JK angalia boriti jichoni mwako ndipo...


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 06 October 2009

Printer-friendly version

NDANI ya mkutano wa Umoja wa Mataifa mjini New York, Rais Jakaya Kikwete analia mbele ya Jumuiya ya Kimataifa akitaka iunge mkono msimamo wa Umoja wa Afrika (AU) wa kupinga utawala uliojiweka madarakani kwa kuiba kura na uliopindua serikali halali.

Kikwete, rais wa pili Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu iruhusu mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, anataka mataifa tajiri au nchi zilizoendelea – ambazo kwa maoni yangu ndiyo waundaji wa hicho kiitwacho jumuiya ya kimataifa – yachukue msimamo kama wa Umoja wa Afrika inapopinga mapinduzi.

Kwamba, pale AU inapokataa kutambua na kushirikiana kidiplomasia na serikali isiyochaguliwa na wananchi, basi mataifa hayo nayo yafuate kwa kukata uhusiano na nchi hiyo husika.

Rais Kikwete amepeleka salamu muhimu kwa ulimwengu juu ya haja iliopo kwa Waafrika kufuata mkondo wa demokrasia ya kweli kwa kuanzia na kuhakikisha kuwa wanaendesha uchaguzi huru na wa haki katika nchi zao.

Maana, serikali iliyopata ridhaa ya watu ni ile tu iliyotokana na uchaguzi uliofanyika katika misingi ya haki, uhuru na uwazi.

Katika mfumo wa uchaguzi unaokidhi viwango, kila aliyestahili kushiriki awe amepewa nafasi; tena ameipata nafasi hiyo kwa uhuru – ikiwa na maana hakutishwa kwa namna yoyote ile katika kuipata haki yake; na isitoshe wakati wa mchakato wa uchaguzi utendaji au usimamizi wa kupatikana haki hiyo kwa raia ulitekelezwa kwa uwazi.

Kilio cha rais Kikwete ni kikubwa. Na amekitoa katika wakati muafaka. Ipo mifano hai ya namna nchi za Afrika zilivyojikuta katika uongozi usiokuwa na ridhaa ya watu wake na Umoja wa Afrika ukachukua msimamo wa kutotambua serikali hizo.

Angalia Guinea na Mauritania, nchi za Afrika Magharibi, ambazo hadi sasa zinaendelea na utawala uliopatikana kwa mapinduzi. Lakini zipo nchi kadhaa ambazo kumetokea migogoro kutokana na madai ya serikali kuvuruga uchaguzi kwa nia ya kung’ang’ania madaraka.

Haya yanaonekana Gabon na Madagascar ambako wametokea wanaharakati walioongoza upinzani dhidi ya tawala zilizo madarakani baada ya kuonekana zilishindwa uchaguzi.

Lakini Kikwete anapiga mbiu hiyo wakati taifa analoliongoza, Tanzania, linakabiliwa na uchaguzi wa serikali za mitaa, vitongoji na vijiji na uchaguzi mkuu wa serikali kuu kwa maana ya rais, bunge na madiwani.

Tanzania ilitokana na muungano wa nchi mbili: Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar; zilizounganishwa 26 Aprili 1964 na kuzaliwa kiitwacho tangu hapo, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Nchi zote ziliwahi kufanya uchaguzi wa vyama vingi kabla ya kuunganishwa. Na baada ya muungano, na uongozi uliporuhusu mfumo huo unaojumuisha siasa za ushindani, kupitia bunge, ilitungwa sheria ya kuifanya siasa ni jambo la muungano.

Lakini bado Zanzibar ina uchaguzi wake wa kupata rais, wajumbe wa kuingia Baraza la Wawakilishi na madiwani. Tanzania inaendesha uchaguzi wa rais, wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano na madiwani wanaotumia mabaraza ya madiwani upande wa Tanzania Bara.

Pande zote za muungano zilifanya uchaguzi wa kwanza mwaka 1995. Chama cha Mapinduzi (CCM), ambacho kilimteua Kikwete kugombea urais mwaka 2005 na kumkabidhi uenyekiti mwaka 2007, kinaendelea kushika hatamu ya uongozi wa Tanzania kwa wagombea wake wa urais Muungano na Zanzibar kutangazwa washindi wa uchaguzi.

Hata hivyo, kumekuwa na malalamiko Zanzibar kwamba mara zote uchaguzi wake umevurugwa katika namna ya kusaidia CCM kubaki madarakani. Ndio kusema mkondo wa demokrasia Tanzania umepata mushkeli mara zote kutokana na yanayotendeka Zanzibar.

Mwaka 1995 ilielezwa matokeo ya CCM kushindwa urais Zanzibar yalibadilishwa mezani na chama hicho kutangazwa mshindi. Mwaka 2000 kadhalika mgombea wa CCM alipewa ushindi baada hila iliyofanywa na dola ikiitumia Tume ya Uchaguzi (ZEC) na hila zikaendelea mwaka 2005.

Uthibitisho wa malalamiko hayo ni mgogoro wa kisiasa unaozidi kukua Zanzibar kwa vile upinzani unaoongozwa na Chama cha Wananchi (CUF) unaendelea kukataa matokeo yanayotangazwa na tume hiyo.

Ni kwa bahati mbaya, inaonekana mgogoro huu hausumbui vichwa vya wanasiasa wa CCM. Sababu yaweza kuwa moja tu: unakiendelezea utawala wa dola. Hawa wamefanya siasa ndio ajira ya maisha kwao kiasi cha kujijengea uhalali wa kutawala daima.

Ni kwa bahati mbaya zaidi kwamba Rais Kikwete mwenyewe ambaye alitamka hadharani 30 Desemba 2005 alipohutubia bunge jipya baada ya uchaguzi mkuu, akiwa amechaguliwa rais, ameshindwa kutimiza ahadi yake ya kuutafutia mgogoro huo ufumbuzi wa kudumu.

Matamshi yake ya hivi karibuni kuwa hayajachoka na jitihada zake, hayana mashiko yoyote hasa kwa kutazama mizengwe inayofanywa katika zoezi la uandikishaji wapiga kura na malalamiko ya watu wengi kunyimwa haki hiyo kwa visingizio mbalimbali vikiwemo vya kisheria.

Katika kinachoaminika kuwa ni kusaidia chama chake, Rais Kikwete hajachukua hatua ya kuhakikishia kila mwenye haki anaandikishwa badala yake wananchi wanaona namna anavyoachia vikosi vya ulinzi anavyosimamia, likiwemo Jeshi la Polisi na Usalama wa Taifa, vitumike kutisha wanaodai haki hiyo.

Serikali ya Mapinduzi inayoongozwa na CCM imepitisha sheria inayoshurutisha mwananchi kupata kwanza kitambulisho cha ukaazi ndipo aandikishwe. Sheria hiyo ililalamikiwa kuwa inabagua wengi kwani kitambulisho chenyewe kinatolewa kibaguzi huku baadhi ya wanaoonekana si wafuasi wa CCM wakiwekwa kando.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa Zanzibar wanakisia watu wapatao 170,000 watabaki nje ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK) la Zanzibar na hivyo kukosa haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi watakao. Wapi uchaguzi huru na wa haki kama wananchi wanakatwa pande wasishiriki?

Sasa ni mchango gani Rais Kikwete ametoa kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki Zanzibar? Na iwapo haupo kama inavyoonekana, anathubutu vipi kusimama jukwaa la kimataifa anapokuwa nje ya nchi, kuchukia serikali zinazojiweka madarakani kwa mabavu? Bado anaamini serikali inayokuja Zanzibar itachaguliwa na watu iwapo tayari vitisho na husda vinashamiri katika uandikishaji wapiga kura?

Lakini mbaya zaidi ni kwa namna gani ataepusha nchi anayoiongoza kufuata yaliyotokea Kenya na Zimbabwe ambako maelfu ya Waafrika wameuawa kwa mkono wa dola katika harakati za kudai haki ya kuchagua viongozi wawatakao?

Ni katika hali hiyo Wazanzibari wa Mji Mkongwe, wanauliza “Kwanini Wazanzibari tunaendelea na mateso kila unapofika uchaguzi. Why?” Na wahenga wamesema “Toa boriti jichoni mwako ndipo uoneshe kibanzi jichoni kwa mwenzako.”

Binafsi najiuliza, “Ni lini hasa sauti za Wazanzibari kupitia visanduku vya kura zitaheshimiwa na CCM?”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: