JK anaweza kusema bado ana serikali?


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 25 April 2012

Printer-friendly version

WIKI iliyopita nilijadili kwa kina suala la uhalali wa serikali ya awamu ya nne. Nilijikita zaidi kuelezea jinsi ilivyoshindwa kukomesha ufisadi unaonuka kila kona.

Nilitoa mfano wa kushindwa kwa serikali hiyo kwa kujadili utendaji wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda. Nilisema kuwa Pinda ni mfano mmojawapo wa aina ya watu wanaoacha kuchukua hatua kwa sababu ya ama woga au matarajio ya baadaye ya kisiasa ambayo leo hayako wazi sana.

Nilikumbusha mambo mawili tu kuhusu maamuzi ya waziri mkuu juu ya serikali kupunguza matumizi. Pinda alipiga marufuku ununuzi wa magari ya kifahari maarufu kama mashangningi hadi kwa kibali maalum. Niliuliza ni kwa kiwango gani agizo hilo limetekelezwa?

Hata hivyo, ukweli wa jambo hilo ni kwamba leo hii serikali inamiliki mashangingi makubwa makubwa kuliko ilivyokuwa kabla ya Pinda kutoa agizo lake.

Pia nilizungumzia suala la semina. Pinda alipiga marufu semina na makongamano ya kila wakati ya watumishi wa serikali. Ni miaka minne sasa tangu Pinda achukue maamuzi hayo, nilijiuliza wiki iliyopita, je, semina na makongamano yamepungua kwa kiasi gani?

Je, uwajibikaji ndani ya serikali umeongezeka zaidi baada ya katazo hilo la waziri mkuu? Nilisema jibu ni jepesi tu, kila siku iendayo kwa Mungu sasa semina na mikutano ya kikazi nje ya ofisi za umma vimekuwa  fasheni, na vinaigharimu serikali sana.

Ingawa uchambuzi wangu ulikuwa umegusa kwa kiasi kidogo tu ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa fedha wa 2010/11 ikionyesha hali ya usimamizi wa matumizi ilivyo mbaya serikalini, ripoti za kamati za kudumu za Bunge, Hesabu Mashirika ya Umma (POAC), Hesabu za Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) zilizotolewa wiki iliyopita, zimenisaidia kuonyesha nilichokusudia kusema.

Wabunge wametaharuki na wamekwenda mbali kiasi cha kukitafuta kichwa cha Pinda sasa. Wabunge mbali ya kuwashupalia mawaziri kwa utendaji wa ovyo kabisa, wameanza jaribio la kutaka kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu Pinda.

Nilipata kusema huko nyuma kuwa kosa kubwa analofanya Pinda ni kuiga staili ya utendaji ya bosi wake. Anachofanya Rais Jakaya Kikwete kwa mapana yake hakina tofauti sana na anachofanya Pinda, wanafanana katika uwajibikaji.

Hawa wameamua kuchagua staili ya kutokuchua hatua, kauli na maneno mengi, lakini shida za wananchi zinabaki pale pale.

Sote tunakumbuka Rais Kikwete alikwisha kusema mara kadhaa kuwa anawafahamu wala rushwa, isipokuwa aliwapa muda wa kujirekebisha. Hii siyo kauli aliyoitoa mafichoni, ilikuwa hadharani.

Lakini pia Rais Kikwete kama alivyo Pinda wamekuwa wanasoma ripoti za CAG mwaka baada ya mwaka, wamejionea wenyewe mabilioni ya fedha zinazotafunwa na watumishi wa umma. Wamejionea jinsi wananchi wanavyopata tabu kutokana na kukosekana kwa huduma muhimu za kijamii, lakini watumishi wa umma wakiwamo mawaziri wakielea kwenye ukwasi wa fedha za walipakodi zilizolenga kuwapelekea maendeleo.

Haya yote yanajulikana kwa Rais, na kwa Waziri Mkuu Pinda ni zaidi. Pinda amesimamia TAMISEMI kwanza kama Naibu Waziri, lakini pia kama Waziri chini ya Ofisi ya Waziri mkuu, amesikia na kushuhudia ulaji wa kutisha ndani ya halmashauri.

Pinda amekabidhiwa na kusoma ripoti za CAG na ile ya LAAC kama kiongozi mwenye wajibu wa kuchukua hatua tangu alipoteuliwa Naibu Waziri mwaka 2000. Anaijua TAMISEMI ndani nje.

Kwa hiyo, kama ni mtu wa kumpa Rais Kikwete taarifa za ulaji ndani ya halmashauri, na kama ni mtu wa kujua waliko wezi wa fedha za umma, hakika hakuna kama Pinda.

Lakini pamoja na kujua yote haya, Pinda aliamua kufanya jambo moja, kumtazama bosi wake anaelekea wapi, basi akaamua kuelekea huko huko – hakuna kuchukua hatua. Acha watu watafune kodi za wananchi; acha barabara zijengwe chini ya kiwango; acha wananchi waachwe njia panda na viongozi wao wanaotamba na kurandaranda huko na huko kwa mikogo ya magari ya kodi za wananchi – Pinda kama bosi wao, kimya. Hakuna kumwajibisha mtu kama bosi wake.

Kwa hali hii ya utendaji wa Pinda, ningeshangaa sana kama angelimaliza kipindi chake cha uwaziri mkuu hadi Oktoba 2015 bila kukutwa na hii aibu inayomwandama sasa, jaribio la kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye.

Pinda alipaswa kujua kuwa katika mfumo wa kiutawala wa nchi hii, ni vigumu mno kumpigia kura ya kutokuwa na imani na Rais. Sababu zake ni nyingi, kwanza masharti ya kikatiba ni magumu kutimizwa. Ibara ya 46A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inaweka utaratibu wa kimpigia kura ya kutokuwa na imani rais.

Makosa ambayo yanaanishwa kweye ibara ya 46A (2) kuanzia (a) hadi (c)  ni kutenda vitendo vinavyovunja katiba na maadili ya viongozi wa umma; vitendo vinavyokiuka maadili ya uandikishwaji wa vyama vya siasa kama kuanzisha vyama kwa  misingi ya udini, kuendesha chama cha siasa upande mmoja wa Jamhuri; kwamba rais amekuwa na mwenendo unaodhalilisha kiti cha urais, hata hivyo, haitatolewa hoja namna hiyo ndani ya miezi 12 tangu itolewe kwake na kukataliwa na Bunge.

Lakini ugumu mwingine wa kumshitaki rais unafafanuliwa kwa mashari ya ibara ndogo ya (2) ya ibara ya 46A kuwa ni kuandikwa kwa kusudio hilo siku 30 kabla ya mkutano wa Bunge unaolengwa kuwasilishwa, lakini ikiambatana na saini za wabunge asilimia 20; kusudio hilo lazima lifafanue makosa aliyotenda Rais na kutaka kuundwa Kamati Maalum ya Uchunguzi dhidi ya makosa ya rais.

Spika anatakiwa akishapokea taarifa iliyotiwa saini na kujiridhisha aruhusu iwasilishwe bungeni na kisha atawahoji wabunge bila kuijadili, na itabidi ipitishwe na theluthi mbili ya wabunge wote. Utaratibu ni mrefu, nimetoa haya kwa ufupi tu.

Katika utaratibu huo, akili ya kawaida kabisa ingekuonyesha kuwa kwa mfumo wa Tanzania hata kama rais akiamua tu kuchapa usingizi bila kufanya lolote, kwa kuwa ana wateule lukuki aliowateua huko na huko, wakiwamo wabunge, mawaziri na waziri mkuu, bila kutaja wana usalama ambao wana uwezo wa kuhujumu mchakato huo, ni vigumu sana kumwajisha. Katiba ya Tanzania inatengeneza rais mfalme kama siyo rais mungu mtu.

Kwa hiyo, wale wote waliokabidhiwa vibarua vya kumsaidia, kama Pinda na mawaziri wengine kama walikuwa na sababu ya kusumbua akili zao, wangegundua kuwa wamekalia kuti kavu zaidi kuliko huyo aliyewateua, na kwa hali hiyo wangewajibika kwa nguvu zaidi kwa maana mbili kuu, moja kumridhisha huyo aliyewateua na hata kuwafurahisha wananchi ambao ndiyo waajiri wakuu.

Lakini la pili, ni kumsaidia huyo aliyewateua asifike mahali serikali yake kwa ujumla ikaonekana kuwa imeshindwa kwani kama akiandamwa nao watakuwa wanaandamwa. Kwa hali hiyo uwajibikaji wao unakuwa na nguvu mbili, kuwanusuru wao wenyewe na kumnusuru bosi wao.

Hata hivyo, kwa hali ilivyo sasa, sijui kama baada ya mkutano wa saba wa Bunge la 10 uliomalizika Jumatatu wiki hii, Waziri Mkuu Pinda na wale mawaziri walioandamwa kwa udhaifu mkubwa watakuwa na sura gani wawapo katika ofisi zao. Sijui kama bado wanajiona wako sawa.

Mwisho ni kwa Rais Kikwete, katika mazingira ya mawaziri wake wanane kuandamwa kiasi hiki, katika jaribio la kumpigia kura ya kutokuwa imani Waziri Mkuu wake haoni kuwa jaribio hilo ni dhidi ya serikali yake?

Kwamba kinachotishwa ni serikali yake na siyo waziri mmoja mmoja, je, serikali hiyo kwa maana ya baraza la mawaziri bado inaweza kubakia ilivyo  hadi kumfikisha mwisho wa utawala wake Oktoba 2015?  Kikwete anapashwa kuwaza zaidi katika mazingira haya, kwa kuwa serikali yake sasa inapita katika majaribu makubwa na mazito.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: