JK, ni kazi kuficha uongo


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 12 February 2011

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

RAIS Jakaya Kikwete, Jumamosi iliyopita, alitoa hotuba aliyolenga kujitakasa kutoka kwenye sakata la kampuni ya kufua umeme ya Dowans.

Akihutubia katika kilele cha maadhimisho ya miaka 34 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mjini Dodoma, Rais Kikwete alisema hawafahamu wamiliki wa kampuni ya Dowans, hajawahi kuwaona, hana hisa wala uhusiano nao.

Halafu akasema na yeye ni miongoni mwa watu ambao wanataka Dowans wasilipwe tuzo ya Sh. 94bilioni waliyoshinda katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC) na kwamba ameagiza wanasheria wapambane vilivyo kortini.

Inawezekana Rais Kikwete hajadanganya ila hajasema ukweli. Serikali yake haina nia thabiti ya kushinda kesi hiyo.

Kwanza ni namna walivyong’ang’ania kampuni moja ya uwakili katika sakata hili. Kampuni hiyo ndiyo ilitumika kuhalalisha mkataba wa Richmond halafu ikatumika kushauri uvunjwe na ndiyo ilitumika kutetea maslahi ya TANESCO.

Pili ni namna alivyoachia kikundi kidogo cha mawaziri ‘kuhodhi’ suala hilo.

Tatu, kama Rais angekuwa na nia thabiti suala hili lingekuwa limemalizika mapema kabla ya kuisababishia aibu serikali yake mwaka 2008.

Rais hasemi kweli kwa sababu Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja aliwataja wamiliki hao. Kama hawajui, kwa nini hajahangika kutumia polisi au Usalama wa Taifa au polisi wa kimataifa ‘Interpol’ kujua undani wa kampuni iliyoiweka mfukoni serikali yake?

Hata akikwepa, akiruka, akifunika mzimu wa Dowans utamwandama hadi ukweli ujulikane.

Ukweli

Rais Kikwete anajua mchango mchafu wa serikali yake katika kuipa mkataba kampuni ‘feki’ ya Richmond. Badala ya kuipa mkataba kampuni yenye uzoefu na uwezo kifedha, serikali yake iliisaidia fedha kampuni hiyo ambayo usajili wake Marekani una utata.

Kamati Teule ya Bunge iliyokwenda Marekeni kufuatilia uhalali wake, ilirudi na majibu kwamba haipo ‘kisheria’ na haikutimiza taratibu za kisheria kujisajili.

Lakini mmoja wa majaji wa ICC anayetoka Marekani, alidai kuwa kampuni hiyo ipo isipokuwa inatumia jina la kibiashara badala ya jina halisi. Kisheria nani yuko sahihi, ICC au Kamati Teule ya Bunge?

Baada ya serikali kuumbuka, kwa Richmond kushindwa kazi, serikali ikafanya kosa jingine la makusudi; haikuita upya kampuni nyingine, zipitie mchakato unaoeleweka kupata zabuni. Ghafla ikadai Richmond imerithisha mkataba wake kwa Dowans.

Kwa nini serikali inayodai inachukia ‘uswahiba’ iliipatia Dowans mkataba katika mazingira ya kujuana? Hivi kazi ya serikali ni kufua umeme au kusimamia sera?

Unyoofu

Mtangulizi wake Benjamin Mkapa alikana ‘akameza moto’ kwamba haijui kampuni ya ANBEN. Yako wapi?

Hicho ndicho kitamkuta Rais Kikwete ambaye ametoka kivyake.

Baada ya serikali yake kusema Katiba haitafanyiwa marekebisho, yeye aliibuka na ‘kupata ujiko’ aliposema kwamba ataunda kamati ya kuhuisha Katiba iliyopo.

Vilevile, baada ya kikao cha Kamati Kuu ya CCM (CC), Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi, John Chiligati alisema CC imeagiza serikali iilipe Dowans kwa vile “sisi ndio tuliokiuka makubaliano”.

Siku mbili baadaye, wabunge wa CCM katika semina yao, walipinga serikali kuilipa Dowans huku kukiwa na msuguano mkali kati ya mawaziri watiifu kwa ulaji wa Dowans na wasio na chao.

Ijumaa iliyopita, Katibu mkuu, Yusuf Makamba alisema ni ruksa kwa mwanachama yeyote anayetaka kuhama chama hicho kupinga uamuzi wa kuilipa Dowans.

Makamba alisisitiza CCM haiwezi kurudi nyuma juu ya uamuzi wa kuilipa kampuni hiyo hata kama gharama yake itakuwa kukimbiwa na wanachama.

Sasa Rais Kikwete anaposema, “Maamuzi yaliyofanywa na Kamati Kuu ya CCM na Kamati ya Wabunge wa CCM yalifanywa chini ya uongozi wangu. Ni uthibitisho tosha wa ukweli huu…”

Ukweli upi? Ule unaosisitizwa na Chiligati na Makamba au huu kwamba yeye ni miongoni mwa wanaopinga Dowans kulipwa? Kwa hiyo ameukana msimamo wa CC na serikali yake?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: