JK bingwa wa kufanya kinyume


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 01 September 2010

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

NAWASHUKURU wapenzi wasomaji wa safu hii kwa maoni yao. Baadhi walinipigia simu na wengine, kama ilivyo ada, walinitumia ujumbe mfupi wa simu.

Wapo walinikosoa kwa namna nilivyochanganya majina ya Patrick Qorro, nikimtaja kama ndiye Matheo Qares, ambaye aliangushwa na Dk. Willibrod Slaa katika uteuzi wa wagombea ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 1995.

Naomba radhi wasomaji na hasa mwenyewe Qares kwa usumbufu waliopata kutokana na kasoro hiyo ya kibinadamu.

Maudhui niliyoyakusudia katika makala husika iliyokwenda kwa kichwa cha habari, “Hata Kikwete angehamia CHADEMA” yamebaki palepale.

Kikwete hakuhama. Alibaki CCM alikoamua kuunda mtandao mzito uliojaa wafanyabiashara na wapigadebe. Akawapiga kumbo wapinzani wake katika chama na kuwashinda wagombea wa upinzani – akawa rais.

Inawezekana alichotaka kukifanya katika uongozi wake hakukijua na hakujua watu stahiki aliotaka wamsaidie.

Alimteua Johnson Mwanyika kuwa mwanasheria mkuu na akamteua Edward Lowassa kuwa waziri mkuu.

Hao ndio waliokuja kuwa fungamano kuu katika kashfa na shutuma nyingi za ufisadi ikiwemo kubwa ya Richmond.

Ikumbukwe kuwa moja ya sababu zilizochangia Kikwete kukosa nafasi ya kwanza katika duru ya pili mwaka 1995 ni fungamano lake na Lowassa.

Kabla ya wajumbe kupiga kura, wagombea walipewa nafasi ya kujieleza na Kikwete alitoa hotuba inayodaiwa ilikuwa na msisismko mkubwa.

Akasema pia akijaaliwa kuwa rais, atafanya kazi bega kwa bega na swahiba wake, Lowassa, ambaye alikataliwa na NEC wakati wa mchakato wa kutafuta wagombea. Inadaiwa kauli hiyo ndiyo ilimgharimu.

Katika mahojiano na waandishi wa habari baada ya mchakato wa kumpata mgombea anayefaa kutokana na wana-CCM 14 walioomba, na hasa 11 waliopita mchujo, Mwalimu Julius Nyerere alisema aliweka veto dhidi ya Lowassa akisema mwanasiasa huyo kijana hakuwa na sifa.

Hadithi ya wahenga – asiyesikia la mkuu huvunjika guu. Miaka 10 baadaye, 2005, au miaka sita baada ya ‘mwenye nchi kufariki dunia’, eti Kikwete akiwa rais akapuuza maoni yake na kumsogeza Lowassa kileleni. Kilichotokea sote tunakijua.

Ndiyo maana Dk. Slaa alipotaja orodha ya watu 11 aliowaita watafuna nchi, wawili hao walikuwemo. Na ilipoibuka kashfa nzito ya utata wa uidhinishaji mkataba wa kufua umeme wa dharura kwa kampuni ya Richmond, ofisi ya Mwanyika, Ikulu na Waziri Mkuu, wakatiwa ‘hatiani’.

Rais Kikwete ndiye mwenyekiti wa vikao vya Baraza la Mawaziri. Alijua ukiukwaji wa taratibu za kumpata mzabuni ila alinyamazia hadi kuteuliwa kampuni ya Richmond ambayo haikuwa na sifa.

Bunge lililoshupalia suala hilo likataja watu kadhaa wa kuadhibiwa. Hao wakatajwa, lakini rais aligoma maana ni “wenzake.” Akamwachia Mwanyika astaafu na akaridhia Lowassa ajiuzulu tu uwaziri mkuu. ‘Soo’ ya ufisadi huo ikafichwa peupe.

Japokuwa Nazir Karamagi (aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini), na Dk. Ibrahim Msabaha (mtangulizi wake wizarani), aliyekuwa Waziri wa Afrika Mashariki, walijiuzulu kutokana na kashfa hiyo, Karamagi alilindwa pia na Bunge na Serikali ya Kikwete alipokurupuka na nyaraka kwenda kutia saini mkataba wa uchimbaji madini Buzwagi.

Haikutosha. Kikwete aliamuru mawaziri waende mikoani kutetea bajeti iliyolalamikiwa na wananchi. Umma ukashuhudia walivyozomewa kila walikoenda.

Ndiyo maana, wiki moja tangu Rais Kikwete aanze kampeni za kutaka kurudi tena Ikulu, huku wapinzani wakisaka pesa za kufika mikoani, anateswa na dhambi ya ahadi.

Aliahidi kupambana na mafisadi, amewalea na aliahidi kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania, maisha ni duni kwao.

Mei alikataa katakata kuwaongezea wafanyakazi kima cha chini cha mshahara, lakini kabla tu ya kampeni ya 2010, aliichomokea nyongeza kimyakimya.

Aliahidi kupunguza gharama za umeme, lakini bei inapaa na tayari wataalamu wanaonya haitashuka; aliahidi ujenzi wa barabara, lakini amemalizia tu miradi iliyoanzishwa na serikali ya awamu ya tatu.

Aliahidi ‘kuua’ mchwa wanaotafuna pesa za umma kwenye halmashauri, lakini hakupuliza dudu killer badala yake amepuliza manukato. Sasa ni mlima.

Naona Rais ahadi zimemshinda. Amebaki sasa bingwa wa kufanya kinyume chake. Twafa!

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: