JK katika mabango, Dk. Slaa mioyoni mwetu


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 27 October 2010

Printer-friendly version
Tafakuri

SIJALI ni nani atakuwa Rais wa nchi hii kesho. Hiki si kitu kinachoninyima usingizi kuliko mwelekeo mzima wa upepo wa siasa ya nchi. Kinachonishangaza ni hicho hapo juu katika kichwa cha habari.

Katika Tanzania ya leo ambayo watawala wetu wanakesha kutabiri umaskini, inashangaza kuona kila kona ina bango la mgombea wa chama tawala. Huyu ni Rais Jakaya Kikweteb aliye madarakani ambaye, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliiingia na kaulimbiu ya Ari Mpya, Kasi mpya na Nguvu mpya alipopishwa kiti cha ikulu mchana ule wa 21 Desemba 2005.

Huyu akashindwa kufanya alichokisema. Umaskini wa Watanzania umewabana katika ngozi na akili. Afadhali ungekuwa katika harufu, lakini uko katika ngozi. Leo mamilioni yanatumika katika kuhakikisha anarudi madarakani.

Ndani ya ‘Keep left’ moja kuna mabango manne. Ndani ya mabango haya kuna gharama za kutoka kwa ‘wanaojipendekeza’ na pia kuna gharama za chama chake, kama si kwa msaada wa serikali anayoiongoza. Swali linaibuka, je, nguvu zinazotumika zinalingana na kukua kwa umaarufu wa mgombea mwenyewe pamoja na chama chake kwa jumla?

Jibu ni hapana. Taratibu Watanzania wanajinasua kutoka katika mtego wa utumwa wa akili. Mtego wa kukubali kuuziwa mbuzi katika gunia. Mbuzi ambaye waliuziwa mwaka 2005 kwa kuambiwa kuwa rais wetu ni ‘Handsome’ kuliko wagombea wengine wa CCM na wale wa vyama vya upinzani.

Leo JK amebaki katika mabango. Moja linamwonyesha akiwa na mwanamuziki Chege, jingine na mlemavu wa ngozi, jingine akapiga magoti kumbusu mtoto mdogo, jingine akiwa na mama yake mzazi…

Lakini pamoja na mabango hayo yote, jina la Dk. Willibrod Slaa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ndilo maarufu zaidi sasa kuliko JK.

Iwe kwa kumsifia au kumkashfu kama wapinzani wake wa siasa, jina la Dk Slaa liko juu, na amepata umaarufu zaidi baada ya kusikiliza alichokisema na si kuangalia sura yake.

Mara kadhaa nimewahi kubahatika kuwepo katika chaguzi za nchi kadhaa za Aafrika. Nilibahatika kuwa Botswana na baadaye Ghana. Hayakuwepo mabango ya vurugu kama haya ya JK na CCM.

Watawala walishinda uchaguzi kwa nguvu ambazo hazikufikia walau robo ya hii ninayoiona kutoka kwa JK. Leo hata JK akishinda, apime nguvu aliyotumia pamoja na ongezeko la umaarufu wa Dk Slaa.

Huu ni mtihani ambao CCM inabidi waupime kwa kina. Ni wakati ambao inabidi wakiendeshe chama chao kisayansi zaidi kuliko kutumia gharama zisizo na msingi. Na hakuna sayansi nyingine zaidi ya kuwaletea watu wao maendeleo.

Nyakati za kuwadanganya Watanzania kuwa rais ana sura nzuri zimepita. Wakiendelea na hadithi hizi za kutuletea rais anayependa kupiga picha na Boyz 11 Men siku zao zitahesabika kwa haraka kuliko utabiri wa Mwalimu Nyerere.

Katika vikao vya kujadili uchaguzi baadaye, CCM lazima wakosoane kutokana na ukweli kwamba sura ya JK haikusaidia kuliko walau kauli za Abdulrahaman Kinana za kukanusha hoja fulani za Dk Slaa.

Na hata katika kuvuta umati wa watu, lazima CCM wajiulize kwa nini walilazimika kutumia zaidi sura za wasanii wa kundi la Original Comedy au mwanamuziki Marlaw.

Akina Jotti waliambiwa wasiondoke kabla ya JK kwa sababu kwa kufanya hivyo umati wa watu ungeondoka na kumwacha akiwa hana watu aliowakusanya kwa malori kutoka wilaya tofauti. Kuna siri gani ndani yake wakati tayari walikuwa na mabango ya Handsome kila kona? Ni swali ambalo inabidi CCM wajiulize.

Kuanzia chaguzi za mwaka 1995, mwaka 2000, kisha mwaka 2005 na huu ambao unafanyika kesho, Watanzania wamekuwa wakibadilika kwa kasi. Ilikuwa rahisi kwa JK kujinadi katika uchaguzi wake wa kwanza kuliko huu.

Ule wa kwanza alionekana mzito, huu wa sasa wamempima tayari na kugundua alivyo mwepesi. CCM
Rais wa Tanzania, bila ya kuzingatia anatoka chama gani, anahitajika kuwa mwanadamu mwepesi wa kutoa maamuzi mazito. Hiki ndicho kinachombeba Dk Slaa.

Sura yake ni kama yangu, lakini anawapa Watanzania ahadi ya kuchukua maamuzi mazito na endelevu.

Vizazi vinasogea na sasa tunawapata watoto kama wale wa Kigoma ambao wako tayari kulala barabarani kwa ajili ya kudai haki zao. Wale na hawa wakichanganyika itakuwa vigumu kuwaambia tumchague Rais wa CCM kwa sababu eti ni handsome.

Tulimchukia Benjamin Mkapa. Mwisho wa siku zama zake tunazikumbuka kwa pande mbili; Uimara wa uchumi pamoja na tabia yake ya kutuambia ukweli katika maamuzi yake mazito. Na sasa tunaamini “U-handsome” wa kazi yake kiuchumi ulikuwa muhimu kuliko ule wa sura yake.

CCM inahitaji kujibomoa na kujipambanua. Inahitaji kujipa sura mpya mbele ya mioyo ya wananchi. ijitoe katika makucha ya mafisadi, wafanyabiashara na iwape wananchi maendeleo. Vinginevyo italazimika kutumia nguvu nyingi katika mabango huku midomoni na mioyoni mwa watu wakiwataja kina Dk Slaa ambao wanaeleweka kwa wanachokiongea na kudhamiria kukitenda.

Kudorora kwa chaguo la CCM ndiyo faida kwa kina Dk Slaa wanaouzika bila ya mabango makubwa barabarani. Kama chama kingekuwa huru, Dk Slaa angeweza kujipambanua ndani ya CCM mwaka 1995.

Lakini kwa vile CCM imeshindwa kujikana, kwa vile imeshindwa kuwakana akina Basil Mramba, Rostam Aziz, Edward Lowassa na wengineo, basi siku zake zinahesabika na kila kukicha kina Dk Slaa wanazaliwa wengi zaidi.

Kwa vile bado CCM inaamini kuwa inaweza kuwa na katibu mkuu mropokaji na kisha ikasonga mbele, bado kina Dk Slaa wengi watazaliwa na CCM itajikuta katika wakati mgumu muda wote.

Bahati mbaya kwa CCM ni kwamba, watu wanamsikiliza na kumwelewa Dk Slaa. Vipi kwa vizazi hivi vipya ambavyo havikuwahi kugusa chama chao? Vipi kwa wale watoto maskauti wa Kigoma?

Ni wakati huo ambapo CCM itakuwa inaweka bango katika kila nyumba ya nchi hii, huku wapinzani wakiitisha mikutano yao kwa meseji za simu tu!

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: