JK aanza kwa gia iliyozoeleka


Hilal K. Sued's picture

Na Hilal K. Sued - Imechapwa 17 November 2010

Printer-friendly version

UONGOZI wa juu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya umeanza duru ya pili ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete kwa gia inayofahamika vema na iliyozoeleka.

Gia hiyo ni ya kurushiana matope, shutuma kali pamoja na kuendeleza kashfa za ufisadi.

Mara baada ya matokeo rasmi ya uchaguzi kutangazwa, vigogo wawili wa chama hicho ambao ni wajumbe wa Kamati Kuu (CC) – Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa zamani Andrew Chenge, na Spika wa Bunge lililopita Samwel Sitta walianza kurushiana matope hadharani katika kuwania kiti cha uspika wa Bunge jipya.

Malumbano hayo yameonyesha kwamba siyo tu Kamati ya Usuluhishi ya Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi ya mwaka jana haikufanya kazi, bali pia yameibua upya mbele ya jamii kashfa ya ufisadi wa rada, ambayo ilianza kusahaulika.

Kwa tafsiri yoyote ile, kashfa hiyo imetia aibu kubwa, utendaji mzima wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) hadi kufikia baadhi ya watu kuipa jina la mzaha – Taasisi ya Kusafisha na Kulea wala Rushwa.

Aidha wasomi na wanaharakati wengine wanaopinga ufisadi wametaka taasisi hiyo ivunjwe, kwani kuwepo kwake hakuna tija kwa nchi, na hasa katika kutimiza malengo yake.

Kuna baadhi pia wamelitaka Bunge jipya kuanza kazi yake kwa kuichunguza taasisi hiyo kwa kuundiwa kamati maalum ya Bunge.

Iwapo Bunge litakubali kufanya hivyo, basi hadithi itakuwa ni ile ile ya siku zote, kuibuka upya makundi ambayo yatakuwa yanatetea masilahi yao na kukwepa ukweli na halihalisi. Kwa upande mmoja namsikitia sana Spika mpya Anne Makinda.

Yote haya yameibuka kufuatia hatua ya Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo – Edward Hoseah kutoa taarifa ‘rasmi’ kwamba tuhuma za ufisadi dhidi ya Andrew Chenge iliyotokana na ununuzi wa rada chakavu na ya bei kubwa kutoka Uingereza zilikuwa tayari zimefutwa.

Hii haikuwa mara ya kwanza kwa Hosea kutoa taarifa kama hiyo inayozua utata. Aliwahi kutoa taarifa kwamba hakukuwa na harufu yoyote ya rushwa katika uidhinishaji wa mkataba wa kampuni ya Richmond kufua umeme nchini.

Serikali ya Uingereza, kupitia ubalozi wake hapa nchini, imelazimika kuingilia kati kwa kutoa taarifa kwamba tuhuma dhidi ya Chenge bado hazijafutwa kama inavyodaiwa na Takukuru na kwamba kwa ushahidi uliopo mtuhumiwa huyo anaweza kupandishwa kizimbani.

Taasisi ya kuchunguza masuala makubwa ya ufisadi nchini Uingereza (SFO) ndiyo iliendesha uchunguzi kuhusu yaliyojiri katika mpango wa rada baada ya kampuni iliyoiuzia Tanzania mtambo huo – BAE – kutuhumiwa kwamba ilitoa mlungula kwa maafisa wa serikali ya Tanzania ili kufanikisha ununuzi.

SFO iligundua kiasi cha dola 1.2 milioni katika akaunti ya Chenge katika benki moja katika kisiwa cha Jersey, fedha ambazo mtiririko wake ulionyesha ulitokana na mlungula kutoka BAE kupitia mtu wa kati.

Wapo wanaohoji hatua ya Uingereza kwamba mbona serikali yake imeamua ‘kufunika’ kashfa inayozunguuka maafisa wa kampuni yao – BAE – kwa kutoa mlungula kwa maafisa wa serikali inayoziuzia zana za kijeshi (wakitaja, pamoja na rada ya Tanzania, Saudi Arabia na Afrika ya Kusini) huku Uingereza hiyo hiyo ikisisitiza ‘wapokeaji’ wa mlungula hapa nchini ndio wachukuliwe hatua za kisheria.

Hoja ya namna hii haina mashiko. Kwanza hakuna ushindani baina yetu na Uingereza katika masuala ya kupigana na ufisadi.

Pili, kufuatana na sheria zao, hatua za kisheria tayari zimechukuliwa dhidi ya BAE kwa kukubali ‘kosa’ na kutozwa faini ambapo kiasi cha fedha hizo irejeshewe serikali ya Tanzania kwa kulipishwa zaidi katika dili ya rada.

Matukio yote haya kamwe hayamwondolei Chenge ‘jinai’ ya tuhuma za kupokea rushwa chini ya sheria zetu nchini, ingawa kumekuwapo jitihada za kichinichini za kufanya hivyo kwa kutumia mwavuli wa ‘kukiri’ kwa BAE katika kashfa hiyo. 

Kuna usemi maarufu usemao ‘Historia hujirudia. Suala la taasisi kuu na nyeti ya serikali kutoa taarifa ‘rasmi’ lakini ya uongo, kwa lengo la kuupotosha limejirudia tena kwa namna ya kushangaza, hasa pale kurudia huko kunamgusa mtu ambaye alihusika moja kwa moja katika kutoa taarifa kama hiyo takriban miaka 16 iliyopita. Nitaeleza. 

Mtu mwingine aliyetajwa kupata mgawo wa mlungula wa kashfa ya rada ambayo inaitikisa nchi ni Dk Idris Rashid, aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuanzia serikali ya Awamu ya Pili ya Ali Hassan Mwinyi.

Dk. Idris alikuwa gumzo kubwa katika vyombo vya habari mapema mwaka 1994 kutokana na sakata la Benki ya Meridien BIAO iliyokuwa benki ya kwanza binafsi ya kigeni kuruhusiwa kufungua tawi nchini tangu benki za kigeni kutaifishwa miaka ya 1960.

Kumbe benki ile ilikuwa ya matapeli ikiongozwa na Andrew Sardanis, mzaliwa wa Cyprus ambaye baadaye alichukua uraia wa Zambia na ambaye alijihusisha na wakoloni wa Kiingereza waliokuwa wakitawala Rhodesia ya Kaskazini (sasa Zambia).

Makao makuu ya benki hiyo yalikuwa katika visiwa vya Bahamas lakini iliweza kufungua matawi katika nchi nyingi za Kiafrika katika mwisho wa miaka ya 80 na mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Kumbe ilikuwa namna ya kuhamisha mabilioni ya fedha za wateja kupeleka nje kwa kushirikiana na mamlaka husika. Benki hiyo ilianza kuporomoka huko Ghana, Gambia na Swaziland ambako wateja walianza kuzungushwa walipotaka kuchukua fedha zao.

Hatimaye hali hiyo ikaikumba Zambia na hapo ndipo wateja wa Tanzania walipoanza kwenda kuchukua pesa zao na kuzungushwa.

BoT iliibuka na kusambaza taarifa rasmi katika vyombo vya habari, liyosainiwea na Dk Rashid mwenyewe, kwamba Benki ya Meridien BIAO tawi la Tanzania lilikuwa imara, hivyo wateja wasihofu wala kuwa na sababu ya kukimbilia kwenda kuondoa fedha zao.

Kumbe hali ilikuwa kinyume, Meridien BIAO ilikuwa hoi ililazimika kufunga milango yake wiki moja baadaye kwa kukosa fedha za kulipa wateja wake. Wateja wengi walipoteza pesa zao.

Kenya na Zambia zilichukua hatua dhidi ya maafisa wao walioonekana kukiuka taratibu za kibenki na hata baadhi yao kushitakiwa. Huko Kenya maafisa kadha wa Benki Kuu ya nchi hiyo walifikishwa mahakamani kwa kusaidia Meridien BIAO kutorosha kwenda nje zaidi ya Sh 450 milioni za Kenya kutoka katika akaunti za wateja.

Hali kadhalika, Zambia maafisa kadha wa Benku Kuu walitiwa mbaroni kuhusiana na kosa kama hilo hilo, kutorosha zaidi ya dola za Kimarekani 90 milioni kwenda nje.

Hapa Tanzania, pamoja na taarifa ya uongo iliyotolewa na Gavana wa Benki Kuu hakuna afisa au mkuu yeyote wa serikali au BoT aliyewajibishwa kutokana na kuanguka kwa Meridien BIAO licha ya mamilioni ya wateja kutoroshwa pia.

Swali kubwa la kujiuliza hapa ni je muhula huu wa pili wa Kikwete bado utaendeleza tamthilia zake kuhusu malumbano baina ya viongozi wake wakuu kuhusu masuala ya ufisadi?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: