JK: Ruksa Lowassa kuhama


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 16 May 2012

Printer-friendly version
Lowassa na Rais Kikwete

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete amewataka wanachama wote wa chama hicho wanaoona hakikaliki, kuhama badala ya kubaki wakilalamika.

Kikwete ametoa kauli hiyo ndani ya kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kilichomalizika mjini Dodoma juzi usiku.

Kauli hiyo ya Rais Kikwete imekuja siku chache baada ya Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa kukaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa tatizo la CCM ni uongozi.

Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara  eneo la Mto wa Mbu ndani ya jimbo lake la Monduli, Lowassa alisema kuwa ingawa CCM ina misingi ya kutetea wanyonge, ina tatizo la uongozi na utendaji.

“Pamoja na uzuri wake, muundo wa chama chetu ni mzuri sana, imani ya chama chetu ni nzuri sana, misingi inayoongoza chama chetu ni mizuri sana, lakini tuna tatizo la utendaji na uongozi ndani ya chama chetu,” alisema Lowassa.

Mmoja wa wajumbe wa kikao hicho cha NEC ameiambia MwanaHALISI kwamba kauli hiyo ndiyo inaonekana ilimchochea Rais Kikwete kusema kuwa “kama kuna wanachama wanaoona viongozi wa chama hawafai, au chama hakitekelezi vema majukumu yake wana haki ya kuondoka”.

Kikwete amewataka wanachama hao, badala ya kubaki wanatishia kuhamia kwenye vyama vya upinzani, ni bora wakahama haraka kwenye chama hicho.

Katika mkutano wake, Lowassa alisisitiza, “Siku CCM inaacha kutetea wanyonge mimi si mmoja wao.”

Aliulaumu uongozi wa chama hicho kwa ama kuchelewa kufanya maamuzi, kufanya maamuzi yasiyo sahihi au kutochukua hatua kwa matatizo yanayowakabili wananchi kwa wakati muafaka.

Lowassa alieleza kuwa matatizo hayo ndiyo yanayowafanya watu wakichukie chama hicho na kukiona kuwa ni kero kwao hivyo kutafuta mbadala wake.

Lowassa ambaye amekuwa miongoni mwa wanachama wanaoshinikizwa kujiuzulu nyadhifa zake kutokana na jina lake kuhusishwa na tuhuma za ufisadi, alitaja misingi mitano ambayo inamfamnya aendelee kuwa mwana CCM.

  • Moja ni kwamba ni chama kinachotetea wanyonge. Umoja na mshikamano
  • Raia wa kawaida analindwa katika kupata na kufaidi rasilimali za nchi dhidi ya matajiri na wawekaji wa nje.
  • Kuna mfumo unaowezesha watu kujisahihisha... “Ndani ya CCM kuna vikao, kuna taratibu za vikao, kuna kufukuzana na kuonyana.
  • Pia ndani ya CCM kuna haki za msingi za mwanachama za kupiga kura au kupigiwa kura.

Lowassa alisema kitendo cha viongozi kushindwa kushughulikia kero ndiyo mwanzo wa chama hicho kuparaganyika kwa kuwa watu wanatafuta mbadala wa kero zao na matatizo yao.

Kauli hiyo ya Lowassa iliamsha hasira za Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama ambaye alimtaka azungumzie matatizo yanayolikabili jimbo lake badala ya kufanya mikutano ya hadhara kukiponda chama.

Mukama amesema si sahihi kwa Lowassa kutoa kauli hiyo kwenye mikutano ya hadhara wakati anajua bayana taratibu za chama hicho.

Amesema Lowassa alipaswa kuzungumzia matatizo ya jimbo lake yakiwemo migogoro ya ardhi, wawekezaji na wananchi, wakulima na wafugaji, maji na kero nyingine mbalimbali na si kukishambulia  CCM.

Kwa mujibu wa Mukama, kama Lowassa amebaini matatizo ya uongozi ndani ya CCM, alipaswa kuyazungumzia ndani ya vikao vya chama kwa sababu ana mamlaka ya kukosoa au kurekebisha.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa CCM Monduli, Ruben Olekuney ameibuka na kusema kwamba Mukama amekurupuka kumjibu Lowassa.

Olekuney amesema Lowassa alikuwa akizungumzia uongozi wa chama hicho eneo la Mto wa Mbu na si wilaya, mkoa au taifa.

Amesema ni kweli kulikuwa na udhaifu kwenye uongozi wa kata na wamechukua hatua kwa kumpa onyo diwani wa eneo hilo kwa kutoa vibali vya ardhi bila ya kufuata taratibu zilizopo.

“Kwa kweli Mzee Mukama anatakiwa kwanza asome maudhui ya yale aliyosema Edward, siyo kukurupuka, huku,” amesisitiza.

Katika kikao hicho, pia matokeo ya uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki yalijadiliwa na kubainika kuwa kilichosababisha chama hicho kushindwa ni makunndi ndani ya chama.

Kuhusu uchaguzi huo, ilielezwa kuwa chama hicho kiliathiriwa na makundi na kusababisha kiti hicho kwenda kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Vyanzo vya habari zimeeleza kuwa iliamuliwa kwamba kamati kuu ikutane na makundi yaliyohusika kila moja kwa wakati wake ili kufatuta suluhu na kuyapatanisha.

Suala jingine lililojadiliwa ni ugumu wa hali ya maisha ambapo baada ya kupata ripoti za ahali ya uchumi, ilibainika tatizo ni bei ya mafuta ambayo ilielezwa kuwa chama hicho hakina uwezo nayo.

Kuhusu bei za vyakula, kikao hicho kilielezwa kuwa serikali itatoa chakula kutoka katika maghala yake na kukisambaza kwa lengo la kudhibiti bei ya nafaka.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: