushindi wake unahojiwa na wananchi, mpinzani wake mkuu amekataa kutambua matokeo.


Ataeleza nini; atawaambia nini wabunge, atawapa dira gani iliyojaa matumaini katika kipindi cha miaka mitano ijayo? KK amekosa msimamo katika mambo ya msingi; amelea ufisadi na uchakachuaji umemwingiza ikulu—hawezi kuwa na jeuri ya 2005.


Alipozindua Bunge la Jamhuri ya Muungano, Desemba 30, 2005, JK alifafanua kwa kina dira, mwelekeo na malengo ya serikali yake. Alitoa Ahadi 10 za Ilani ya CCM kwamba Serikali ya Awamu ya Nne:

 • Itahakikisha kuwa Amani, Utulivu na Umoja wa nchi yetu na watu wake vinadumishwa;
 • Itadumisha na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana tangu Serikali ya Awamu ya Kwanza hadi leo;
 • Itaendeleza vita dhidi ya umaskini, ujinga na maradhi, tena kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya;
 • Itatimiza ipasavyo wajibu wake wa utawala na maendeleo, na itaendesha dola kwa misingi ya utawala bora na uwajibikaji; utawala wa sheria unaoheshimu na kulinda haki za binadamu;
 • Itaimarisha uwezo wake wa kulinda maisha na mali za raia wake. Tutapambana na uhalifu wa kila aina, na majambazi hayataachwa yatambe yatakavyo;
 • Itahakikisha mipaka ya nchi yetu ipo salama. Hatutamruhusu mtu au nchi yeyote kuchezea mipaka ya nchi yetu na uhuru wetu;
 • Itafanya kila iwezalo kuhakikisha Tanzania ina mahusiano mazuri na mataifa yote duniani, pamoja na mashirika ya kimataifa na kikanda;
 • Itajali sana maslahi na mahitaji ya makundi maalum katika jamii kama vile wanawake, vijana, watoto, wazee, walemavu na yatima;
 • Itaongoza mapambano mapya ya kuhifadhi mazingira ili vizazi vijavyo virithi nchi nzuri, na msingi imara wa maendeleo endelevu; na
 • Itaendeleza michezo, na shughuli za utamaduni na burudani.

Alivyojiangusha

Ili afanikiwe vizuri watu waliokuwa na mapenzi mema walishauri asithubutu kuingiza urafiki, udugu katika uteuzi wa wabunge kushika nafasi za uwaziri.


Alisikia lakini ama hakuzingatia au haambiliki. Baada ya kuapishwa kushika dola, JK alifanya uteuzi wa wasaidizi wake.


Alimteua Johnson Mwanyika kuwa mwanasheria mkuu na swahiba wake Edward Lowassa kuwa waziri mkuu. Hao wawili walihusishwa moja kwa moja na kashfa ya Richmond iliyoyumbisha Serikali ya JK.


Mwanyika alistaafu kabla hajachukuliwa hatua kama lilivyopendekeza Bunge, na Lowassa alijiuzulu wadhifa huo.


Waliomfuata Lowassa ni aliyekuwa Waziri wa Madini na Nidhati, Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha aliyekuwa Waziri wa Afrika Mashariki ambao Tume ya Bunge ilibaini kuwa walihusishwa katika kashfa ya Richmond.


Hao wote walijiuzulu Februari 8, 2008, JK akapata fursa ya kulivunja Baraza la Mawaziri akaunda jipya lenye mawaziri 47. JK alimpoza Lowassa kwa kusema hiyo ni ajali ya kisiasa.


Wakati anavunja Bunge Julai 16, 2010, JK alijisifu kuwa anaona fahari kusema, “Tumepiga hatua kubwa katika kutekeleza malengo yetu hayo. Tumefanikiwa pia mambo mengine mbalimbali tuliyoahidi katika ilani ya Uchaguzi ya Chama tawala au kujitokeza kwa nyakati au mahali mbalimbali”.


Alisema, “Viwango vya mafanikio vinatofautiana kwa kila sekta, hata hivyo, tumesonga mbele kwa kasi ya kuridhisha, japo bado tuna safari ndefu kuelekea kwenye maisha bora kwa kila Mtanzania”.


Anaposema “tuna safari ndefu kuelekea kwenye maisha bora kwa kila Mtanzania” wananchi wanahoji mbali kiasi gani. Maana mbali ya ahadi 10 JK aliahidi pia;

 • Kujenga nyumba za walimu nchi nzima na vituo vya afya kila kata, lakini hiyo imebaki kuwa ndoto.
 • Kuboresha mishahara ya wafanyakazi lakini ameishia kukorofishana nao na kutishia kuwapiga virungu.
 • Kuboresha bei ya mazao; amefanikiwa kiasi kwa kuanzisha stakabadhi ghalani, lakini bei bado ni ndogo.
 • Kupunguza gharama za umeme, lakini gharama  zimepanda sawia na petroli, dizeli na mafuta ya taa.
 • Kupitia upya mikataba ya madini ili iwe na manufaa; amejaribu lakini aliruhusu mkataba wa mgodi wa Bulyanhulu kutiwa saini nje ya nchi tena usiku.
 • Kudhibiti ujambazi kwa asilimia kubwa, lakini yakaibuka mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi ‘albino’.

Rushwa

Ahadi yake ya kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya rushwa, ubadhirifu wa mali ya umma na matumizi mabaya ya madaraka nchini anasema imetimia. Lakini ukweli ndiyo sehemu iliyomsababisha alaumiwe na hata serikali yake kuyumba.


Kwanza rushwa ilijikita ndani ya chama tawala. Mwaka 2007 wakati wa uchaguzi wa viongozi kuanzia ngazi ya vijiji, wilaya, mikoa na ngazi ya taifa; rushwa ilitumika.


Wabunge wawili na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa kutoka mkoani Arusha walinaswa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), lakini baadaye ikaelezwa hawakuhusika, wakafutiwa tuhuma
Rushwa imetumika pia katika uteuzi wa wagombea ubunge mwaka huu. Watu kadhaa walidaiwa kunaswa lakini ni wawili tu waliofikishwa kortini.


Katibu mkuu wa CCM, Yussuf Makamba alithibitisha pasina shaka kwamba kila mgombea ndani ya CCM alitoa rushwa ila walizidiana.


Kitakwimu, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita atasema amefanikiwa kwa kufikisha mahamani kesi za rushwa 780 ambapo serikali imeshinda kesi 160. Kesi gani hizo?

Kikwete ataanza muhula wa pili wa uongozi wake huku akisumbuliwa na masuala mazito aliyokwepa kuyapa ufumbuzi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.


Rushwa ya rada inayomkabili aliyekuwa Mwanasheria mkuu na Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge. Alinaswa na Taasisi ya Kuzuia Makosa Makubwa ya Rushwa ya Uingereza (SFO) na serikali kupitia Takukuru imefunika.


Takukuru iliyowahi kudai hakukuwa na harufu ya rushwa katika mkataba wa Richmond iliibuka na kudai faili la tuhuma za rushwa dhidi ya Chenge nchini Uingereza limefungwa.


Hata hivyo, Uingereza imekanusha madai ya Takukuru. Je, hii si aibu kwa serikali ya JK? Uaminifu wa Takukuru uko wapi?

Je, JK amefanikiwa katika vita dhidi ya umaskini, ujinga na maradhi? Je, ametimiza ipasavyo wajibu wake wa utawala kwa misingi ya utawala bora na uwajibikaji; utawala wa sheria unaoheshimu na kulinda haki za binadamu?

Je, uchakachuaji matokeo ya uchaguzi mkuu ni sehemu ya demokrasia na utawala bora?

Desemba 30, 2005 JK aliwatoa hofu wananchi kutokana na wapinzani wake wa kisiasa kudai kuwa tabasamu lake ni dalili kwamba hawezi kuwa na msimamo.


Alisema, “I might be wearing a smile, but I am firm on serious issues.” Nina msimamo katika masuala ya msingi.” Kwa kuangalia aliyoahidi na aliyofanya miaka mitano iliyopita, JK ‘amechakachua’ mambo ya msingi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: