JK atapata wapi ‘watakatifu’ wapya?


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 25 April 2012

Printer-friendly version

RAIS Jakaya Kikwete anakabiliwa na mtihani mgumu. Ana jukumu zito la kuchekecha upya miongoni mwa wabunge wa CCM kupata “watakatifu” wapya.

Hii ni baada ya “watakatifu” wake wa awali kutikiswa. Wametuhumiwa kwa wizi, ubadhirifu na kushindwa kutekeleza majukumu yao. Kwa maneno machache wameonekana wanamwangusha aliyewateua.

Rais Kikwete alipochekecha miongoni mwa wabunge wa chama chake baada ya uchaguzi wa mwaka 2010, alipata wateule wake takriban 47. Bila shaka aliona wengine hawatoshi kuvaa viatu vya uwaziri, hadi akaamua kuchukua kwenye akiba yake.

Ili kuziba pengo la “watakatifu” lililojitokeza, Rais Kikwete kwenye mkoba wake wa pembeni aliwateua Profesa Makame Mbarawa na Shamsi Vuai Nahodha kuwa wabunge, ili kujazia baraza lake.

Hizi zilikuwa dalili tosha kuwa kwenye kapu la wabunge wa kuchaguliwa na viti maalum, “watakatifu” walikuwa wamekwisha hadi akachukua nje ya bunge. Hii si mbaya, kwa kuwa katiba inamruhusu kufanya hivyo.

Sasa kibao kimegeuka. Wale aliowaona “watakatifu” wakati ule wamechafuka. Wamejaa tuhuma na baadhi yao wametajwa hadi bungeni kuwa ni wezi. Wananchi hawawaamini tena. Wabunge wenzao wamewakataa, wanawalazimisha wajiuzulu, si hivyo bosi wao, Waziri Mkuu Mizengo Pinda aachie ngazi.

Mawaziri wanaotuhumiwa ni Mustafa Mkulo (Fedha), Cyril Chami (Viwanda na Biashara), William Ngeleja (Nishati na Madini), Omar Nundu (Uchukuzi), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), George Mkuchika (Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEAMI), Profesa  Jumanne (Kilimo Chakula na Ushirika) na Dk Hadji Mponda (Afya).

Tuhuma dhidi ya mawaziri hawa zimeibuliwa katika ripoti za kamati za kudumu za bunge za Hesabu za Serikali Kuu (PAC), Serikali za Mitaa (LAAC), na Mashirika ya Umma (POAC) zilizotokana na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Baada ya dalili kuonekana kuwa mawaziri wanaotuhumiwa wasingejiuzulu, hata baada ya wenzao wa CCM kuwashinikiza, umeandaliwa mkakati mbadala wa kuwalazimisha – kupiga kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu.

Tayari hoja imewasilishwa bungeni, ikiungwa mkono na saini za wabunge zaidi ya 70, kutaka ipigwe kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu.

Kura hiyo ikipigwa, na zaidi ya nusu ya wabunge wakaiafiki, rais anaarifiwa na waziri mkuu anaachia ngazi.

Waziri mkuu kuachia ngazi si kazi ndogo wala si mchezo. Ni jambo linalomaanisha kwamba Baraza la Mawaziri linakuwa limevunjwa. Kwa maneno mengine, serikali inakuwa imeanguka, isipokuwa rais peke yake.

Wabunge wamefikia hatua hiyo baada ya kuona hakuna dalili za mawaziri hao kujiuzulu. Wameamua kuwashinikiza wafanye hivyo, au wajikute wako nje ya baraza, baada ya waziri mkuu kuenguliwa.

Pamoja na tuhuma dhidi yao sasa, Rais Kikwete aliona hawa ndio “watakatifu” wake miongoni mwa wengi. Inawezekana alifanya kazi hii mwenyewe, akachambua nani awemo na yupi asiwemo. Au alisaidiwa na vyombo vya dola vya kuchuja wateule wake.

Mawaziri hawa wameshutumiwa waziwazi ndani na nje ya bunge. Wachache kati yao wamejitetea na wengine wamekaa kimya.

Pengine hii ndiyo sababu Rais Kikwete amevuta subira akiwa safarini Brazil na baadaye Malawi, ili apate fursa ya kuchambua ili kubaini pumba ipi na mchele ni upi. Labda anachekecha kichwa kwanza, kuona ni wapi atapata “watakatifu” wapya ndani ya muda mfupi wa serikali.

Itakumbukwa hata katika kipindi chake cha kwanza, alilazimika kuunda upya serikali baada ya kujiuzulu waziri wake mkuu wa kwanza, Edward Lowassa na mawaziri wawili wengine kutokana na kashfa ya kushinikiza mkataba wa ukodishaji wa mitambo ya kufua umeme wa dharura kwa kampuni ya Richmond.

Mawaziri waliojiuzulu pamoja naye ni Dk. Ibrahim Msabaha wa Afrika Mashariki na Nazir Karamagi wa Nishati na Madini.

Haiingii akilini kuona hata kabla ya miaka miwili kupita “watakatifu” wa Kikwete wanafunikwa na uchafu usiosafishika. Miaka miwili ni kipindi kifupi kwa kiongozi msafi kubadilika na kuwa mchafu, hasa kama kuna usimamizi makini juu yake.

Kama tuhuma dhidi ya mawaziri hawa ni za kweli, ninashawishika kuamini kwamba wateule hawa huenda walikuwa wachafu hata kabla ya kuteuliwa au itakuwa usimamizi uliopo juu yao ni legelege unaotoa mwanya kwao kuchafuka haraka.

Lakini pia, kama mawaziri hawa waliteuliwa wakiwa wachafu, napata mashaka kama nchi yetu ina vyombo makini vya kuchunguza watu na kubaini uwezo na udhaifu wao kabla ya kupendekezwa kwa rais wateliwe, hasahasa kwenye nafasi nyeti kama uwaziri.

Wasiwasi wangu ni iwapo Rais Kikwete akichekecha tena kwenye “makapi” aliyoyaacha wakati ule, atapata watu wa namna gani, ikiwa “watakatifu” walimalizika mwaka 2010.

Ni rais kusema ohoo bado wabunge kibao, au ukasema Watanzania ni wengi hadi milioni 45. Lakini nani asiyejua kuwa wananchi kwa sasa hawana imani na serikali yake karibu yote?

Nani asiyejua kuwa wabunge waliopo pia hawaaminiki kwa wananchi waliowachagua? Nani asiyesikia kuwa wabunge wengi ni wala rushwa na wengine walitoa rushwa ili wachaguliwe?

Au nani asiyejua kuwa wabunge wengi walifadhiliwa na matajiri wachafu ili kupata nyadhifa walizonazo? Hivi ni nani asiyejua kuwa mtu yeyote aliyetoa rushwa kupata ubunge, akipata nafasi ya madaraka kipaumbele chake ni kurejesha fedha za waliomwingiza madarakani?

Tukio la karibuni la rushwa iliyokithiri kwa wabunge wakati wa mchakato wa kuwania ubunge wa Afrika Mashariki na mwaka jana wakati wa sakata la aliyekuwa Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, David Jairo la kutuhumiwa kuhonga wabunge ili wapitishe bajeti ya wizara hiyo, ni mifano michache ya uchafu wa wabunge.

Kutokana na uchafu huo, hapana shaka ni kazi ngumu kwa Rais Kikwete kupata “watakatifu” wapya. Kitakachosaidia, ni “mkoba” wake aliopewa na katiba, ambao bado una nafasi saba za kuteua wabunge.

Kwa mujibu wa katiba, Ibara ya 66 (1) (e), Rais Kikwete anazo nafasi 10 za kuteua wabunge. Ametumia tatu kwa kuwateua Nahodha, Profesa Mbarawa na Zakia Meghji.

Bila shaka atalazimika kuingia kwenye mkoba huo kutafuta Watanzania wengine wenye uwezo ili awateue kuwa wabunge na baadaye mawaziri, vinginevyo itakuwa vigumu kwake kupata “watakatifu” wapya.

0788 346175
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: