JK hana uwezo, ujasiri na mbinu kuiokoa CCM


Hilal K. Sued's picture

Na Hilal K. Sued - Imechapwa 15 December 2010

Printer-friendly version

UCHAGUZI mkuu uliopita unasahaulika polepole. Lakini kama ilivyo ada, mwisho wa uchaguzi mmoja ndiyo mwanzo wa uchaguzi mwingine.

Kwa upande wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mwaka 2015 utakuwa ni mtihani mkubwa katika kumpata mgombea wake wa urais.

Hisia za wengi ni kwamba mchakato ndani ya chama hicho utakuwa na mvutano zaidi, ukiambatana na rafu nyingi kuliko ilivyokuwa 2005.

Pamoja na mgombea wake wa urais, Jakaya Kikwete, kupata ushindi uchaguzi wa 2010, ni dhahiri amepata shida sana licha ya ukweli kwamba chama kilifanya kampeni ya nguvu kubwa na wakutumia fedha nyingi zaidi kuliko huko nyuma.

Bado, matokeo ya mwisho yaliongezea upinzani viti vya ubunge maradufu kwa wapinzani. Kambi hiyo ilikosa viti saba tu kufikia idadi ambayo ingeinyima CCM faida ya theluthi mbili ya kura bungeni ya kupitisha watakacho.

Ni matokeo yanayoipa CCM changamoto kubwa pamoja na kiongozi wake mkuu, Rais Jakaya Kikwete katika kuhakikisha inabaki madarakani 2015.

Yeye ndiye awezaye kutoa mwongozo katika kupatikana mgombea thabiti.

Changamoto kubwa zaidi kwake ni hali itakavyokuwa katika serikali hasa kwa matokeo yaliyoingiza wabunge hodari, makini na wazungumzaji wazuri wa masuala ya kitaifa kwa kambi ya upinzani.

Kwamba safari hii Bunge litawaka moto si kitu cha kufikirika. Bunge la Kumi linatarajiwa kuonyesha kwamba lile la tisa lilikuwa maskhara.

Watu wengi wanadhani kwa kuwa anamaliza miaka mitano ya mwisho, basi hakutatokea mabadiliko yoyote makubwa na yanayoweza kushawishi wananchi kuwa na imani na CCM hadi uchaguzi ujao.

Bado mafisadi na wapambe wake wanaonekana kukiongoza chama hicho – tena kwa pua. Hivyo upinzani Bungeni unaweza kuwarahisishia wananchi katika kupoteza imani hiyo.

Pamoja na hali inayoonekana ya kujitahidi kuutenga mtandao wake uliomwingiza madarakani 2005 na ambao katika muhula wa kwanza umeishia kutuhumiwa sana kwa ufisadi, bado kutatokea mivurugano katika mchakato wa kutafuta mgombea ajaye.

Hata hivyo mambo mawili huenda yakaepusha mivurugano hiyo iwapo yatafanywa kwa dhati na umakini:

Kwanza, ingawa ni utaratibu tu kimazoea, siyo kanuni iliyoandikwa, ni kutambua kuwa ni wakati muafaka kwa Zanzibar kutoa mgombea baada miaka 20 ya upande wa Bara kuteuliwa.

Pili, ni kuingiza hoja ya jinsia – kwamba imefika wakati wa kupata rais mwanamke. Ili mojawapo lipite, kuna umuhimu wa kujenga hoja iliyoshiba katika vikao vya juu vya chama na maamuzi yafanyike mapema.

Bahati mbaya ni minyumbuliko hii miwili inaweza isitokee kutokana na ukweli kuwa hakuna wagombea wanaofaa.

Kuhusu la kwanza – kuna minong’ono kuwa kuteuliwa kwa aliyekuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha, kuwa waziri wa mambo ya ndani, inatajwa kuwa ni maandalizi ya kutafuta mgombea 2015.

Nasita sana kufikiria hilo kutokea kwani pamoja na kukubalika kwake Zanzibar, Nahodha hana umaarufu Bara, ingawa anaonekana ni kiongozi msafi.

Ni vigumu kumfikiria akifanya kampeni kali majukwaani dhidi ya mtu kama Dk. Willibrod Slaa, kwa mfano, (ambaye dalili nyingi zinaonyesha atagombea tena).

Mwaka 2005 CCM ilikuwa na mgombea mzuri kutoka Zanzibar, Dk. Salim Ahmed Salim. Hakupitishwa na vikao vya juu kwa sababu ya mizengwe, kampeni chafu na tuhuma ambazo mwenyewe aliziita za “kipuuzi” zilizozushwa na wapinzani wake ndani ya chama.

Lakini cha kusikitisha zaidi ni kwa viongozi wa juu Zanzibar kumkataa, wakitaja sababu za kihistoria zisizokuwa na msingi kwa sasa. Kuna hata baadhi walimtuhumu kwa mauaji.

Pamoja na ukweli huwa ni fakhari kwa sehemu ndogo ndani ya Muungano kama Zanzibar kutoa rais wa Jamhuri, viongozi hao walisema, “Kama ni huyu la, endeleeni tu huko Bara kutoa marais, sisi hatuna neno.”

Ni mambo ya kushangaza kwa kweli, na kielelezo tosha cha namna wanasiasa wa CCM wa Zanzibar wanavyoridhia haraka matakwa ya wenzao Bara.

Katika suala la Dk. Salim, kuna baadhi yao walitumiwa na kambi ambayo mgombea wake alishinda ili kumkataa mwanadiplomasia huyo.

Dk. Salim, aliyewahi kuwa waziri wa ulinzi na naibu waziri mkuu wa Tanzania, alipata kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) – sasa Umoja wa Afrika (AU) na akapendekezwa kushika wadhifa kama huo kwa Umoja wa Mataifa.

Siamini kwa mfano katika miaka michache ijayo Zanzibar wanaweza tena kupata mgombea mzuri wa urais kama huyo, na ambaye wenzao wa Bara watamkubali haraka.

Hivyo suala la CCM kuwa na mgombea wa urais kutoka Zanzibar ni kama ndoto tu kwani Rais wa Jamhuri kutoka Zanzibar anaweza kuuvuruga mtandao mzima wa ufisadi uliojipenyeza katika safu za juu ya uongozi uliopo sasa.

Kwa hoja ya mgombea mwanamke, baadhi ya viongozi wa CCM watajaribu kuiingiza katika kile kitakachoelezwa kama kupata mgombea muafaka ili kuepusha mivutano inayoweza kuibuka.

Hali hiyo imeshuhudiwa katika kumpata mgombea wa uspika wa Bunge mwezi uliopita kwani kuwa na Spika mwanamke kamwe haikuwa ajenda ya chama hicho kabla. Ajenda hiyo ilikuja kwa lengo la kutuliza kambi moja yenye kuandamwa na tuhuma za ufisadi iliyopania kumpitisha mgombea wao. Hakuna sababu inayoeleweka kwa nini kulikuwa na umuhimu wa kufanya hivyo.

Ajenda hiyo ilikuwa kitu cha dharura tu, hivyo mtu aweza kusema kwamba Anna Makinda amekuwa Spika kwa bahati tu.

Suala kwa CCM kuwa na mgombea mwanamke nalo ni gumu vilevile na changamoto kubwa itakuwa katika kupata mgombea mwenye nguvu ya kuhimili mikikimikiki ya kampeni kama vile ya Dk. Slaa. Ni nani basi?

Kwa harakaharaka, mtu anaweza kusema kwa kuwa ngome ya kura nyingi za CCM ni wanawake, lakini linapokuja suala la wanawake kumpigia kura mwanamke mwenzao kuwa rais wa nchi ni kitu kigumu kidogo.

Kwanza uchaguzi uliopita umeonyesha kwamba dhana hiyo imeanza kubomoka – wapiga kura wengi wanawake walivipigia vyama vya upinzani, hata vijijini.

Ziko nchi zilizowahi kuwa au zenye marais wanawake kama India, Bangladesh, Ufilipino, Indonesia, Chile na Argentina. Kwa Afrika, ni Liberia pekee hadi sasa.

Katika uchaguzi wa 2008, Wamarekani walionekana kukubali kuwa na rais mwanamme mweusi kuliko mwanamke mweupe – pamoja na ukweli kuwa kuna wapiga kura wengi weupe (asilimia 70) kuliko weusi, na kwamba wapiga kura wanawake ni wengi zaidi kuliko wanaume. Hivyo katika chama cha Democratic, walimteua Barack Obama (mwanamme) kuliko Hillary Clinton (mwanamke).

Na kwa misingi hii naamini mgombea urais mwanamke atakuwa ni gharika kubwa kwa CCM.

 

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: