JK: Kura ulizozikataa ni nyingi


Paschally Mayega's picture

Na Paschally Mayega - Imechapwa 19 May 2010

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

RAIS wangu Jakaya Kikwete, ulipohutubia wazee wateule wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa mkoa wa Dar es Salaam 3 Mei 2010 na kusema kwamba kama ni kura za urais utazipata kwa wengine, haraka nilibaini kuwa kumbe bado unautaka tena urais.

Kama hivyo ndivyo, kura moja ni mali sana na hasa katika kipindi hiki ambacho wananchi wengi wameamka.

Kura moja ni mali sana katika kipindi hiki ambacho wananchi wanajua kuwa anayehonga hela ndiye mwizi wao,

Wanachukua hela yake lakini hawampi kura. Wakati huu, ambao wanaokubali kuvishwa fulana za njano na vitenge vya kijani wakati wa kampeni tu wanazidi kupungua, unyenyekevu kwa wananchi ni muhimu kuliko majivuno na majigambo.

Mamlaka umepewa kwa ridhaa ya wananchi. Kuwafokea au kuwatishia kuwaua kwa risasi zao wenyewe ni sawa na kujikana mwenyewe na ni dalili za kushindwa uongozi.

Umedhihirisha machoni mwa wengi kuwa umeishiwa busara hata kidogo.

Kijakazi mimi, laiti ningekuwa mbele ya macho yako, ningekuangukia miguuni mwako na kukuomba uwaangukie, siyo wafanyakazi tu, bali pia wananchi wote wa nchi hii kwa kauli chungu na ya kwanza kusikika tangu taifa hili lipate uhuru!

Mwenyezi Mungu atuepushe na kauli za kuvunja mioyo kama hii ya kwako!

Kura 350, 000, tena uliendelea zaidi kuwa ukichanganya na wafanyakazi wa mashirika ya umma wanafikia 450,000 hizo ni kura nyingi mno. Kuzikosa ni muhali.

Kama hawa 450,000 ni wanaume basi baadhi yao wana wake zao. Kama ni wanawake wana waume.

Fanya kila familia ina watoto wawili wenye haki ya kupiga kura ambao nao watakukataa kutokana na kauli za maudhi na vitisho dhidi ya wazazi wao. Je, mpaka hapa unajua kuwa utakuwa umepoteza kura ngapi?

Wafanyakazi hawa 350, 000 wana watoto wanaowasomesha; wafanyakazi wa ndani na wale wa mashambani. Nao wanafamilia zao. Kwa kauli yako ile, wote hawa umekataa kura zao.

Kuna kura nyingi za wanafunzi wa vyuo vikuu waliolazimishwa kukosa uzalendo kwa nchi yao, nazo umezikataa. Ni kwa sababu wazazi wao umekataa kuwazidishia kipato ili kuweza kulipia karo ya mwanawe.

Fedha hazitoki mpaka kwa migomo na maandamano. Je, uzalendo wa vijana hawa kwa nchi yao utatoka wapi? Wanajiuliza, kama wewe ulisoma bure kwa nini wao uwatoze karo? Wape sababu kama zipo.

Vinginevyo, hii itabaki kuwa dhuluma kwa tabaka la watoto wa masikini itayokuja kulipwa siku moja kama siyo na ninyi watawala wa sasa, basi na watoto wenu.

Vijana wanakaa wiki moja wanasikia uko Bulgaria. Wiki nyingine Uturuki. Halafu Marekani. Baada ya muda mchache, unarejea Tanzania.

Lakini baada ya siku mbili, umerudi tena Marekani. Unaruka utadhani ikulu kuna kunguni. Hatimaye umemaliza dunia yote, hadi Jamaica kwenye bembea.

Rais wangu Kikwete, mwanzoni tuliambiwa kuwa huko majuu, unakwenda kuhemea, lakini kila unaporudi machungu yanazaidi. Kama mawingu yangekuwa yanamwachia rangi yake msafiri wa ndege kama udongo wa Songea ufanyavyo, tayari ungekuwa hukamatiki.

Lakini kuna wengine wengi uliokataa kura zao. Kuna sisi wastaafu unaotulipa Sh. 20,250 (elfu ishirini) kwa mwezi.

Mwana mwema Halima Mdee alisimama kidete bungeni kutulilia sisi wazazi wake. Waziri wa fedha, bila chembe ya soni, tena mbele ya waziri mkuu alisimama bungeni na kusema uongo.

Kwamba eti tulikuwa tunalipwa Sh. 37,500 (elfu thelathini na saba na mia tano) na sasa watatulipa 50,000/= kwa mwezi.

Juzi nilikwenda kuchukua kiinua mgongo changu. Nimelipwa ileile – Sh. 20,250/= (elfu ishirini na mia mbili na hamsini tu.

Hata kwa uongo huu, Spika wa Bunge la Jamhuri Samwel Sitta ameshindwa kumchukulia hatua zozote waziri kwa kulidanganya bunge. Wananchi wanauliza: “Ndugu Sitta, viwango ulivyoahidi viko wapi?"

Rais wangu katika mazingira haya, kura zetu umezikataa. Sasa zitakuwa sawa na lila na fila kamwe hazitangamani.

Tunaposikia rais wetu amekwenda likizo kwenye hifadhi za wanyama katika mahoteli ya kifahari akiandamana na kundi la watu tunaziona fedha nyingi ilizonazo serikali. Lakini kipaumbele chake siyo kuwatumika wananchi, bali furaha na anasa.

Kwa hilo, mama zetu waliozagaa nchi nzima wakiuza vitumbua na maandazi ili angalau wapate wao na watoto wao mlo mmoja, wanaishia kufa njaa.

Rais wangu umezikataa kura za wote wanaoishi kwa kuwategemea wafanyakazi. Wenye daladala wanaumia kuwaona wafanyakazi wakitembea kwa miguu badala ya kupanda mabasi kutokana na hali ngumu.

Pia kura za wenye nyumba waliowapangisha wafanyakazi wanaoshindwa kulipa kodi zao kwa wakati nazo umezikataa.

Kura nyingi zaidi zitakazokukataa wewe ni za Wantanzania uliowaahidi maisha bora, lakini sasa wanashuhudia ugumu zaidi wa maisha.

Wanasema bora ungewaacha na maisha yaleyale uliyowakuta nayo.

Rais wangu, uliposema watakaogoma watapambana na polisi watakaotumia
virungu, mabomu na risasi za moto ndipo ulipofikia hitimisho!

Waliosema ‘Kikwete amechemsha’ waliisema hali halisi. Kauli ya kutamkwa na mtu mwenye moyo mgumu sana kama Iddi Amin au Mobutu.

Kuua wanaodai haki yao! Wale wale waliokuweka hapo! Nyerere aliona mbali!

Vijana wako, yaani mkuu wa majeshi, IGP na wengine walikusikiliza kwa makini. Kauli ile chungu kwao ilikuwa amri.

Hivi kuongea na wazee wako, mpaka na wakuu wote wa majeshi wawepo? Ulikuwa unatangaza vita?

Unatisha watu! Viongozi waliolazimika kuzikimbia nchi zao hawakuwa na majeshi na bunduki za moto? Walikuwa navyo lakini utaua wangapi?

Wananchi sasa wanayakumbuka maneno ya Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye aliposema, “Mtu yeyote anayeitafuta Ikulu kwa pesa nyingi, akifika atasafisha njia kwa mtutu wa bunduki.” Hayo yametimia.

Oh! Sumaye, wananchi sasa watayakumbuka maneno yako nukta kwa mkato. Uliona mbali.

Anney Anney mlemavu aliyetupwa jela kwa kulililia Azimio la Arusha aliniambia kuwa serikali yetu hivi sasa imekuwa sawa na mbwa aliyekosa pua.

Mungu asaidie sauti hii imfikie Anne Kilango Malecela kama alibakiza baiskeli moja ya miguu mitatu baada ya kumpatia yule mlemavu mwingine, ampatie na huyu imsaidie kuendea kwenye kesi yake!

Mbwa ana macho na masikio lakini maisha yake yanategemea uwezo wa pua yake kunusa. Serikali hainusi hatari inayolikabili taifa kwa kauli na vitendo vyake.

Watakaogoma watafukuzwa waajiriwe wengine. Hao wapya wataishi kwa kula upepo? Kinachoshindikana kuwaita vijana wako wa TUCTA ukaongea nao wewe mwenyewe ni nini?

Hasira hasara! Hasira haijawahi kujenga popote. Sasa umevunja kabisa daraja la mawasiliano kati yako na wafanyakazi! Kati yako wewe na wananchi wanaoitaka amani.

Ni kura kiasi gani umezikataa kwa hotuba ile? Kinywa kiliponza kichwa!

Rais wangu kura za mawaziri, wabunge, wakuu wa mikoa na wilaya na hawa wazee wa CCM wa Dar es Salaam pekee zitatosha kukurudisha Ikulu?

Kama utapita kwa ‘Simple majority’ wewe utakuwa rais wa kwanza Tanzania kuchaguliwa na watu wachache.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: