JK ameshindwa kunusuru chama chake


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 13 April 2011

Printer-friendly version
Rais Jakaya Kikwete

RAIS Jakaya Kikwete ameshindwa kukiokoa chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka katika tope la ufisadi. Kile alichoita, “CCM kujivua gamba, kimeishia kuchuna ngozi.”

Mikutano ya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (NEC) iliyomalizika mjini Dodoma, Jumatatu iliyopita, imeongeza ukubwa wa majeraha.

Imefanya kazi mbili: Kwanza, imezalisha makundi mapya na imestawisha yale ya zamani.

Maamuzi yaliyofikiwa ya kuivunja sekretarieti naKamati Kuu (CC) yanaonyesha kuwa mikutano hiyo iliyotarajiwa kujadili mambo ya msingi yanayokikabili chama hicho, imeishia kupeana posho, kunywa chai na kutupiana mipasho.

Maamuzi yaliyofikiwa ya kujiuzulu kwa CC yanaonyesha mambo mawili makubwa. Kwanza, inawezekana kweli kama inavyodaiwa na wapinzani, kuwa chama hicho kilishindwa katika uchaguzi mkuu uliopita.

Pili, wajumbe wa CC hawajui kuwa matatizo ya msingi ya chama chao ni udhaifu wa kiongozi wao mkuu – Rais Jakaya Kikwete na serikali yake. 

Akizungumza na waandishi wa habari Jumamosi usiku, aliyekuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Habari, Itikadi na Uenezi, John Chiligati alisema sababu kuu ya CC kujiuzulu ni kuchafuka kwa chama kutokana na tuhuma za ufisadi.

Lakini ni wazi sasa kwamba ndani ya CCM, tuhuma za ufisadi zimeshatapakaa kutoka kuwa tuhuma za mtu mmojammoja, hadi kuwa za chama kizima.

Kwa mfano, kwa miaka sita mfululizo, viongozi wakuu wa chama hicho wameshindwa kujinasua katika tuhuma za wizi wa mabilioni ya shilingi ndani ya Benki Kuu (BoT) kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).

Kwa miaka sita, CCM imeshindwa kukana kuwa haijawahi kutumia hata shilingi ya fedha zilizoibwa katika akaunti ya EPA kwenye kampeni zake za uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

Haijawahi kueleza saini za viongozi wake wakuu zilizopo kwenye baadhi ya nyaraka za wezi wa EPA ziliingiaje mikononi mwa watuhumiwa.

Zipo nyaraka zinazomuonyesha Salome Mbatia ambaye wakati wizi unafanyika alikuwa mshika fedha wa chama hicho akipewa sehemu ya fedha zilizoibwa kwa matumizi ya chama chake. Hili halijafafanuliwa.

Naye mwenyekiti wa chama hicho, Rais Kikwete hadi anavunja CC, ameshindwa kufanya mambo mawili. Kwanza, kukana madai ya wengi kuwa aliingia madarakani na fedha za wizi zilizokwapuliwa na kampuni ya Kagoda Agriculture Limited, inayohusishwa na swahiba wake mkuu, Rostam Aziz.

Pili, kujibu madai ya wapinzani wake, kwamba fedha nyingi zilizotumiwa na wanamtandao kuchafua baadhi ya viongozi wenzake katika chama kama vile, Fredrick Sumaye, John Malecela, Dk. Salim Ahmed Salim na Profesa Mark Mwandosya, zilikusanywa na kusambazwa na swahiba wake.

Pili, ni Kikwete na serikali yake walitoa msamaha wa jumla kwa wezi wa fedha hizo. Hadi CC inajiuzulu, haijawahi kusikika viongozi wake wakikemea wizi uliofanyika wala msamaha uliotolewa.

Wizi wa fedha za umma uliofanywa na makampuni ya Tangold Limited, Deep Green Finance Ltd., na Meremeta Limited, hauwezi kukinusuru chama hicho, iwapo Kikwete ataendelea na utamaduni wake huu wa kulinda anaowataka na kuwatosa asiowataka. 

Lakini si hivyo tu: Ni Kikwete na serikali yake waliomteua mtuhumiwa wa wizi wa fedha za EPA, Elisifa Ngowi aliyedaiwa kuwa ofisa wa usalama wa taifa, kuingia katika timu ya rais ya kutafuta wezi wa fedha hizo.

Katika wizi wa EPA, Ngowi anaonekana katika nyaraka za makampuni ya Clayton Marketing Limited na Excellent Services Ltd., iliyosajiliwa mwaka 1992.

Mbali na Ngowi wanahisa wengine wa makampuni hayo, ni Emily Samanya, Peter Sabas, Lecis Msiko na Massimo Feneli.

Katika mazingira hayo, tuhuma za EPA haziwezi kuishia kwa Rostam pekee. Hili ni donda ambalo limeitafuna serikali na chama chenyewe.

Uamuazi wowote wa kujivua gamba kwa njia hii, kutaweza kuondoka hadi ngozi yenyewe.

Nalo sakata la wizi wa fedha za Rada lililomfanya Andrew Chenge kuondolewa katika ujumbe wa CC, haliwezi kuvuliwa gamba na ngozi ikabaki salama.

Sababu ni kwamba ukiondoa rushwa ya dola za Marekani 1.5 milioni ambazo Chenge anatuhumiwa kupewa na kampuni ya Uingereza, BAE System, hakuna mahali ambapo CCM ilikemea serikali yake juu ya mradi huo feki. Kinachoonekana ni shinikizo la viongozi la kutaka rada inunuliwe.

Kazi kubwa ya kutaka ununuzi usifanyike ilifanywa na viongozi wa vyama vya upinzani, vyombo vya habari na asasi za kiraia. Sasa hicho kinachoitwa “kujivua gamba” kinatoka wapi?

Katika mkataba tata wa kufua umeme wa Richmond, Kikwete alikaidi kutekeleza maagizo ya Bunge yaliyotaka kuondoa katika nafasi zao baadhi ya watuhumiwa akiwamo mwanasheria mkuu wa serikali, Johnson Mwanyika na katibu mkuu wa nishati na madini, Athur Mwakapugi.

Wengine ambao Kikwete amelinda mpaka mwisho, nikamishina wa madini na nishati, Bashiri Mrindoko na mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Edward Hoseah.

Wakati Mwanyika na Mwakapugi walifanya kazi hadi kustaafu kwa heshima, Mrindoko na Hoseah bado wanaendelea na nyadhifa zao mpaka sasa.

Hivyo, pamoja na kutaka Edward Lowassa aondolewe katika nyadhifa zake ndani ya chama, ili kurejesha hadhi ya serikali na chama kilichopo ikulu, Kikwete alipaswa kuhakikisha watuhumiwa wote wanaondoka serikalini. Hakufanya hivyo.

Kimsingi pamoja na matatizo hayo, kufanya vibaya kwa CCM katika uchaguzi uliopita kumesababishwa na mambo mengi.  Kwanza, ni mfumo wa kupatikana wagombea ndani ya chama chenyewe.

Wengi waliopitishwa kuwania ubunge walishinda kwa mizengwe. Katika baadhi ya maeneo, mshindi alipatikana kwa kura chache ukilinganisha na zile walizopata washindani wake.

Kwa mfano, kuna baadhi ya majimbo kati ya wapiga kura 10,000 waliojitokeza, mshindi alipata kura 2,500. Zaidi ya asilimia 75 ya kura zilimkataa.

Lakini kwa kuwa uchaguzi wa kura za maoni ulibeba lundo la wagombea, baada ya mgombea “aliyeshinda” kupitishwa na kutokana na muda kuwa mdogo, mengi ya makundi ya uchaguzi yalishindwa kuvunjwa.

Pili, mtaji mkuu wa CCM katika uchaguzi ni mabalozi wa mashina. Katika uchaguzi uliopita, kuna madai kuwa mabalozi hawakuwezeshwa.Fedha nyingi ziliwekezwa katika kampeni za Kikwete.

Tatu, baadhi ya wagombea walitumia jina la ikulu na rais na kudai kuwa wamejitosa katika kinyang’anyiro kwa kuwa walitumwa na Kikwete.

Hata hivyo, wananchi walipowagundua waliwakataa. Miongoni mwa waliopitishwa lakini wananchi wakagoma kuwachagua, ni Ramadhani Madabida ambaye aligombea ubunge katika jimbo la Kilwa Kusini.

Alishindwa katika kura za maoni. NEC ilirejesha jina lake. Hatimaye jimbo la Kilwa Kusini likaangukia kwa Chama cha Wananchi (CUF).

Ni magamba yapi yamevuliwa?Yaliyobaki yatavuliwa lini?

0
Your rating: None Average: 3.3 (3 votes)
Soma zaidi kuhusu: