JK: Kombani, Ghasia wa nini?


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 09 May 2012

Printer-friendly version
Tafakuri
Waziri Hawa Ghasia

IJUMAA iliyopita Rais Jakaya Kikwete alifanya kile ambacho wengi hawakutarajia kwamba angekifanya. Hakutarajiwa avunje utamaduni wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuchukua hatua za kuwajibisha wezi na wakosaji wengine katika ofisi za umma.

Inawezekana wapo wanaoamini kwamba Rais amefanya maamuzi magumu, na wanaosifu kwamba kaonyesha njia. Mimi ninatofautiana nao kwa asilimia mia.

Japokuwa ni kweli hatua za kuwawajibisha baadhi ya waliotajwa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Heabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2009/10 zimechukuliwa kwa ngazi ya mawaziri, lakini pia Rais ameonyesha kutokukubali mawaziri watolewe kafara mwaka baada ya mwaka huku watendaji ama ndani ya ofisi za serikali au taasisi zake wakiendelea kupeta na wakati mwingine watendaji hao ndio wahusika wakuu wa wizi na uzorotaji wa mambo.

Pamoja na sifa anazomwagiwa Rais Kikwete katika maamuzi haya ya kuwaweka pembeni mawaziri sita, na kwa kweli akiwa ameanza kuvunja mwiko wa kulindana kwa kiwango fulani, bado sifa hizi zina hitilafu kubwa.

Rais Kikwete alikuwa mtu wa kwanza kupewa ripoti ya CAG kama ibara ya 143 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inavyoelekeza, na angechukua hatua hizi mapema zaidi.

Ingawa ibara hiyo inamtaka Rais kuhakikisha kuwa ripoti ya CAG inawasilishwa kwenye mkutano unofuata wa Bunge si zaidi ya siku saba baada ya kuanza kwa mkutano huo, haisemi kwamba Rais anaipokea tu hataisoma.

Rais anapewa ripoti hiyo ili akiwa mkuu wa muhimili wa utendaji, ajue wasaidizi wake wamefanya nini kuhusu usimamizi wa matumizi bora wa fedha za umma. Ni fursa inayompa Rais nafasi ya kuwatambua wasaidizi wake, kama wanamsaidia kutekeleza kweli majukumu aliyowapa au wanamkwamisha.

Kwa kujua hivyo, Rais hahitaji hata kidogo kusubiri eti wabunge wachachamae, kamati za Bunge za Hesabu ya Mashirika ya Umma (POAC), Hesabu za Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) zichachamae, ndipo ajue ndani ya serikali yake kuna uoza.

Ibara ya 143 (2) inampa Rais faida ya kutambua ndani ya nyumba yake nini kinaendelea kabla ya kuumbuliwa na muhimili mwingine wa madaraka ya dola, kama Bunge au hata na vikundi vingine vya kiharakati.

Kwa bahati mbaya, tangu ripoti ya CAG ya 2009/10 ilipowasilishwa bungeni Aprili mwaka jana, ilimchukua Rais Kikwete mwaka mzima kutafakari na kuchukua hatua dhidi ya wasaidizi wake hadi pale wabunge walipoamua kuwaandama mawaziri wake.

Mwenendo wa Rais wa kuitisha hata Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupata baraka zake ili kuwatimua mawaziri walioshindwa, wezi, wazembe na wenye kila aina ya udhaifu, ni mambo yanayoonyesha wazi kuwa sifa hizi anazomwagiwa sasa hastahili kwa sababu ni kama amesukumwa kuchua maamuzi ambayo kwa kipindi cha mwaka mzima alishindwa kuchukua.

Tunajua vilivyo, hakuna kokote Rais anakowajibika kisheria kutafuta maoni ya CC ya chama chake ambayo hata hivyo yeye ni mwenyekiti wake, kabla ya kufanya maamuzi ya kikatiba. Hakuna.

Kutafuta ushauri huo ama ni kutaka kujiepusha na lawama juu ya maamuzi yake, au ni kutaka kujivua wajibu wa moja kwa moja wa kuwafukuza kazi watu ambao yeye ndiye anawapa kazi kwa utashi wake binafsi.

Kwa hiyo, hali hii inapunguza sifa anazomwagiwa Rais katika maamuzi ya kuwafuta kazi mawaziri sita.

Mbali ya udhaifu huu, wapo mawaziri wawili ambao Rais amewabakisha katika baraza jipya wakati kimsingi walipaswa kuwa nje siku nyingi. Hawa ni aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia aliyehamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu –Tamisemi.

Mwingine ni aliyekuwa Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kimbani aliyepelekwa Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

Ghasia amekuwa Utumishi tangu awamu ya nne iingie madarakani mwaka 2005; lakini kwa miaka yote hiyo ameshindwa kufuta wizi kupitia watumishi hewa ambao kila mwezi wanaigharimu serikali mamilioni ya fedha.

Ripoti ya CAG mwaka baada ya mwaka inaonyesha mishahara kwa wafanyakazi hewa, na rais mwenyewe alikwisha kusema kuwa hali hiyo inamkera. Lakini mwaka baada ya mwaka wafanyakazi hewa wanaendelea kuwa utamaduni wa serikali, mabilioni ya fedha za walipa kodi yanapotea kwa njia hii.

Ugonjwa huu ambao mwaka jana ulihamia hata kwenye vyuo vya elimu ya juu, umemshinda Ghasia. Katika hali hiyo, inakuwa vigumu kujua alichokiona Rais kwa Ghasia hadi akampa mzigo mwingine mzito wa Tamisemi.

Vilevile Ghasia ameshindwa kuboresha ufanisi katika kusimamia sekta ya utumishi wa umma. Huyu mama hana jipya.

Kazi ya Tamisemi aliyopewa ni mzigo mzito wenye kuhitaji mtu madhubuti siyo mwili tu bali pia ubongo unaochemka kutambua changamoto zinazokabili halmashauri mbalimbali nchini ambazo zimekuwa kiota cha ulaji rushwa wa kutisha.

Kuhusu Kombani, kama kweli hatua zimechukuliwa kwa mawaziri wote kulingana na udhaifu wa wizara zao kwa mujibu wa ripoti ya CAG, mtu wa kuwambwa msalabani kwa madudu ya Tamisemi kwa mwaka wa fedha wa 2009/10 hakuwa George Mkuchika ambaye sasa amehamishiwa Ofisi ya Rais Utawala Bora, ila Kombani.

Ndiyo maana Mkuchika ameachwa, lakini na Kombani kaachwa kuendelea kutamba? Kama hatua zimechuliwa dhidi ya madudu yote, haieleweki Kombani anakwepaje “panga.” Kibaya zaidi anapelekwa katika nafsi ya kwenda kusimamia utumishi wa umma.

Kombani hakufanya lolote la maana katika Wizara ya Sheria na Katiba. Huyu aliungana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Fredrick Werema, kukataa kwamba Tanzania ilikuwa inahitaji katiba mpya.

Alisema katiba iliyopo inatosheleza kila kitu na alipuuza wito wa kuwako kwa katiba mpya hadi Rais Kikwete alipoibuka na kuahidi kuwapatia Watanzania katiba mpya.

Hata mchakato wa awali wa kuandikwa kwa sheria kuunda tume ya kuratibu maoni ya wananchi, Kombani aliboronga. Aliwasilisha muswada wa ovyo bungeni ambao uliamsha uasi mkubwa ndani ya nchi.

Hakuishia hapo tu, hata ahadi yake kuwa wananchi wengi zaidi wangehusika kutoa maoni yao juu ya muswada huo hakuitekeleza. Kombani alipwaya katika Wizara ya Sheria na Katiba.

Kwa kuishiwa hoja, aliamua kulumbana na Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu, katika wizara yake wakati wa kupitishwa kwa muswada wa tume ya katiba, badala ya kujenga hoja.

Kombani anashangaza wengi kwamba amebaki vipi katika baraza hili jipya! Kwa mapungufu haya, Rais Kikwete anaonekane amefanya jambo la ajabu katika mabadiliko ya mawaziri.

Ninakaa katika hili kukubali kuwa lipo la kumpongeza, ila ameshurutushiwa, akakosa ujanja wa kukwepa wajibu huu wa lazima.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: