JK na miaka mitano ya kusononeka Ikulu


Isaac Kimweri's picture

Na Isaac Kimweri - Imechapwa 01 December 2010

Printer-friendly version
Tafakuri

RAIS Jakaya Kikwete amekwisha kukamilisha kwa takriban asilimia 85 ya kazi ya kuuda serikali yake. Tayari ameteua mwanasheria mkuu wa serikali; waziri mkuu; mawaziri na manaibu wao.

Kwa maana hiyo, nafasi ambazo aghalabu hupata wateule wapya kila baada ya uchaguzi (nafasi za kisiasa) zilizobakia ni wakuu wa mikoa na wilaya.

Nafasi za wakuu wa mikoa zilizo wazi kwa sasa ni pamoja na Dar es Salaam uliokuwa unaongozwa na William Lukuvi, sasa waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Kilimanjaro uliokuwa unaongozwa na Monica Mbega aliyeangushwa kwenye ubunge Iringa Mjini, na Dk. James Msekela, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma aliyeangushwa Tabora Kaskazini.

Pia kuna nafasi za wakuu wa wilaya ziko wazi baada ya wengine kujitosa kwenye ubunge na ama kushinda au kushindwa.

Kwa maana hii, kama kuna ulazima wa kuendelea na uteuzi kwa sasa nafasi za kutazamwa ni za wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, ingawa kwa sasa si lazima sana. Itoshe tu kusema kuwa Rais Kikwete anaweza kuendesha serikali yake kwa uteuzi ambao amekwisha kuufanya.

Ingawa ushindi wa Rais Kikwete unampa fursa na haki kisheria ya kuunda serikali kikatiba, bado kuna jambo moja ambalo litamsononesha katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Mwaka 2005 Rais Kikwete alishinda uchaguzi kwa takribani asilimia 82, mwaka huu ameshinda kwa asilimia 61 hivi; yaani amepoteza asilimia 20.

Hiki ndicho kitu kitakachomuumiza Rais Kikwete kwa miaka mitano ijayo, kwamba hiyo asilimia 20 na ushei imekwenda wapi?

Lakini kingine kinachofanana na hicho, ni kwamba hata hiyo asilimia 61 inapopimwa kwa idadi yote ya wapiga kura walioandikishwa yaani watu 20.2 milioni, kiwango cha waliopiga kura ni asilimia 42.

Kwa maana hiyo, waliomchagua Kikwete ni asilimia 27 hivi. Kwamba rais amepigiwa kura na asilimia 27 ya wapigakura wote, ni kitu kingine kitakachomsononesha rais kwa miaka mitano ijayo.

Lakini msononeko huu una kitu kingine kikubwa ndani yake; hiki ni aina ya kampeni alizofanya Rais Kikwete katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Kwanza, tangu siku ya kwanza ya kuchukua fomu ya kuwania urais kwa muhula wa pili, Rais Kikwete alifanya kosa la kiufundi kwa kumkabidhi mwanaye Ridhiwani, mkoba wenye fomu zake ili azitembeze nchi nzima kusaka wadhamini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ridhiwani alichukua wajibu huo na kuungana na baadhi ya viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UV-CCM) kutembea nchi nzima kusaka wadhamini.

Uamuzi wa kumpa mwanaye fomu uliopohojiwa, Kikwete alisema hiyo ilikuwa kazi binafsi na kwa maana hiyo alikuwa sahihi kumpa mwanaye kwa kuwa alimwamini. Hapa ndipo alipoanza kile Wazungu wanachosema ‘goof’ kwa Rais.

Aligeuza suala la urais kuwa la binafsi, alibinafsisha harakati hizo wakati yeye mwenyewe hadi anachukua fomu hizo alikuwaakijua fika alikuwa taasisi ya umma. Ni taasisi kwa sababu alikuwa bado Rais, lakini pia alikuwa Mwenyekiti wa CCM, na mbaya zaidi CCM, kiutaratibu hairuhusu rais aliyeko madarakani anayetaka kutetea kiti hicho kupingwa au kushindanishwa na yeyote.

Kikwete alikuwa taasisi. Lakini hili kwa bahati mbaya alishindwa kuliona, matokeo yake kulikuwa na aina fulani ya kususa kwa watu wa ndani ya chama chake.

Ndiyo maana katika mikutano yake mingi nguvu ya fedha ndiyo ilionekana zaidi ikitenda kazi kuliko utashi na kujituma kwa watu kwa maana ya kumuunga mkono kwa dhati kabisa, tofauti na mpizani wake aliyekuwa hana nguvu nyingi si za dola wala za fedha kama zake.

Pili, katika kosa la kiufundi, ni kuruhusu familia yake kwa maana watoto na mama yao, nao kujitumbukiza kwenye kampeni, kuchukua mstari wa mbele, kana kwamba walikuwa wanasaka mitaji ya kampuni yao, wakajitumbukiza kusaka kura kwa niaba ya Rais ambaye alikuwa taasisi.

Mwenendo huu mpya wa kisiasa kwa Kikwete, ulizua maswali mengi si nje ya CCM tu, bali hata ndani yake; ingawa watu wa ndani walikosa ujasiri wa kuhoji moja kwa moja.

Walichofanya wengi wao ilikuwa kukimbiza ubawa wao au vidole vyao ili wasiungue. Hali hii ilikuja kujitokeza kwenye hesabu ya kura.

Tatu, aina ya rasilimali ambazo safari hii Kikwete alitumia ni kubwa kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na mwaka 2005. Kulikuwa na mabango mengi na makubwa mno barabarani kila kona ya nchi.

Kulikuwa na vipeperushi vya kila aina vya kujitangaza; kulikuwa na opena za chupa zilizokuwa na nembo ya CCM, ambazo ikifungua kizibo cha chupa, inaimba nyimbo za kumsifu na kumkapenia Kikwete.

Opena hizi zilimwagwa kwenye baa; kulikuwa na raba (viatu); kulikuwa na fulana na kofia za kila aina; kulikuwa na vipindi vya redio na televisheni; kulikuwa na makala na picha kwenye magazeti.

Pia kulikuwa na helikopta tatu safari hii tofauti na mwaka 2005 ambapo CCM haikutumia kabisa helikopta ikidai ni gharama katika kampeni zake.

Kulikuwa na misafara saba tofauti, ulikuwako wa mgombea mwenyewe, yaani Rais Kikwete na wasaidizi wake; kulikuwa na wa mgombea mwenza, Dk. Mohamed Gharib Bilal; kulikuwa na wa kkewe, Salma; kulikuwa na wa mwanaye Ridhiwani na marafiki zake; kulikuwa na wa uongozi wa juu wa UVCCM ambao ulijigawa mara mbili; pia kulikuwa na mgombea urais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, ambaye hakusita kumwombea Rais Kikwete kura kwa upande wa Zanzibar.

Misafara yote hii iligharimu fedha nyingi, kama posho za wajumbe, magari ya kuwasafirisha kuandaa majukwaa ya kuhutubia, kugawa vipeperushi na mabango mengi, kurusha mikutano hiyo moja kwa moja kwenye redio na televisheni.

Kwa kifupi, itoshe tu kusema gharama za kampeni za Rais Kikwete mwaka huu haziwezi kwa vyovyote kulinganishwa na zile za mwaka 2005; safari hii fedha nyingi ajabu zilitumika.

Tatizo linalojitokeza mara tu baada ya nguvu kubwa kiasi hicho kuitumika, ni aina ya mavuno aliyopata Rais Kikwete. Swali linalomsumbua kwa sasa ni wapi ‘ali-goof’.

Je, ni mwendelezo wa makundi ndani ya CCM?. Je, ni hasira za wale waliokosa kuteuliwa kokote si kwenye uongozi wake wa miaka mitano au kugombea ubunge au udiwani? Je, ni hasira za wanamtandao ambao wanamini wameenguliwa baada ya kazi ya mwaka 2005 au ni uamuzi wa Rais kudhani mradi wa kusaka urais ni wa kifamilia zaidi kuliko wa kitaasisi?

Haya ni maswali magumu na mazito ambayo Rais Kikwete anaingia nayo Ikulu, atakaa nayo pale Ikulu Mungu akimjalia afya njema hadi 2015, lakini zaidi sana akifikiria kama angekuwa na nafasi tena ya kuomba kura angepitia nje tofauti na hiyo aliyotumia? Kwa vyovyote atakavyowaza bado majibu hatakuwa nayo!

Ndiyo maana yote aliyofanya Rais Kikwete kusaka kura akitazamia ushindi wa kishindo sasa amethibitisha pasi na shaka yoyote kwamba kishindo hakikutokea badala yake yakawepo madai ya uchakachuaji wa kura. Katika mazingira kama hayo, analo moja tu, kuishi maisha ya kusononeka wakati alipaswa kufurahia zaidi.

Mtangulizi wake, Benjamin Mkapa mwaka 1995 aliingia kama dhalili, akipata asilimia 61.8, lakini mwaka 2000 alipata kura asilimia 71.7, alikuwa amekubalika, ameungwa mkono na kwa kweli alikuwa amefanya kazi. Mwaka 2000 hali akijua kwamba alikuwa na uwezo wa kuwaita ndugu na familia yake wamfanyie kampeni, hakufanya hivyo, alijua urais ni taasisi ama kupitia chama au timu iliyoundwa kitaifa kufanya kazi hiyo.

Ni kwa njia hiyo Mkapa alikaa Ikulu awamu yake ya pili akiwa na raha bila sononeko moyoni.

Hili ni somo kwa wote kwamba urais ni taasisi, hata kama mtu ana umaarufu wa kiwango gani, bila kuzingatia hilo makubwa yanaweza kumkuta wakati na saa yoyote. Kila la kheri JK na sononeko lako.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: